HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 22, 2021

BASHE: TUMEFANIKIWA KUFUNGUA SOKO LA PARACHICHI NCHINI AFRIKA YA KUSINI


Dodoma, Tanzania.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema ya kuwa “Serikali ya Tanzania imefanikiwa kufungua soko la parachichi nchini Afrika ya Kusini baada ya muda mrefu wa majadiliano baina ya mamlaka za Afrika ya kusini na Tanzania na kuhitimisha miaka kumi ya mgogoro wa zao la parachichi uliokuwepo baina ya nchi hizi mbili”

Aidha, Mheshimiwa Bashe ameyataja mafanikio haya kama hatua muhimu ya kulinda masoko ya mazao yanayozalishwa nchini na kujenga ushirikiano mpya katika sekta ya Kilimo ili kuhakikisha kunakuwa na ubora wa mazao pamoja na bidhaa zitokanazo na kilimo ili kuleta tija ya kilimo miongoni mwa wakulima nchini.

Mafanikio haya ya sasa yanakua ni sehemu Muhimu ya kumaliza sintofahamu iliyotokea mapema mwezi Februari mwaka 2021 ambapo mamlaka za Afrika ya kusini ziliharibu zaidi ya Tani 3 za parachichi ambazo zilisafirishwa nchini humo na kampuni ya kitanzania ya Kuza. Hata hivyo tokea hapo viongozi wa Wizara ya Kilimo, wataalamu wa Afya za mimea na taasisi za udhibiti viwango na ubora za panda zote zimekuwa zikikutana ili kuwa na makubaliano rafiki Kwa pande zote mbili.

Zao la parachichi ni moja ya mazao Muhimu Kwa ajili ya sekta ya biashara nchini ambayo imekuwa ikikua Kwa kasi. Uchunguzi kitakwimu unabainisha ya kuwa mnamo mwaka 2012, kiasi cha mauzo ya nje ya zao la Parachichi yalifikia kilo 488,492, huku miaka mitatu baadae yaani mwaka 2015 Tanzania ilisafirisha Kilo 2,579,976 Ikiwa ni ongezeko la 428.48%

Kwa mujibu wa mtandao wa taasisi ya sekta binafsi nchini (TPSF) mnamo mwaka 2018 pekee, Tanzania iliuza nje ya nchi jumla ya Tani 7,551 za parachichi ambazo ziliingizia taifa fedha za kigeni zenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 8.5 ikiwa ni sehemu ya biashara Kwa nchi za mabara ya Ulaya, Afrika na Asia huku bara la Ulaya pekee likiwa ni mnunuzi Mkuu Kwa kutumia asilimia 85 ya parachichi zote zinazozalishwa nchini.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini; Tanzania ni nchi ya Pili kwa uzalishaji wa zao la parachichi barani Afrika ikiwa nyuma ya Kenya huku uzalishaji nchini Tanzania ukifikia tani 190,000 Kwa mwaka



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad