HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 28, 2021

TASAC kufanya Sensa ya vyombo vidogo vya usafiri majini

 

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Nchini (TASAC) Nashoni Sigalla akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunga mafunzo ya maafisa uvuvi kwa ajili ya Sensa itakayoanza hivi karibuni kwa nchi nzima kwa vyombo vidogo vya majini.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Nchini (TASAC) Nashoni Sigalla akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunga mafunzo ya maafisa uvuvi kwa ajili ya Sensa itakayoanza hivi karibuni kwa nchi nzima kwa vyombo vidogo vya majini.

*Yabainisha matokeo ya sensa katika kufikia uchumi wa Bluu na usalama wa vyombo hivyo.

Na Chalila Kibuda,Michuzi Tv,Bagamoyo 
SHIRIKA la Uwakala wa Meli nchini (TASAC) kuanza kufanya sensa ya vyombo vidogo vya usafiri majini katika maziwa,mito pamoja na bahari ili kuweka kanzidata ya kupanga maendeleo na usalama  katika sekta hiyo.

 Sensa hiyo itashirikisha  Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) pamoja na Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambapo sensa hiyo itaanza Oktoba Mosi hadi Oktoba 30 mwaka huu na kutambua idadi ya vyombo hivyo na shughuli zake. 

Akizungumza wakati wa semina ya siku mbili kwa maafisa uvuvi yenye lengo la kuwajengea uwezo kufanya sensa hiyo Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TASAC na  Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa Shirika hilo  Nashon Sigalla amesema sensa hiyo ya nchi nzima pamoja na mambo mengine imelenga kuinua maendeleo ya sekta hiyo kusaidia katika utungaji sera za kiudhibiti.

Amesema sensa hiyo ni  mpango wa maendeleo pia itasaidia kuhimarisha usalama wa mali na uhai wa watumiaji na wamiliki  wa vyombo hivyo nchini kote.

Sigalla amesema msingi wa  sensa ya vyombo hivyo itakayofanywa katika maeneo ya bahari, maziwa na mito ikijishughulisha na kazi za uvuvi, ubebaji wa mizigo pamoja na usafirishaji wa abiria itasaidia kutambua idadi ya vyombo hivyo na majukumu yake na baadae taarifa zake kuwekwa katika kanzidata maalumu.

"Tanzania inatekeleza uchumi wa blue unaohusisha masuala yote ya uchumi wa bahari, imani tunayoijenga  kupitia sensa hii itatuwezesha kuona ni hatua zipi zichukuliwe kufanikisha maendeleo yake na kutatua changamoto zilizopo zinazokabili sekta hiyo"amesema Sigalla.

Aidha amesema kwa kuzingatia utaratibu uliopo,sensa hiyo itavishirikisha vyombo vidogo vyenye urefu usiopungua urefu wa mita 24 na uwezo wa kubeba mizigo isiyozidi tani 50 katika maeneo yote ya ukanda wa bahari, maziwa na mito ambapo shughuli ya usafiri huo unahusika.

Pamoja na kusaidia kupanga shughuli za kimaendeleo, sensa  ya vyombo hivyo pia itawasaidia wataalamu wa vyuo vya juu kufanya utafiti wao kuhusu uwepo wa vyombo hivyo kwa kuona kwa kiasi gani vinasaidia katika ukuaji wa maendeleo nchini wa dhamira ya Serikali ya uchumi wa bluu.

Sigalla alisema dhima nyingine ya sensa hiyo imetokana na mahitaji ya kitaifa ya upatikanaji wa taarifa hizo kwa ajili ya kuona njia sahihi kusaidia ukuaji wa maendeleo ya sekta hiyo inayotoa huduma zake katika maji.

Mmoja wa walengwa wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Uvuvi kutoka Mkoa wa Kagera Maengo Nchimani amesema matarajio mafunzo hayo yatawasaidia  kufanikisha malengo yaliyokusudiwa huku akiamini ujio wake ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya taifa. 

Nchimani amesema  kumekuwepo na vyombo vingi vinavyotoa huduma ya usafiri na ubebaji wa mizigo katika mito,maziwa na bahari huku akiwataka wamiliki wa vyombo hivyo na wasimamizi wake kujiandaa nayo mara itakapoanza.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad