HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 22, 2021

RC RUKWA AKERWA NA MIMBA ZA UTOTONI

 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ameagiza Wakuu wa Wilaya za mkoa huo kuhakikisha wanafuatilia na kudhibiti kuongezeka kwa wanafunzi wa kike wanaokatisha masomo kutokana na tatizo la mimba.

Akizungumza juzi (19.11.2021) mjini Sumbawanga Mkuu huyo wa Mkoa alionesha kutofurahishwa na kasi ya kuongezeka kwa wanafunzi wa kike wanaoshindwa kukamilisha masomo yao sababu ikitajwa kuwa ni kupata ujauzito.

“Lazima tuongeze mapambano kudhibiti mimba za utotoni .Sijafurahishwa kuona wilaya ya Nkasi ikiwa na idadi ya wanafunzi Ishirini Tano (25) mwaka huu waliopata mimba wakiwa wanasoma. Hii haikubaliki. Wakuu wa wilaya nendeni mkadhibiti vitendo hivi” alisisitiza Mkirikiti.

Takwimu za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa zimeonesha kuwa katika mwaka huu 2021 wilaya ya Nkasi imekuwa na matukio 25 ya wanafunzi wa kike kupata mimba huku wilaya ya Kalambo ikiripoti wasichana wanane (8) na Wilaya ya Sumbawanga nayo ikiwa na wanafunzi wanane (8).

Mkirikiti aliagiza pia Maafisa Elimu Kata kutimiza majukumu yao kwa kufuatilia walimu na watu wanaojihusisha na kuwapatia mimba wanafunzi kwani zipo taarifa baadhi ya walimu wanahusika na vitendo hivyo kinyume na maadili ya kazi.

“Maafisa Elimu Kata mmepewa pikipiki na serikali ili zitumike kutekeleza majukumu ya kusimamia elimu kwenye mashule ikiwemo kufuatilia wazazi na walezi wasiolea watoto wao hatua inayopelekea baadhi ya watoto wa kike kupata mimba na watoto wengine kuacha shule bila sababu” alisitiza Mkirikiti.

 Aidha, Mkirikiti amemwagiza Afisa Elimu Mkoa wa Rukwa Samson Hango kuhakikisha timu anayoingoza inajipanga kuchukua hatua kali za kinidhamu na kisheria kwa walimu wote wanaoshabikia mimba za utotoni kwenye maeneo yao.

Katika hatua nyingine Mkirikiti ameagiza vijana wa skauti kote mkoani Rukwa kutumika na halmashauri kubaini wazazi wanaotekelekeza watoto na kusababisha wahamie mitaani na kuitwa ’watoto wa mtaani’ ambao wanazidi kuongezeka hususan Manispaa ya Sumbawanga.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba alisema atahakikisha anashirikiana na vijana hususan skauti kufundisha vijana umuhimu wa maadili mema ili waweze kuwa raia wema na kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi.

Waryuba aliongeza kusema jamii inatakiwa kuelimishwa juu ya umuhimu wa uzalendo hatua itakayosaidia kuwa na jamii bora itakayochukia maovu ikiwemo rushwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Mkirikiti akiongea na wanafunzi wa shule ya sekondari Kirando wilaya ya Nkasi kwenye moja ya ziara zake kuhamasisha elimu .
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akiongea na vijana wa skauti mjini Sumbawanga jana ambapo alikemea kuongezeka kwa matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike mkoani humo.
 Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba akiongea kwenye kikao cha skauti na Mkuu wa Mkoa jana mjini Sumbawanga ambapo alisema atakashirikiana nao kutoa elimu ya kuchukia vitendo viovu ikiwemo rushwa na mimba za utotoni.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (kulia) akiwa na Katibu Tawala Mkoa huo Denis Bandisa (kushoto) jana wakati wa kikao na vijana wa skauti ambapo aliagiza Wakuu wa Wilaya za Nkasi, Kalambo na Sumbawanga kuchukua hatua za kudhibiti vitendo vya wanafunzi wa kike kupata mimba na kushindwa kuendelea na masomo.


 

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad