HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, January 28, 2021

Class, Mwale kumaliza ubishi kesho Next Door Arena, Pulev, Miller nao watamba

 

 


Dakika 30 ndizo zitaamua bingwa wa WBF wa mabara kati bondia Ibrahim Class na Dennis Mwale kesho Ijumaa Januari 29 kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Masaki jijini Dar es Salaam.

Mabondia hao watakata mzizi wa fitina katika pambano la raundi 10 litakalosindikizwa na mengine manane.

Leo mabondia hao walipima uzito na afya, tukio lililogubikwa na tambo nyingi, huku Class akiahidi kumaliza pambano mapema.

"Sitarajii Mwale acheze na kumaliza raundi zote, niko fiti na ninachokihitaji ni matokeo yasiyokuwa na utata," alitamba Class jana.

Mabondia hao watazichapa pambano la raundi 10 ambalo litapigwa kwa dakika 30, ingawa Class amesisitiza kulimaliza mapema.

Mkurugenzi wa Jackson Group Sports Agency, Kelvin Twissa alisema maandalizi yamekamilika na mabondia wote kutoka nje ya nchi wamewasili tayari kwa pambano hilo lililodhaminiwa na benki ya CRDB, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na hoteli ya Onomo.

Amesema milango ya Next Door Arena itakuwa wazi saa 10 jioni kwa mashabiki kuanza kuingia na pambano la kwanza litaanza saa moja usiku.

Mapambano mengine leo ni kati ya bondia kutoka Bulgaria Tervel Pulev ambaye atapambana na Vikapita Merero wa Namibia katika uzito wa Cruiser wakati Bondia kutoka DR Congo, Ardi Ndembo atapambana na Mtanzania Pascal Enock katika uzito wa juu.

Bondia wa kike Happy Daudi atacheza na bondia wa Zambia Lolita Ndembo katika uzito wa superwelter la raundi nane huku Saidi Mrosso atazichapa na Gomatsang Gaasite wa Botswana na Jacob Maganga atazipiga na Hafidhi David.

Shaaban Jongo atapigana na Shawn Miller wa Marekani kuwania mkanda wa kimataifa wa WBF wa uzito wa juu, Nasibu Ramadhani atapigana na Nkosinati Biyana kutoka Afrika Kusini na Stumai Muki atapambana na bondia kutoka Zimbabwe, Revai Madondo.

Hiyo ni mara ya kwanza katika historia ya ndondi nchini mabondia kutoka nje ya nchi kuja kuzichapa nchini wote wakicheza ugenini.

Mkuu wa wateja wa kampuni ya Jackson Group Sports, Cynthia Marealle aliwaomba mashabiki kufika kwa wingi leo ili kushuhudia mabonia hao wakiwania ubingwa huo. Cynthia alisema pia kuna mapambano ya mabondia wa kike na kuwaomba wanawake kuja kuona jinsi mabondia wawili wa Tanzania, Stumai Muki na Happy Daudi wakionyesha vipaji vyao.

"Jackson Group Sports imewajali wanawake na ndiyo maana hata kwenye pambano la kwanza, washiriki na kuonyesha uwezo mkubwa. Safari hii tumeongeza idadi ya mapambano kwa lengo la kutoa fursa zaidi, nawaomba kufika kwa wingi ili kuwapa sapoti," alisema Cynthia.

Meneja wa Miradi na Maendeleo ya Biashara wa kampuni ya Jackson Group Sports, Levis Paul (Katikati) akiwatambulisha bondia Ibrahim Class wa Tanzania (kushoto) na Dennis Mwale wa Malawi ambao wanapanda ulingoni Ijumaa (Januari 29) kwenye ukumbi wa Next Door Arena. Mabondia hao wanawania mkanda wa uzito wa Super Feather wa WBF.

Tervel Pulev (kulia) dhidi ya Vikapito Merero huku Kubrat Pulev (wa kwanza kulia) akishuhudia


 Ibrahim Class akipima uzito


Shawn miller (kushoto) akipima uzito na Shaaba Jongo wa pii kulia

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad