HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, October 10, 2021

TADB yafufua kiwanda cha kuchakata pamba Geita

 WADAU katika mnyororo wa thamani wa zao la pamba mkoani Geita wameishuru Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kutoa mkopo kiasi cha shilingi bilioni 3.3 kwa kiwanda cha kuchakata zao hilo cha Masumbwe Ginnery kilichopo kanda ya ziwa, ambapo zaidi ya wakulima 12,000 wa zao hilo kutoka vyama 84 vya msingi vya ushirika (AMCOS) wamenufaika kwa kuuza pamba yao kutokana na uwepo wa kiwanda hicho.

Wakulima wameanza kunufaika na zao hilo kutokana na uwepo wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na Chama kikuu cha Ushirika cha (MBCU LTD) ambacho kipo katika kata ya Nyakasaluma, Masumbwe  wilayani Mbogwe Mkoani Geita.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya kukua kwa kilimo cha pamba, Mwenyekiti wa Chama hicho Bw.Benadict Bulugu ametoa shukrani zake kwa TADB kwa kuwezesha kuwepo kwa kiwanda hicho amacho kimekuwa mkombozi kwa wakulima wengi kanda ya ziwa.

‘‘Kiwanda hiki kinauwezo wa kuchambua pamba marobota 240 kwa siku na kutoa huduma ya uchakataji wa zao hilo kutoka kwa wakulima hivyo kufanya uhitaji wa pamba kuongezeka na hivyo kuhamasisha wakulima wengi kuzalisha pamba kwa tija,’’ alisema Bw.Bulugu

Alisema changamoto inayowakabili katika uzalishaji ni kukatika kwa nishati ya umeme mara kwa mara, na hivyo kuiomba serikali kuboresha huduma hiyo ambayo ni  muhimu ili uzalishaji wao ufanyike kwa ufanisi Zaidi na kunufaisha watu wengi.

‘’Wanachama wa zao hili wameweza kunufaika na ongezeko la bei kutoka shilingi 1,050/-hadi kufikia shilingi 1800/- hii ni kutokana na uwekezaji uliofanywa na ushirika kupitia mkopo kutoka TADB,” alisema Bw.Bulugu

Alieleza kuwa ongezeko la bei hiyo limekuwepo baada ya chama hicho kuanza kununua malighafi hiyo kwa wakulima vijijini waliopo katika wilaya ya Mbogwe, Bukombe, Geita, Nyang’wale, Biharamulo na Kasulu, ambao wameanza kuonja utamu wa zao la pamba, ambalo kimsingi katika miaka ya nyuma, bei ya zao hilo ilikuwa ikiwakatisha tama wakulima.

Kaimu meneja wa chama kikuu cha ushirika (MBCU L.T.D) David Magai, amesema mwamko wa wakulima hivi sasa wa kulima zao hilo uko juu baada ya kiwanda kuanza kufanya uzalishaji kwa kuelekeza macho yake maeneo ya vijijini kununua zao hilo.

Tunatarajia kuwa msimu ujao wa kilimo tutapata malighafi nyingi kutoka kwa wakulima kwa wegi watahamasika kulima kutokana na ongezeko la bei na uhakika wa soko ambalo ni uwepo wa kiwanda,” alisema Bw.Magai

Matokeo hayo vilevile yanahusisha ongezeko la ajira zaidi kwa watumishi 168, wakiwemo vibarua 140 na watumishi 28 wenye ajira za kudumu.

Mkuu wa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita Charles Kabeyo, ameishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) kwa kutoa fedha za mkopo kwa kukikopesha kiwanda hicho zaidi ya shilingi bilioni 3.3, kwa lengo la kukufua kiwanda hicho na sasa kimeanza kutoa huduma ya uchakataji wa pamba.

“Msimu uliopita kupitia kiwanda hicho, kimeweza kununua kilogramu za pamba milioni 1.5 na hivyo kuwaomba wakazi wa wilaya hiyo kuendelea kulima pamba kwa wingi zaidi ukizingatia ni zao la kibiashara na kwamba soko lipo,” alisema Bw.Kabeyo

Kaimu Mkurugenzi wa mipango, sera na utafiti wa benki hiyo Mzee Kilele, amesema kwa kuwa benki hiyo ni benki ya kisera ya serikali itaendelea kuhakikisha zao la pamba linainuka nchini ikiwa ni pamoja na kuliongezea thamani, ili kuendelea kuimarisha thamani yake katika soko la dunia.

“Kutokana nawekezaji uliofanywa tumeelezwa kuwa kiwanda kitoa ajira za kudumu 28 , ajira za mkataba 168 hivyo kupelekea kupunguza tatizo la kukosekana kwa ajira,” alisema Bw.Kilele

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad