Benki ya CRDB kukopesha TZS 460 bilioni miradi ya kilimo na teknolojia zinazolinda mazingira - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 2, 2021

Benki ya CRDB kukopesha TZS 460 bilioni miradi ya kilimo na teknolojia zinazolinda mazingira

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Uwezeshaji Miradi inayozingatia Mabadiliko ya Tabianchi (GCF), Yanick Glémarec wakati wa Mkutano wa 26 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) unaofanyika katika mji wa Glasgow, Scotland.
 
 ========   ========   ========

Benki ya CRDB, taasisi ya fedha inayoongoza Tanzania imetenga dola 200 milioni za Marekani (sawa na TZS 459.9  bilioni) kufanikisha miradi ya kulinda mazingira nchini.

Mkopo huo wa aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki, unajumuisha dola 100 milioni (TZS 230 bilioni)  zilizotolewa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kutunza Mazingir (GCF) pamoja na kiasi kama hicho kilichotengwa na benki ikilenga kuwanufaisha zaidi ya watu milioni sita wanaojihusisha na sekta ya kilimo nchini.

CRDB ni benki ya kwanza ya biashara kutambuliwa na GCF kuwa taasisi ya fedha itakayokopesha mikopo ya utunzaji mazingira ukanda wa Afrika Mashariki na ya nne barani Afrika. Inaungana na taasisi nyingine kufanikisha uwekezaji unaokusudia kutunza mazingira Afrika na kusaidia utekelezaji wa miradi na mikakati ya kutunza na kulinda mazingira nchini. Benki ilitambuliwa na mfuko huo tangu mwaka 2019 baada ya kufanyiwa tathmini ya kina kujiridhisha na uwezo na utayari wake kufanikisha miradi ya utunzaji mazingira.

Oktoba 7, 2021 Bodi ya GCF iliidhinisha mradi wa Programu ya Matumizi ya Teknolojia Endelevu za Kilimo Tanzania (TACADTP) ulioombwa na kuwasilishwa na Idara ya Mikopo Endelevu (SFU) iliyopo chini ya Kurugenzi ya Maboresho ya Biashara yenye jukumu la kuongoza mabadiliko ndani ya Benki hii iliyoorodheshwa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE). 
 
Ombi hilo liliwasilishwa likiwa sehemu ya mkakati endelevu wa Benki unaokusudia kuipa nafasi ya pekee katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kulingana na Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG).
 
Balozi wa Tanzania Uingereza, Dkt. Asha-Rose Migiro akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika katika mji wa Glasgow, Scotland. Benki ya CRDB ni mdau wa Umoja wa Mataifa kupitia Mfuko wa GCF ambao unalenga katika uwezeshaji wa miradi ya maendeleo ambayo inazingatia mabadiliko ya tabianchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kuidhinishwa fungu hilo kunaongeza msukumo wa benki kutekeleza lengo namba 13 la SDG  linalosisitiza kuchukua hatua katika kuyalinda mazingira.

“Afrika ndio mwathirika mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi ingawa inachangia kidogo kwenye uchafuzi wa mazingira. Tunataka tuongoze katika vita hivi vya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuhamasisha miradi na shughuil zinazolinda mazingira na hii ndio sababu ya msingi iliyotufanya tushirikiane na GCF," alisema Nsekela.

Katika kutekeleza Programu ya Matumizi ya Teknolojia Endelevu za Kilimo Tanzania,  Benki ya CRDB inakusidia kutoa mikopo nafuu itakayowawezesha wakulima hasa wa vijijini kuboresha shughuli zao pamoja na kuimarisha kipato. Mikopo hiyo inalenga kusaidia na kurahisisha matumizi ya teknolojia rafiki za kukabiliana na uchafuzi wa mazingira maeneo ya vijijini.

“Kuhakikisha tunakwenda sawa, tumeingiza vigezo na viwango vya masuala ya mazingira, jamii na utawala katika mfumo wetu wa biashara Ili shughuli zetu zote zilingane na matarajio ya utekelezaji wa SDG," amesema Leo Ndimbo, mkurugenzi wa idara ra maboresho ya biashara wa Benki ya CRDB.

Programu hii itaiwezesha Benki ya CRDB kubuni namna nzuri zaidi za kuiwezesha miradi ya kilimo pamoja na wakulima wenyewe kutumia teknolojia za kisasa zaidi kwa mazingira ya Tanzania kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na changamoto nyingine za mazingira pamoja na kuongeza tija.

"Hii programu itasaidia kuimarisha sekta ya kilimo nchini kwa kuwezesha upatikanaji wa teknolojia bora. Hili litawezekana kwa kuanza kutoa mikopo itakayozifanya teknolojia hizi ziwe nafuu kwa wakulima wetu nchini pamoja na kampuni zinazojishughulisha na kilimo pamoja na msaada wa kiufundi kutoka kwenye mamlaka za Serikali,” alisema Meneja Mwandamizi wa Mikopo Endelevu, Kenneth Kasigila. 
Kasigila alifafanua zaidi kwamba mikopo hiyo pia itasaidia kuongeza uelewa wa viashiria vya hatari vya kimazingira na hatua za kuchukua kukabiliana navyo miongoni mwa wadau muhimu wanaojumuisha Serikali, wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya kilimo pamoja na seta ya fedha.

Kwa zaidi ya miaka 20 sasa ya kuwepo kwake, Programu ya TACATDP inakusudia kuwafikia wanufaika wa moja kwa moja zaidi ya milioni 1.2 na wasio wa moja kwa moja zaidi ya milioni 4.9 (sawa na asilimia 4.67 ya watu wote nchini) kwa kuwapa mikopo itakayowasaidia kukabiliana na changamoto za kimazingira kwenye sekta ya kilimo.

Programu hiyo itakayozinduliwa mapema mwakani, inakusudiwa kuongeza uwezo wa Tanzania kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha rutuba ya udongo, kupunguza gharama za kilimo na uzalishaji wa hewa ya ukaa pamoja na kuimarisha upatikanaji na usimamizi wa vyanzo vya maji.  
 
Vilevile, itasaidia kupunguza kiasi cha mazao yanayopotea baada ya mavuno, kukuza kipato cha mkulima, kuongeza uhakika wa ubora na kiasi cha mavuno pamoja na viinilishe, kuongeza ufanisi wa pembejeo uzalishaji (kwa idadi na ubora), kuongeza uzalishaji wa chakula, na kuboresha maisha ya wananchi.   

CRDB ndio benki inayoongoza kwa kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo ikiwa na takriban asilimia 45 ya mikopo yote inayotolewa kwenye eneo hilo. Benki inao uzoefu w akutosha kwenye sekta hiyo ikikumbukwa kwamba ilianzishwa kama benki ya ushirika wa maendeleo vijijini miaka ya 1980.

"Tunao mkakati makini kabisa wa kuiwezesha sekta ya kilimo na mnyororo wake wa thamani kwa sababu tunaelewa na kuzitambua fursa ilizonazo katika kuboresha maisha ya kaya,” amesema Nsekela.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad