CHAMURIHO AWATAKA TANROADS KUTOA ELIMU - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 1, 2021

CHAMURIHO AWATAKA TANROADS KUTOA ELIMU

 
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, amewataka watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kutoa elimu ya kutosha kwa wasafirishaji kuhusu matumizi sahihi ya magari yanayostahili kupita katika barabara na madaraja nchini.

Dkt. Chamuriho amesema hayo jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha menejimenti na mameneja wa Wakala huo ambacho kinalenga kutatua changamoto mbalimbali za wakala huo na kupanga mikakati ya kiutendaji.

“Nimefanya tathimini ya haraka haraka nikagundua kuwa bado kuna magari ambayo ni mazito sana ambayo yanastahili kuwa site tu na si kutembea barabarani kama inavyoonekana sasa, jambo hili si sahihi watendaji naomba mlisimamie kwa karibu mkilifumbia macho litaendelea kuharibu miundombinu yetu”, amefafanua Dkt. Chamuriho

Aidha, Dkt. Chamuriho ameuagiza wakala huo kuongeza usimamizi mzuri wa mizani pamoja na watumishi wa mizani kujengewa uwezo kwa kupewa mafunzo ili waweze kutoa huduma bora kwa wateja na kupunguza malalamiko ya wasafirishaji.

Waziri Dkt. Chamuriho ameusisitiza uongozi wa TANROADS kuongeza juhudi katika kusimamia wakandarasi wa ndani ili waweze kujengewa uwezo wa kufanya kazi kwa weledi zaidi kwa sababu wengi wao bado wanahitaji usimamizi wa karibu ili waweze kufanya vizuri, pamoja na kuboresha kitengo cha Wahandishi Washauri kutoka katika wakala huo (TECU).

Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatius Mativila, amesema kuwa mizani zote nchini zimefungwa CCTV kamera kwa lengo la kufuatilia kwa karibu utendaji wa mizani hizo ili kuhakikisha kuwa huduma zinatolewa kama inavyostahili.

“TANROADS tumeshafunga kamera katika mizani zote na ni matumaini yetu kuwa barabara zitalindwa na zitadumu kwa muda mrefu”, amesema Mhandisi. Mativila.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, akizungumza na menejimenti na mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), kutoka mikoa yote Tanzania (hawapo pichani), katika kikao kazi cha wakala huo kilichofanyika jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi. Rogatius Mativila, akimkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho (hayupo pichani), kufungua kikao kazi cha uongozi na Mameneja wa TANROADS kutoka mikoa yote nchini, jijini Dodoma.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Nkolante Ntije, akichangia mada katika kikao kazi cha menejimenti na mameneja wa TANROADS kutoka mikoa yote nchini na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, jijini Dodoma
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti na mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), kutoka mikoa yote nchini mara baada ya kufungua kikao kikazi, jijini Dodoma

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad