KASEKENYA AWATAKA WATUMISHI WA MIZANI KUONGEZA KASI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 23 December 2020

KASEKENYA AWATAKA WATUMISHI WA MIZANI KUONGEZA KASI


 

KASEKENYA AWATAKA WATUMISHI WA MIZANI KUONGEZA KASI

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka watumishi wa mizani kutumia muda mfupi kupima na kuruhusu magari katika vituo vya mizani nchini ili kuondoa msongamano wa magari katika maeneo hayo.

Akizungumza mara baada ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja, Awamu ya kwanza (OSIS) katika  mizani ya Vigwaza mkoani Pwani, Mhandisi Kasekenya amesema Serikali imejipanga kuhakikisha hakutakuwa na ucheleweshaji wa malori katika vituo vya mizani hivyo kuwataka wasafirishaji kuzingatia sheria na kanuni wanapopakia mizigo ili kuepuka usumbufu.

"Lengo letu ni kuhakikisha magari yote yanabeba mizigo inayokubalika kisheria ili kuepuka faini na kulinda barabara tunazozijenga kwa fedha nyingi", amesema Mhandisi Kasekenya.

Kasekenya ameelezea matokeo chanya yanayotarajiwa baada ya ujenzi wa mradi huo kukamilika ni kupungua kwa  muda na gharama za usafirishaji, kuboresha usalama wa magari barabarani, kupunguza msongamano wa magari barabarani, kuondoa ukaguzi wa mara kwa mara kwa wasafirishaji hasa wa kuelekea mikoani na nchi jirani.

Aidha, amemtaka Mkandarasi China Railway Seventh Group anayejenga mradi huo kukamilisha kwa wakati na Serikali haitasikiliza visingizio vya mvua mara baada ya muda wa mkataba kumalizika.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Pwani, Mhandisi Yudas Msangi, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa mradi huo utasimamiwa kwa uangalifu na kwa kuzingatia viwango vilivyokubaliwa kimkataba na kutoa fursa za ajira kwa watanzania.

Msangi amefafanua kuwa zaidi ya magari 1700 yanapimwa kila siku katika mizani hiyo.

Zaidi ya shilingi bilioni 17 zinatumika katika utekelezaji wa mradi huo ulioanza tarehe 02/09/2020.

 

Muonekano wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja, Awamu ya Kwanza (OSIS) katika  mizani ya Vigwaza, mkoani Pwani.
Mhandisi kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Pwani Charles Ndyetabula, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipokagua shughuli za upimaji magari katika mizani ya Vigwaza.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Pwani Mhandisi Yudas Msangi, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipokagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja, Awamu ya Kwanza (OSIS) katika  mizani ya Vigwaza.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akisisitiza jambo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Pwani Mhandisi Yudas Msangi, wakati alipokagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja, Awamu ya Kwanza (OSIS) katika  mizani ya Vigwaza. 


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad