HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 22, 2021

TRA YAFUNGUA UKURASA MPYA, WAFANYABIASHARA KUWEKEWA MAZINGIRA RAFIKI YA ULIPAJI KODI

 KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata ametembelea kiwanda cha Uzalishaji sukari cha Kagera Sugar kilichopo mkoani Kagera kwa lengo la kujionea shughuli za Uzalishaji wa sukari kiwandani hapo pamoja na kuimarisha mahusiano na walipakodi wakubwa nchini.

Katika ziara yake kiwandani hapo, Kamishna Mkuu amebainisha kuwa TRA kwa sasa imefungua ukurasa mpya na wafanyabiashara kwa kuweka mazingira rafiki ya ukusanyaji kodi huku ikizingatia sheria za kodi pamoja na taratibu zake.

"Tumefungua ukurasa mpya na wafanyabiashara ili kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kukusanya kodi bila kutumia nguvu na sisi TRA tumejipanga kufanya hivyo kwa weledi ili tuweze kufikia lengo la makusanyo." Amesema Kamishna Mkuu Bw. Kidata

Katika ziara hiyo kiwandani, Kamishna Mkuu pia ametembelea miradi mbalimbali ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na kiwanda hicho ili kuongeza uzalishaji unaolenga kutosheleza uhitaji wa sukari hapa nchini.

Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa uzalishaji umeme kwa matumizi ya kiwanda, umwagiliaji, hospitali, shule ya awali, daraja na miradimbalimbali kwa ajili ya kuongeza uwekezaji wa kiwanda na kuongeza uzalishaji.

Aidha, Kamishna Mkuu amewapongeza wawekezaji wa kiwanda hicho na kuwaahidi kushirikiana nao katika kutatua changamoto zote za kikodi pamoja na kuweka mazingira rafiki ya ulipaji kodi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kiwanda cha Sukari Kagera Bw. Seif ameshukuru Kamishna Mkuu wa TRA kwa kufika kiwandani hapo kujionea shughuli za uzalishaji wa sukari na jinsi kiwanda kinavyofanya uwekezaji mkubwa ili kuongeza uzalishaji wa sukari.

"Kwa kweli Tunakushukuru sana ujio wa Kamishna Mkuu wa TRA, hii inatupa faraja kubwa kuona TRA wanatambua uwekezaji huu kwa kulipa kodi lakini pia kama sehemu ya jamii ya mkoa wa Kagera kwa kutoa ajira.

Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Kidata ameendelea na ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa ikiwemo Mwanza na Kagera lengo ni kukutana na wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa masuala ya kodi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kiwanda cha Kagera Sugar Bw. Seif A Seif akitoa maelezo ya uzalishaji wa sukari kiwandani hapo kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA na viongozi wa Mamlaka waliotembelea kiwandani hapo.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Bw Alphayo Kidata (wa pili kutoka kushoto) na mwenyeji wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kiwanda cha Kagera sugar Bw. Seif A. Seif wakitembelea kiwanda cha Kagera Sugar kilichopo mkoani Kagera.

Viongozi mbalimbali wakipata maelekezo walipotembelea kiwanda cha Kagera suger kilichopo Mkoani Kagera.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad