HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 23, 2020

Dkt.Abbasi: Kiingilio cha Tamasha la Serengeti Music Festival kutumika kusaidia Sekta ya Sanaa

 
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa  na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi amesema kuwa Tamasha la Serengeti Music Festival  litakuwa na vitu vingi ikiwemo tuzo mbalimbali kuanzia 2021,  pia litaboreshwa zaidi.

Dkt.Abbasi ameyasema hayo leo Desemba 22,2020 Jijini Dar es Salaam katika Studio za Clouds FM ndani ya Kipindi cha XXL ambapo alikwenda  kuzungumzia maandalizi ya tamasha hilo litakalofanyika tarehe  26, Desemba 2020 katika Uwanja wa Uhuru kuanzia saa 08:00 mchana.

"Jina Serengeti katika tamasha hili linaasi muktadha wa kuanziasha uhusiano wa ushirikiano wa Sanaa na Utalii kwani kupitia Mbuga ya Serengeti taifa limepata heshima makubwa na tunahitaji wasanii watumie vipaji vyao kutangaza utalii wa nchi,"alisema Dkt. Abbasi.

Akiendelea kuzungumza kuhusu maandalizi ya Tamasha hilo Dkt. Abbasi alieleza kuwa kiingilio katika tamasha hilo ni Tsh. Elfu Tano na fedha hizo kutumika kusaidia mambo mbalimbali katika sekta ya Sanaa. Pia alieleza malipo kiingilio hicho yanafanyika kupitia mfumo wa N - Card na kadi hiyo inatumika katika mambo mbalimbali ikiwemo kulipia usafiri wa Mwendokasi, kukata tiketi za kutazama mechi za Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uhuru pamoja na tiketi za kivuko cha kigamboni. 

Halikadhalika Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa N- Card hizo zinapatikana katika Sunderland Sports Wear Kariakoo/Nyamwezi, Merere Sports Wear Kariakoo mkabala na Big bon Msimbazi, Uwanja wa Uhuru, Shafii  Dauda Sinza Makaburini na Tabata, Maduka yote ya Vunjabei Dar es Salaam pia katika siku hiyo ya tamasha kadi hizo  zitakuwa zikiuzwa uwanja uhuru wakati wote.

Pamoja na hayo nao mahasimu wa Bongo Fleva wa zamani  kutoka kundi la TMK Juma Nature na King Crazy GK kutoka East Coast Team walisisitiza kutoa burudani  kali kwa mashabiki zao huku kila mmoja akisisitiza yeye ni msanii bora zaidi ya mwengine.

Akihitimisha mahojiano hayo Dkt.Abbasi alitaja Orodha ya wasanii ambao watashiriki tamasha hilo na kusema zaidi ya wasanii arobaini watatoa burudani katika usiku huo wa kusheherekea vipaji vya wasanii wa Tanzania na burudani hiyo itaanza kuaanzia saa nane mchana. Pia alisema kuwa Muziki wa Tanzania unakuwa kwa kasi na wasanii wamekuwa wakipata tuzo mbalimbali za kimataifa.

Kijana Msanii Mchoraji wa Picha kutoka Mwanza Deonatus Sotery akimkabidhi zawadi ya picha Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni  Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi aliyomchora katika studio za clouds fm redio mara baada ya mahojiano ya Maandalizi ya Tamasha la Serengeti Music Festival litakalofanyika tarehe 26,Desemba 2020 Uwanja wa Uhuru, katika kipindi cha XXL.
Msanii Juma Nature kutoka Kundi la TMK akiimba mmoja ya wimbo wa kundi lao katika Studio za Clouds Fm Redio leo Desemba 22,2020 wakati wa mahojiano ya namna walivyojipanga kutoa burudani katika Tamasha la Serengeti Music Festival litakalofanyika tarehe 26,2020 Uwanja wa Uhuru, ambapo katika kipindi hicho waliandamana na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni  Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi.
Msanii King Crazy GK kutoka Kundi la East Coast Team akiimba mmoja ya wimbo wa kundi lao katika Studio za Clouds Fm Redio leo Desemba 22,2020 wakati wa mahojiano ya namna walivyojipanga kutoa burudani katika Tamasha la Serengeti Music Festival litakalofanyika tarehe 26,2020 Uwanja wa Uhuru, ambapo katika kipindi hicho waliandamana na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni  Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni  Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi (watatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wasanii wa Muziki wa Hiphop wa zamani kutoka kundi la TMK msanii Juma Nature(wa kwanza kushoto) na King Crazy GK (wa pili kulia) kutoka kundi la East Coast Team ambao ni mahisimu wa jadi katika studio za clouds fm redio mara baada ya mahojiano ya maandalizi ya Tamasha la Serengeti Music Festival litakalofanyika Desemba 26,2020, Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam,ambapo makundi ya wasanii hao nayo yatatoa burudani katika tamasha hilo.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni  Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi akizungumza kuhusu maandalizi ya Tamasha la Serengeti Music Festival  litakalofanyika tarehe 26,Desemba 2020 Uwanja wa Uhuru, katika Studio za Clouds Fm katika Kipindi cha XXL, leo Desemba 22,2020 Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad