HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 28, 2021

TANESCO: Wajamaa na Dunia Mpya ya Biashara

 

Na Ezekiel Kamwaga
TANESCO ni shirika la huduma lakini pia ni shirika la kibiashara. Ndio maana kila mwaka linakaguliwa mahesabu na ripoti ya hasara au faida inatolewa kwa umma. Kama halistahili kuendeshwa kibiashara kungekuwa hakuna haja ya kila mwaka kuripoti faida au hasara, na kungekuwa hakuna haja ya kutakiwa kutoa gawio serikalini.

Shirika linalotakiwa kupata faida ni lazima liendeshwe kwa misingi ya kibiashara - ikiwemo kuongeza tija, kupunguza matumizi, kuongeza mauzo, kuwajali wateja kwa kuwapa huduma bora, kuajiri wafanyakazi kwa sifa na kuwajali kwa maslahi stahiki, kuongeza rasilimali zake, na mambo mengineyo ambayo kampuni zenye mafanikio hupaswa kufanya.

Ni dhana potofu kuamini kwamba Shirika la Umma halipaswi kuzingatia misingi hii ya kibiashara. Ni upotofu pia kuamini kwamba Shirika la Umma likizingatia misingi hii basi gharama za huduma zinapanda. Ukweli ni kinyume.

Hakuna kundi la Watanzania - wawe wasomi, makada wa vyama vya siasa au watumishi wa serikali kuwa pekee ndio wenye uwezo, maarifa na uzalendo kwenye usimamizi wa mali za umma. Kama huo ndiyo ungekuwa ukweli, nchi yetu isingefika hapa ilipo sasa ambapo tunatumia fedha za kununulia dawa na madawati kuruzuku mashirika ya umma.

China imekuwa na mashirika mengi makubwa ya umma. Kwenye wimbi la ubinafsishaji, China ikasita kubinafsisha. Ilichofanya ni kuamua kuyaendesha kibiashara. Sasa hivi sehemu kubwa ya uchumi wa China inaendeshwa na mashirika yao ya umma. Ilifanya hivyo kwa kuwapa uendeshaji wa mashirika yake watu wenye uzoefu wa kuendesha biashara.

Ufaransa ina mashirika ya umma ambayo hata Wakurugenzi watendaji wake si Wafaransa. Wametafuta watu kote duniani wenye uwezo na kuwapa kazi kuyaendesha mashirika yao kibiashara kwa faida ya Wafaransa wote.

Hapa kwetu uteuzi wa Bodi mpya ya Tanesco iliyojaa Watanzania (ambao hawajahukumiwa kwa kosa lolote) imeonekana kama si jambo la heri katika macho na nafsi za baadhi ya watu wachache.

Huko kwa wenzetu waliofanikiwa mashirika makubwa ya umma ya umeme yanauza sehemu ya hisa zake kwenye masoko ya mitaji.

Mheshimiwa Makamba ameonyesha ujasiri na kutoa dira ya namna ambavyo mashirika yetu yanapaswa kuendeshwa.

Unatafuta best brains kwenye nchi na unawapa. Kama mmiliki (yaani Serikali) unatoa malengo ya jumla: kwamba unataka huduma bora, huduma kila pahala na huduma nafuu na unataka gawio pia.

Mwalimu Nyerere alipata kusema huko nyuma kwamba kufanya mambo kwa namna ileile na kutegemea kupata matokeo tofauti ni jambo lisilo la akili.

Waziri Makamba amejaribu kufanya kitu tofauti. Tusubiri kuona kama tutapata tunachohitaji kutoka Tanesco.

Bahati nzuri ni kwamba njia aliyoamua kuipitia, ndiyo njia ambayo imefanikiwa kwa wenzetu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad