MAPINGAMIZI KESI YA MBOWE NA WENZAKE YATUPILIWA MBALI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 20, 2021

MAPINGAMIZI KESI YA MBOWE NA WENZAKE YATUPILIWA MBALI

 


Mwenyekiti wa chadema, Freeman Mbowe akiteta jambo na wakili wake, Peter Kibatala leo katika Mahakama mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa 'Mafisadi'.  
Wafuasi wa Chadema wakimuaga Mbowe mara baada ya kesi yake kuahairishwa mpaka itakapopangiwa jaji mwingine

=====   =====   =====

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa 'Mafisadi' imetupilia mbali Mapingamizi mawili yaliyowekwa na upande wa utetezi katika kesi ndogo ndani ya kesi Msingi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu kwa sababu mapingamizi hayo hayana mashiko kisheria.

Katika mapingamizi hayo, walikuwa wakipinga kupokelewa kwa maelezo ya onyo ya mshtakiwa Adam Kasekwa kwa madai kuwa yalichukiliwa nje ya muda na kwamba kabla ama wakati alichukuliwa maelezo hayo aliteswa.

Kufuatia uamuzi huo Mahakama imeyapokea maelezo ya Kasekwa na kusema ushaidi unaonyesha maelezo hayo yalitolewa na mshtakiwa mwenyewe kwa hiyari yake na kwamba yalichukuliwa ndani ya muda.

Uamuzi huo umetolewa leo Oktoba 19,2021 na Jaji Kiongozi, Mustapha Siyani.

Mbali na Mbowe na Kasekwa, watuhumiwa wengine katika kesi ya msingi ya ugaidi ni, Halfan Bwire na Mohammed Ling'wenya.

Akisoma uamuzi hio Jaji Siyani amesema, katika pingamizi la kwanza la mshtakiwa kuchukuliwa maelezo nje ya muda kulikuwa na sababu ya kwamba muda ambao ulitumiwa kwa ajili ya kumtafuta mshtakiwa mwenzao Mosses Lingenya na muda wa safari kutoka Arusha kuja Dar es Salaam haupaswi kuwa sehemu ya masaa manne ambayo mtuhumiwa anapaswa kuhojiwa kisheria pindi anapokamatwa.

Amesema, kifungu namba 50 (2) na cha 51 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinaruhusu muda wa kumhoji mtuhumiwa kuongezwa kwa masharti maalum, ikiwemo mkuu wa upelelezi kuongeza muda kwa ajili ya kufanya upelelezi au kuomba kibali cha kuongeza muda huo mahakamani.

Amesema, hoja ya upande wa jamhuri ya uchelewa kumhoji Kasekwa kwa sababu ya mtuhumiwa huyo kuwasaidia kumtafuta mwenzao, Moses Lijenge mkoani Kilimanjaro na Arusha na kumsafirisha kutoka Moshi kuja Dar es Salaam, ina mantiki.

"Ni maoni yangu kwamba kuchelewa kwa kuhojiwa au kuchukuliwa maelezo Kasekwa kulikuwa na sababu na kwamba zinafanana na matakwa ya sheria kwani katika kesi hii polisi walikuwa na sababu ya kuchelewa kuchukua maelezo ya mshtakiwa kutokana na shuguliza kiupelelezi zilizokuwa zikieendelea ikiwa ni pamoja na kumtafuta mshitakiwa Lijenje pamoja na kusafirisha watuhumiwa hao kutoka Moshi hadi Dar es Salaam.

Jaji Kiongozi Siyani amesema, upande wa utetezi haukupinga kitabu cha mahabusu (dentetion register) kilicholetwa na jamhuri mahakamani hapo kama sehemu ya ushahidi wake, kilichoonesha kuwa mtuhumiwa alihojiwa kituo kikuu central Dar.

"Pingamizi la utetezi lilipaswa kuwa dhidi ya kielelezo cha jamhuri ambacho ni kitabu cha mahabusu (detention register) kinachoonesha kuwa mtuhumiwa alipokelewa na kuhojiwa Kituo cha kati cha Polisi Dar es Salaam, pamoja na kupinga mtuhumiwa kufikishwa kituoni hapo lakini hawakufanya hivyo na pia hakuna mahali ambapo mtuhumiwa alipinga kuhojiwa Kituoni hapo , bali alisema alitoa maelezo kwa mateso hivyo mapingamzii ya utetezi ya kwamba alihojiwa kwa mateso hayana mashiko.

Katika hoja ya kwamba kuchukuliwa maelezo akiwa katika mateso, Jaji Siyani amesema, mshtakiwa alikubali kwamba alitoa maelezo lakini hakuna ushahidi wa kwamba hakufika kituo cha polisi kati ambapo maelezo hayo yalichukuliwa.

Jaji Siyani amesema, shahidi wa kwanza wa upande wa Mashtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, (RPC) Ramadhan Kingai wakati akitoa ushahidi wake alidai maelezo ya onyo ya Kasekwa yalichukuliwa kituoni hapo kuanzia majira ya saa moja na nusu hadi saa tatu asubuhi lakini hakuna mahali panapobishaniwa kuwa mshitakiwa huyo hakufika kituoni hapo.

Alisema maelezo ya shahidi yanakinzana na hoja ya msingi ya kuteswa kwake na kwamba hakuna ubishi kuwa Kasekwa alitoa maelezo kwa ridhaa yake na kwahali hivyo amepokea maelezo hayo kama kielelezo namba moja cha upande wa Mashitaka.

Kasekwa na Ling'wenya walikamatwa tarehe 5 Agosti 2020 maeneo ya Rau Madukani, Moshi Kilimanjaro na kuhojiwa tarehe 7 Agosti mwaka jana, Kituo Kikuu cha Polisi Dar ea Salaam.

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka unawakilishwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi Pius Hilla, Robert Kidando, Abdallah Chavula, Nassoro Katuga, Esther Martin na Janetreza Kitali huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Peter Kibatala akisaidiana na Rwekama Rwekiza, John Malya, Frederick Kihwello, Selemani Makauka, Michael Lugina, Iddi Msawanga, Jebra Kambole, Cisty Aloyce na Maria Mushi.

Kufuatia uamuzi huo, kesi ya msingi inaendelea kusikilizwa kwa upande wa jamhuri kuleta ushahidi wake.

Katika kesi ya msingi ambayo Mbowe aliunganishwa na wenzake watatu ambao walisomewa mashtaka kabla yake, anakabiliwa na mashitaka mawili yakiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi.

Katika shtaka la kwanza Mbowe alidaiwa kula njama kwa nia ya kutenda kosa chini ya sheria ya ugaidi na katika shtaka la pili ilidaiwa kati ya Mei na Agosti,2020 akiwa katika hoteli ya Aisha iliyoko Moshi mkoani Kilimanjaro alitoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad