MATUKIO YA UKEKETAJI BADO YAPO HANANG’ - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 20, 2021

MATUKIO YA UKEKETAJI BADO YAPO HANANG’

 

Na Joseph Lyimo
MATUKIO ya vitendo vya ukatili vya uekeketaji bado vimeshamiri Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, ambapo inadaiwa asilimia 90 ya wanawake wa eneo hilo wamefanyiwa ukeketaji.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya madhara makubwa yanayoweza kujitokeza kwa vitendo vya ukeketaji wa wanawake ikiwemo, kuzimia, fistula, kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua mtoto, kuzimia, kupata uambukizo (Infection), kuambukizwa virusi vya ukimwi (VVU) na kupata Tetanus.

Madhara mengine ni maumivu ya Kisaikolojia, maumivu wakati wa kukojoa, kuziba kwa njia ya mkojo, kuchanika vibaya wakati wa kujifungua, maumivu ya kisaikolojia, kuchelewa kujifungua na kifo.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanatupa lawama zao kwa taasisi zinazohusika na haki za wanawake na watoto kwani wanakaa maeneo ya mjini huku vijijini vitendo hivyo vikiendelea kushamiri kutokana na ukosefu wa elimu hiyo.

Kwenye wilaya ya Hanang’ zaidi ya asilimia 90 ya wanawake wamefanyiwa ukeketaji huku polisi wakiendesha zoezi la kuwakamata wanawake wanaobainika kushiriki matukio hayo ya kikatili.

Hivi karibuni wanawake wawili wakazi wa kijiji cha Milongori, Kata ya Ishiponga wilayani Hanang’ eneo ambalo limepakana na Mkoa wa Singida, walikamatwa kwa kushiriki kuwakeketa watoto wadogo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Kamishna msaidizi (ACP) Merrisone Mwakyoma amewataja wanawake hao kuwa ni Regina Kwekuu (40) na Esther Bashiru (19) ambao ni wakazi wa kijiji hicho cha Milongori.

Kamanda Mwakyoma amesema wanawake hao wanashikiliwa kwa kuwakeketa watoto akiwemo mwenye umri wa miezi minne na mwingine akiwa na mwezi mmoja tangu azaliwe.

“Kuwafanyia tohara watoto wa kike wachanga ni mbinu mpya inayotumiwa na watu hao wakiamini kuwa kuwafanyia watoto wachanga ukeketaji ni vigumu kubainika ila tumewabaini,” amesema.

Amesema wanawake hao wapo hospitali ya wilaya ya Hanang Tumaini wakiwauguza watoto wao wakiwa chini ya ulinzi wa polisi kwa ajili ya kuchukua hatua nyingine za kisheria.

Ameeleza kuwa wanaume wa eneo hilo wamekana kufahamu muendelezo wa vitendo hivyo kwakuwa vinafanywa na wanawake kwa siri kubwa licha ya kwamba wanasema si jambo la kushangaza.

Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Hanang’ ya Tumaini Dkt Benedict Ngaiza amethibitisha kupokelewa kwa watoto hao hospitalini hapo na kueleza kuwa asilimia 90 ya wanawake wa wilayani hiyo wamefanyiwa vitendo vya ukeketaji.

Mkazi wa kata ya Katesh, Magreth Udaa amesema Serikali inapaswa kukemea vitendo hivyo kwani ni matukio ya kusikitisha, hivyo wachukue hatua ya kubaini wakeketaji na kuwachukulia hatua

“Hawa wanawake wanaokeketa watoto wa wenzao wanapata kipato hivyo serikali ichukue hatua kwa kufanya mikakati ya kuwakamata mangariba wanaofanya vitendo hivyo na kuwachukulia hatua,” amesema Udaa.

Mkuu wa dawati la jinsia Hanang’ mkaguzi msaidizi wa polisi, Blandina Majubu amesema kujulikana kwa vitendo hivyo vya ukeketaji kumeibuliwa na mtu mmoja ambaye alitoa ushirikiano kwenye hilo.

Mratibu wa chama cha wanasheria wanawake Tanzania (TAWLA) mkoa wa Arusha, Happiness Mfinanga amesema jamii inapaswa kutoa taarifa pindi ikibaini kutokea matukio ya vitendo vya ukatili kwa mtu yeyote.

“Jamii isifumbie macho ukatili, unaweza kutoa taarifa kwa vyombo vya sheria ikiwemo polisi kupitia dawati la jinsia na ofisi za maofisa wa ustawi wa jamii kwenye eneo la karibu,” amesema Mfinanga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad