DKT. MABULA AHIMIZA KASI YA UPIMAJI ARDHI BAHI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 22, 2021

DKT. MABULA AHIMIZA KASI YA UPIMAJI ARDHI BAHI

 
Na Munir Shemweta, BAHI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameitaka halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kuongeza kasi ya upimaji ardhi katika maeneo mbalimbali ili kuepuka ujenzi holela.

Alisema, kwa sasa maeneo mengi katika halmashauri hiyo yamepanuka kimji na hivyo kuhitaji kupangwa vizuri kwa kuzingatia taratibu za mipango miji ili kuepuka ujenzi holela.

" Kwa sasa mji wa Bahi unapanuka kwa kasi na cha msingi hapa ni kuwahi kupima maeneo na kama hakuna mpango basi mji huu utakuwa na shida na cha msingi ni kuweka nguvu katika kupanga na kupima ili usiwepo ujenzi holela" alisema Dkt Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi alisema hayo tarehe 22 Sept 2021 wilayani Bahi wakati akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya hiyo akiwa katika muendelezo wa ziara yake katika wilaya za mkoa wa Dodoma.

Katika kinachonekana kuongeza kasi ya upimaji ardhi katika wilaya ya Bahi, Naibu Waziri wa Ardhi aliagiza kuundwa timu ya mkoa kwa ajili ya kupima takriban viwanja 8000  ilivyokwama kwenye zoezi la urasimishaji makazi holela.

" Kwa kuwa makampuni yaliyokuwa yakifanya urasimishaji makazi holela Bahi yameshindwa kukamilisha kazi kwa wakati naagiza ofisi ya ardhi mkoa kukaa na mkurugenzi wa halmashauri ya Bahi iundwe na timu ya mkoa ije hapa kwa gharama ya mkurugenzi ili kukamilisha upimaji" alisema Dkt Mabula.

Aidha, Dkt Mabula ameitaka halmashauri ya wilaya ya Bahi kuangalia namna ya kuwawezesha watumishi wa umma kwa kuwapatia viwanja kwa makundi ili waweze kununua kwa kulipa kwa awamu.

" Muwawezeshe watumishi wa umma  kuwa na rasilimali ardhi kwa kuwaptia viwanja maana leo uko Bahi kesho uko eneo lingine na zipo halmashauri zimefanya hivyo lengo kumuwezesha mtumishi kupitia sekta ya ardhi katika kumiliki na kupata makazi" alisema Naibu Waziri wa Ardhi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Mwanahamisi Munkunda amemshukuru Naibu Waziri wa Ardhi kwa uamuzi wa kuagiza kuundwa kwa timu ya mkoa kwa ajili ya kukamilisha ulipimaji wa zoezi la urasimishaji.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya ya Bahi ameomba pia eneo la Zanka katika wilaya hiyo nalo kufanyiwa upimaji katika viwanja vyake 181 ambapo alisema kati ya viwanja hivyo ni 17 pekee ndivyo vilivyopimwa hasa ikizingatiwa eneo hilo kwa sasa inakuwa kwa kasi.

Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Bahi eneo la Zanka ni eneo muhimu ambalo baadhi ya maeneo yake yameanza kuingia kwenye migogoro ikiwemo ile ya kuuziana mara mbili na kusisitiza eneo hilo haliwezi kuachwa bila ya kupimwa.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watumshi wa sekta ya ardhi katika  halmashauri  ya Bahi tarehe 22 Sept 2021 mkoani Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Mwanahamis Munkundu akizungumza katika kikao baina ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Bahi tarehe 22 Sept 2021 akiwa katika ziara ya kukagua utendaji  kazi wa sekta ya ardhi.
Baadhi ya watumishi wa sekta ya ardhi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa kikao na watumishi hao wilayani Bahi tarehe 22 Sept 2021 mkoani Dodoma.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (katikati) akimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Bahi mkoani Dodoma Mwanahamis Munkunda (Kulia) mara baada ya kikao na watumshi wa sekta ya ardhi katika  halmashauri  ya Bahi tarehe 22 Sept 2021 mkoani Dodoma. Kushoto ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma Thadei Kabonge (PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE WIZARA YA ARDHI)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad