HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 26, 2021

MAJALIWA ATEMBELEA KAMBI YA TEMBO WORRIORS

RAIS Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi milioni 150 kwa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa wenye ulemavu, Tembo Warriors, inayoendelea na maandalizi ya kufuzu Kombe la Dunia kupitia michuano ya Afrika (Canaf) itakayofanyika jijini Dar es Salaam, kuanzia kesho ambapo Tanzania ni mwenyeji.

 

“Mhe Rais anafahamu mko hapa mnajiandaa kuipigania nchi na amesema nije hapa kwa niaba yake na ametoa kiasi cha shilingi milioni 150 ili kuwawezesha mfanye vizuri zaidi. Simamieni vizuri fedha hizi na mhakikishe zinatumika kama ilivyokusudiwa.”

 

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Novemba 25, 2021) baada ya kutembelea kambi ya wachezaji wa timu hiyo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. “Viongozi na Watanzania kwa ujumla tuna imani kubwa na timu yetu tunaamini mtafanya vizuri na sisi tutakuja hapa kuwaunga mkono”.

 

Naye, mlezi wa timu hiyo  Mheshimiwa Riziki Lulida ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya maandalizi amesema kwa kuwa Tanzania ni mwenyeji wa mashindano hayo ambayo yatajumuisha timu kutoka nchi 15 za ukanda wa Afrika, ni vyema timu hiyo ikaungwa mkono ili kufanya vizuri na kuwa miongoni mwa timu nne zitakazofuzu katika michuano ya dunia.

 

Mheshimiwa Riziki ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kutoa fedha hizo na ameahidi kuwa watazitumia vyema ili kuhakikisha timu hiyo inashinda na kuleta heshima kwa Watanzania na hatimaye iweze kufuzu kushiriki michuano ya kimataifa.

 

Kwa Upande wake, nahodha ya timu hiyo, Steven Manumbu, pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia pia ametoa ahadi kuwa watajitahidi kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano hayo ili waweze kushiriki katika mashindano ya dunia ya michezo ya Walemavu.

 

Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Kazi, Ajira, Vijana  na Walemavu, Mhe. Jenister Mhagama, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Mabeyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu-Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda, na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa wenye ulemavu  (Tembo Worriors ) wakati alipotembelea kambi ya timu hiyo kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Mkoani Dar es salaam Novemba 25, 2021. Timu hiyo inajiandaa na michuano ya kufuzu  Kombe la Dunia kupitia michuano ya Afrika  mwaka 2021 yanayotarajiwa kufanyika Dar es salaam kuanzia kesho na Tanzania ni Mwenyeji wa michuano hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa wenye ulemavu  (Tembo Worriors ) wakati alipotembelea   kambi ya timu hiyo kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Mkoani Dar es salaam, Novemba 25, 2021. Timu hiyo inajiandaa  na michuano ya kufuzu  Kombe la Dunia kupitia michuano ya Afrika  mwaka 2021 inayotarajiwa kufanyika Dar es salaam kuanzia kesho na Tanzania ni Mwenyeji wa michuano hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 

Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa wenye ulemavu  (Tembo Worriors) wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipotembelea kambi ya timu hiyo kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Mkoani Dar es salaam, Novemba 25, 2021. Timu hiyo  inajiandaa  kufuzu  Kombe la Dunia kupitia michuano ya Afrika  mwaka 2021 inayotarajiwa kufanyika Dar es salaam kuanzia kesho na Tanzania ni Mwenyeji wa michuano hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad