HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, December 23, 2020

WANANCHI WATOA MWEZI MMOJA HALMASHAURI YA SONGEA KURUDISHA FEDHA


 Na Muhidin Amri, Songea

WAKAZI wa kijiji cha Nakahegwa  wilaya Songea mkoani Ruvuma,wametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea, kurudisha fedha kiasi cha milioni 10 ilizochukua ambazo zilitolewa kukamilisha ujenzi wa kituo cha Afya kinachojengwa katika kijiji hicho.

Wamesema,wanazihitaji  fedha hizo zilizotolewa na Serikali ili waweze  kukamilisha ujenzi  huo ambao umesimama kwa muda mrefu kutokana na upungufu wa fedha, hivyo kusababisha wananchi kuendelea kuteseka kwa kukosa huduma za matibabu karibu na makazi yao.

Wakizungumza jana mbele ya  wajumbe wa shirikla lisilo la kiserikali Roa kupitia ufadhili wa Foundation for Civil Society unaotekeleza mradi wa mfumo wa ufuatiliaji wa uwajibikaji jamii(UUJ)yaani Social Accountability Monitoring(SAM) unaoshugulisha na elimu ya uwajibikaji na ushirikishwaji  jamii katika miradi ya Afya wamesema,  fedha hizo  zinahitajika sana kwa ajili ya kukamilisha  kazi zilizobaki kama madirisha,kujenga matundu ya choo, na kununua baadhi ya vifaa tiba.

Wamesema,  wamechoka kutembea umbali mrefu kwenda Hospitali ya mkoa Songea umbali wa km 35 kufuata matibabu wakati serikali ilishatoa fedha kwa ajili ya kupeleka huduma za Afya katika kijiji chao.

Wamesema, fedha hizo zilichukuliwa na uongozi wa Halmashauri ya wilaya bila kushirikishwa kamati ya ujenzi na hakuna makubaliano wala taarifa iliyotolewa kwa wananchi, jambo linalotia hofu juu ya  usalama na matumizi sahihi  ya fedha hizo.

Wamemtaka mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha fedha  hizo zinarudishwa haraka  iwezekanavyo  ili kukamilisha kazi zilizobaki ili  waweze kupata huduma  za Afya, badala ya kwenda mbali kama Songea  mjini  na vijiji jirani kufuata  matibabu mara kwa mara.

Romanus Komba(63)  mjumbe wa  kamati ya ujenzi alisema, fedha hizo zililetwa na Halmashauri kupitia idara ya Afya kwa ajili ya kumalizia  kazi ndogo ndogo,  lakini wao kama wahusika hawakushirikishwa katika matumizi  na hazikuwekwa kwenye akaunti yoyote  ya mradi bali zilibaki katika idara ya Afya na ndiko zilikopotea.

Alisema,  katika kikao cha mwisho kati ya uongozi wa Halmashauri na wajumbe wa kamati ya ujenzi, Halmashauri ilihaidi kurudisha fedha hizo lakini  mpaka sasa bado hazijarudishwa.

Alisema, kila wanapofuatilia katika ofisi ya mkurugenzi mtendaji  na  kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya wanapewa majibu yasio ridhisha na kukatisha tamaa, na kuiomba ofisi ya Mkuu wa mkoa kuingilia kati suala hilo.

Mary Mbawala,alisema, fedha hizo zikipatikana  haraka kuna uwezekano mkubwa  kazi ya ujenzi kukamilika na wananchi watapata matibabu jirani badala ya kwenda maeneo mengine kufuata huduma ya matibabu.

Alisema,  wanaopata tabu zaidi ni akina mama hasa wajawazito kwani pindi wanapata uchungu wanashindwa kwenda kujifungua katika kituo hicho kwa kuwa hakijakamilika  na baadhi ya vyumba vinavyotumiwa na wauguzi kutoa baadhi ya huduma hakuna faragha(usiri).

Alisema, badala yake wajawazito wanalazimika kwenda hadi Songea au Hospitali ya Misheni Peramiho kwa ajili ya kujifungua na kufuata huduma nyingine muhimu.

Boniventura Komba alisema, katika mradi huo kuna matatizo mengi yaliyotokea ikiwemo fundi  aliyepewa jukumu la kujenga nyumba ya mtumishi kutoroka bila kukamilisha kazi na kuiomba Halmashauri ya wilaya kumsaka fundi huyo ili aweze kumaliza ujenzi kwani ndiye iliyemtafuta na sio kamati ya ujenzi.

“tulikaa kikao kilichohudhuriwa na Mbunge Jenista Mhagama na viongozi wa Halmashauri wakiongozwa na  mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri Rajabu Mtiula, katika kikao kile Jenista aliagiza kurudishwa fedha na kutafutwa fundi aliyekimbia, halmashauri walihaidi kutekeleza maagizo hayo”alisema.

Hata hivyo wao kama wajumbe wa kamati ya ujenzi wanasikitika kuona viongozi  hao wamebadilika na kuwaagiza wamsake fundi ambaye hawamfahamu kwani  aliletwa na  Halmashauri na sio kamati.

Kwa upande wake mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Dkt Geofrey Kihaule alikiri kuwepo kwa suala hilo ambapo alisema, Halmashauri walitenga fedha za  nyongeza shilingi milioni 10 kwa ajili ya kukamilisha kazi ya ujenzi wa kituo,kumalizia nyumba ya mtumishi, kuingiza maji pamoja na umeme.

Alisema,  kati ya fedha hizo  shilingi milioni  mbili wamezitumia  kununua thamani za ofisini kwa ajili ya kituo, na walishindwa kuzipeleka fedha zote  kutokana na changamoto ya  mahitaji ya vituo vingine vilivyotakiwa kufunguliwa wakati ule ikiwemo Hospitali ya wilaya iliyopo kijiji cha Mpitimbi kata ya Mpitimbi.

Dkt Kihaule alisema,  kuna fedha ambazo wanategemea kupata  mwezi Januari  na mara zitakapofika ujenzi wa kituo hicho utafanyika  na kuwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati huu ambapo Halmashauri iko katika hatua ya mwisho kukamilisha ujenzi wa kituo  hicho na vituo vingine vya afya vinavyojengwa katika halmashauri hiyo.

Alisema, wana matumaini makubwa ifikapo mwezi Januari mwakani huduma za Afya katika  vijiji mbalimbali katika halmashauri hiyo zitaimarika na kuwataka wananchi waendelea kuunga mkono juhudi  zinazo fanywa za kuimarisha huduma hizo.

Akiongea kwa njia ya simu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Simon Bulenganija alisema, fedha hizo zilichukuliwa  kipindi cha tishio la ugonjwa wa Corona ili kununua vifaa na  pindi Halmashauri itakapokuwa na hali nzuri,  fedha hizo zitarudishwa ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa. Katibu wa mradi wa Sam unaoshughulika na kutoa elimu kwa wananchi wa kata tano katika halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma juu ya Uwajibikaji na Ushirikishwaji wa jamii miradi ya Afya kufahamu kama fedha zinazotolewa na Serikali kupitia mfumo wa force Akaunti wananchi wamehusishwa na wamewajibika akiongea na wananchi wa kijiji cha Mgazini kata ya Mgazini wilayani Songea. Picha zote na Mpiga na Muhidin Amri

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad