HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 22, 2021

TAKUKURU CHUKUENI HATUA KWA MIRADI YENYE MASHAKA NKASI-RC MKIRIKITI

 

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali akiongea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Kabwe ambapo ameishukuru serikali kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo inayochochea maendeleo ya Nkasi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (kulia) akiongea na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali (katikati) jana alipokagua ujenzi wa mradi wa hospitali ya wilaya ya Nkasi mjini Namanyele ambapo aliagiza TAKUKURU kuchukua hatua kwa wote waliohusika kufuatia uwepo wa malalamiko ya matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akiongea na wanafunzi wa shule ya msingi Ntangayika kijiji cha Chala wilaya ya Nkasi jana ambapo aliagiza hatua za haraka kuwezesha shule hiyo kupata madawati ili kuepusha watoto kuendelea kukaa chini.
Sehemu ya majengo ya hospitali mpya ya wilaya ya Nkasi iliyopo Namanyele ambayo ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 2.3 huku mradi huo ukiwa haujakamilika hatua iliyomfanya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti kuagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi na kuchuka hatua kwa watendaji watakaobaimika kukwamisha mradi huo.
(Habari na picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)

MKUU wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ameitakata Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wilaya ya Nkasi kuchunguza na kuchukua hatua kwa watendaji wote wa serikali na binafsi waliohusika katika kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo .

Mkuu huyo wa Mkoa akiwa kwenye ziara ya kikazi wilayani Nkasi (21.10.2021) alibaini kasoro kwenye miradi ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kasu na mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Namanyele ambapo miradi hiyo imekuwa na kasi ndogo licha ya serikali kutoa fedha zote.

Taarifa zinaonesha serikali kuu ilitoa fedha za mradi ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya ya Nkasi kwa awamu tatu, ambapo awamu ya kwanza ilitoa shilingi 1,500,000,000 awamu ya pili shilingi 300,000,000 na awamu ya tatu shilingi 500,000,000 lakini ujenzi bado haujakamilika.

Akiwa kwenye eneo la ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nkasi mjini Namanyele Mkuu huyo wa Mkoa alikagua mradi huo ambao serikali imekwisha toa zaidi ya shilingi Bilioni Mbili na Milioni Mia Tatu lakini ujenzi wake bado hauridhishi huku kukiwa na malalamiko mengi ya watoa huduma wakiwemo mafundi na wazabuni kutolipwa fedha zao .

“Ni aibu kuona miradi hii haikamiliki kwa wakati licha ya serikali kutoa fedha zote zinazotakiwa .Wananchi wanahitaji kuona miradi yao inakamilika kwa muda uliopangwa. Nataka kuona Takukuru mnachukua hatua kwa mujibu wa sheria fedha za umma hazipaswi kuchezewa nasi viongozi tupo kimya” alisema Mkirikiti.

Mkirikiti alitoa wito pia kwa madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kusimamia miradi ya maendeleo ikiwemo kudhibiti matumizi yasiyo na tija yanayofanywa na watumishi wa umma kwenye maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa mkoa amekemea tabia iliyojengeka kwenye jamii ya kuwasifia watu wanaofanya vitendo kinyume cha utaratibu kwa kuwaita “ majembe “ huku wakihujumu miradi ya maendeleo.

“Hivi mnamwitaje mtu jembe wakati miradi ya maendeleo haikamiliki. Kazi yenu madiwani ni kusimamia fedha za umma zilizochangwa na wananchi na zile zilizotolewa na serikali kuu ili miradi ikamilike na kuwasaidia wananchi kuondokana na shida zao” alisisitiza Mkirikiti.

Mkirikiti aliongeza aliongeza kusema kuwa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa mkoa wa Rukwa inatakiwa kuchukua hatua za kisheria kwa watumishi wote waliobainika kutumia vibaya madaraka yao kuharibu utekelezaji wa miradi hatua inayopelekea fedha za umma kutumika vibaya.

Mradi mwingine ambao mkuu huyo wa Mkoa alibaini kasoro ni ule wa ujenzi wa kituo kipya cha Afya Kasu ambapo serikali imetoa shilingi Milioni 500 lakini Halmashauri imefanya matumizi ya shilingi Milioni 60 kinyume na taratibu bila kuwa na kibali cha kubadilisha matumizi ya fedha hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Peter Lijuakali alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa kasi ya ujenzi wa majengo kwenye Hospitali mpya ya Wilaya ya Nkasi imepungua kwa kiwango kikubwa kutokana na uwepo wa malalamiko ya watoa huduma wakiwemo mafundi na wazabuni kutolipwa.

Lijuakali aliongeza kusema ameunda timu ya uchunguzi ambapo tayari imewasilisha taarifa kuwa kuna tatizo la mradi huo kutekelezwa bila kuwa na nyaraka mahsusi hatua inayoonyesha uwepo wa mianya ya matumizi yasiyo sahihi ya fedha za serikali na kwamba ana wasiwasi endapo mradi huo utakamilika kwa wakati.

“Mradi huu wa hospitali yetu ya wilaya una mapungufu mengi ikiwemo tatizo la ukosefu wa taarifa muhimu za utekelezaji wake toka kwa wataalam. Nitawasilisha kwako Mkuu wa Mkoa taarifa ya uchunguzi juu ya mwenendo wa ujenzi uone na kuchukua hatua ili kuunusuru kwani sina hakika kama utakamilika kwa wakati kwani naambiwa fedha zimeisha na mradi bado” alisema Lijuakali.

Mkuu huyo wa Mkoa yupo kwenye ziara ya kikazi wilaya ni Nkasi ambao pia amezungumza na wananchi wa kijiji cha Kabwe na kuwahamsisha kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO -19 ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa korona pamoja na kuwahamasisha kujiandaa kwa zoezi la sense ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2022.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad