HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 24, 2021

TUME YA MADINI KUIMARISHA USIMAMIZI MADINI UJENZI, VIWANDANI

 Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Medini, Mhandisi Yahya Samamba (kulia), akizungumza jambo kwenye Semina Elekezi kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula (katikati) na kushoto ni Kamishna wa Madini wa Tume ya Madini Janeth Ruben.


Asteria Muhozya na Tito Mselem Dodoma
IMEELEZWA kuwa, pamoja na mambo mengine, ili kufikia lengo la kukusanya Shilingi 650 Bilioni iliyopangiwa Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, Tume ya Madini itaweka nguvu kubwa katika Usimamizi wa Madini ya Viwandani na Ujenzi ili yaweze kuchangia ipasavyo.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba Agosti 23, 2021 wakati akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Madini na hali ya upatikanaji na Utoaji wa Huduma katika Masoko kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Tume ya Madini zinaonesha kuwa, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 Madini ya Ujenzi yalichangia asilimia 2 na Madini ya Viwandani yalichangia asilimia 2.

Aidha, itakumbukwa kuwa, mapema mwezi Mei, 2021 mara tu baada ya Wizara kuwasilisha Bungeni Hotuba yake ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2021/22, Tume ya Madini iliwasilisha wizarani mapendekezo ya mkakati kuhusu namna ya kufikiwa kwa makusanyo hayo ambapo miongoni mwa yaliyopendekezwa ni pamoja na kuimarishwa kwa usimamizi katika madini ya ujenzi.

Akizungumzia hali ya utoaji na upatikanaji wa huduma katika masoko ya Madini Samamba alisema kuwa, tangu kuanzishwa kwa Masoko ya Madini mwezi Machi 2018, hadi kufikia Juni 2021, jumla ya Masoko ya Madini 41 na Vituo Vidogo vya Ununuzi 59 vimeanzishwa na kuongeza kwamba, kati ya masoko yaliyoanzishwa, 26 ni ya dhahabu, masoko 14 ni ya madini ya vito na soko 1 ni la Madini ya Bati.

‘’ Mhe. Mwenyekiti kati ya vituo 59 vya ununuzi wa Madini vilivyoanzishwa, vituo 55 ni vya ununuzi wa Madini ya dhahabu, vituo 2 ni vya ununuzi wa madini ya vito na dhahabu, 1 cha madini ya almasi na 1 cha madini ya vito,’’ alisema Mhandisi Samamba.

Akielezea hali halisi ya mapato katika masoko, Mhandisi Samamba aliieleza Kamati kuwa, tangu kuanzishwa kwa masoko hayo mwaka 2018 hadi kufikia mwezi Juni 2021, usimamizi wa masoko ya madini umeendelea kuimarika ambapo katika kipindi rejewa kilogram 32,592.84 za dhahabu, karatu 32,636.59 za Madini ya almasi na kilogramu 144,102.09 za Madini ya bati ziliuzwa kupitia masoko hayo.

Pia, aliongeza kuwa, karati 249,869.53 za tanzanite, kilogramu 3,461,183.27 na karati 47,029.11 za Madini ya vito mbalimbali ziliuzwa kupitia masoko hayo na kuipatia Serikali jumla ya shilingi bilioni 258.17.

‘’Mchango wa masoko kwenye mapato yatokanayo na Madini umeongezeka kutoka asilimia 2.62 mwaka 2018/19 hadi kufikia asilimia 26.44 mwaka 2020/21,’’ aliongeza Mhandisi Samamba.

Akizungumzia mchango wa masoko ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2020.2021, alisema masoko hayo yamechangia kiasi cha shilingi bilioni 145.23 sawa na asilimia 26.44 ya mapato yatokanayo na mrabaha na ada za ukaguzi ikilinganishwa na mwaka 2019/20 ambapo masoko hayo yalichangia kiasi cha shilingi bilioni 104.63 sawa na asilimia 21.28.

Aidha, akielezea matazamio katika Masoko ya Madini aliyataja baadhi kuwa ni pamoja na mapato yanayotokana na madini yanatazamiwa kuongezeka kutokana na kufutwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa Madini yanayoingizwa ndani ya nchi, kurejea kwa mnada wa Madini ya vito Arusha ambako kunatarajia kuvutia uingizaji wa Madini ya vito na ununuzi kutoka nchi za nje na hivyo kuchochea mzunguko na mitaji ya wafanyabiashara wakubwa kuongezeka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad