HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, October 10, 2021

WANAWAKE WAFANYIWA MATUKIO 474 YA UKATILI BABATI

 

Na Joseph Lyimo
OFISI ustawi wa jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Mkoani Manyara, Mathias Focus amesema matukio ya ukatili kwa wanawake yamezidi kufanyika ambapo kwa mwaka 2020 matukio ya 474 yameripotiwa kwa wanawake kufanyiwa ukatili wa aina tofauti.

Focus ameyasema hayo wakati akielezea matukio mbalimbali ya kikatili yanavyofanyika kwa wanawake wa wilaya ya Babati, hivyo jamii inapaswa kubadilika na kuachana na vitendo hivyo.

Amesema miongoni mwa matukio hayo 474 yalivyofanyika kwa wanawake wa Wilaya hiyo ya Babati, imeelezwa kuwa ukatili wa kimwili ni matukio 249, ukatili wa kijinsia ni matukio 117 na ukatili wa kingono ni matukio 48.

Amesema amesema ukatili mwingi unaofanyika kwa wanawake hao ni ukatili wa kimwili, wanawake wamekuwa wakivutwa nywele kwa kukosea kupika na wengine kuambulia kipigo.

Amesema pia ukatili wa kihisia unaharibu ubongo huku akisema mara nyingine kuna maneno ya fedheha wanafanyiwa akitoa mfano mtoto anapokosea anatukaniwa mama yake.

"Wivu wa kupitiliza ni ukatili wa kihisia ambao unaathiri wanawake kisaikolojia kwa kuwa wapo ambao wanafuatiliwa kila wanachofanya kupitia ukatili wa wanawake," amesema Focus.

Amesema miongoni mwa sababu za ukatili ni watu kuwa na jeuri ya uwezo wa kielimu au kifedha, kuwa na mamlaka, dini na migogoro mbalimbali ya kifamilia.

Ameyataja madhara ya ukatili kwa wanawake ni kuwa na majeraha, vifo, magonjwa ya zinaa na wanawake hao kujitenga na jamii.

Amewashukuru waandishi wa habari wa mkoa wa Manyara kwa namna kwa wanavyoamua kutoa elimu kwa kundi hilo la wanawake juu ya kupinga ukatili wanaofanyiwa.

Mkazi wa kata ya Riroda, Magreth John amesema unyanyasaji wa wanawake kwenye eneo hilo umekithiri kwani mfumo dume bado una nguvu kubwa na elimu haijatolewa vyakutosha eneo hilo ili kukomesha hayo.

Magreth amesema kundi hilo la wanawake limekuwa linapitia vikwazo vingi vya maisha kwani wengine huwa wanabakwa ila hawajui waanzie wapi ili kukomesha hali hiyo.

Amesema wanawake huwa wanahofia kutangaza kubaka kwa kudhani kuwa watadhalilika hivyo kutoa ila baada ya kupata elimu hiyo watakuwa na uelewa wa kupata haki zao na kuepuka kufanyiwa ukatili.

Mkazi mwingine Mariam Nicodemus amesema ameachwa na mume wake na ametelekezewa watoto na hasaidiwi kitu chochote na hana uhuru wa kufanya jambo lolote kwa kuwa anamtafuta kila anapoenda na anamzuia kwenda kuabudu kanisani.

“Japokuwa tumeachana na huyu mwanaume ila amekuwa ananifanyia matukio mengi ya ukatili ila nashindwa kuchukua hatua zozote kutokana na hofu ya kipigo kutoka kwake,” amesema Mariam.

Faudhia Ayub amesema yeye ni miongoni mwa wahanga wa matukio ya ukatili kwani alifukuzwa kwenye nyumba aliyokuwa anaishi na hivi sasa hafahamu mustakabali wake utakuwaje.

Faudhia amehoji mke akifiwa na mwanaume wake jamii haimsaidii na hapewi matumizi na wengine wamefukuzwa na ndugu wa mwanaume anasaidiwaje?

Mratibu wa chama cha wanasheria wanawake nchini (TAWLA) kanda ya kaskazini, Happines Mfinanga amesema ili kukomesha matukio ya ukatili wa wanawake inapaswa kila mmoja avunje ukimya juu ya hilo.

“Ukiona matukio ya ukatili yanafanyika usinyamaze, unapaswa kutoa taarifa kwenye sehemu husika ikiwemo polisi na madawati ya jinsia ili kukomesha unyanyasaji huo,” amesema Mfinanga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad