Waziri Hasunga aipongeza Benki ya CRDB kwa kuongeza tija kwenye kilimo - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 23, 2020

Waziri Hasunga aipongeza Benki ya CRDB kwa kuongeza tija kwenye kilimo

Waziri wa Kilimo, Mh. Japhet Hasunga ameipongeza Benki ya CRDB kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Benki hiyo katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo nchini ili kuharakisha maendeleo ya Watanzania mmoja mmoja na nchi kwa ujumla. Waziri Hasunga ametoa pongezi hizo katika hafla ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta iliofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na kampuni za ETC Agro, Loan Agro na Agricom.

Waziri Hasunga amesema pamoja na Serikali kuweka juhudi kubwa katika kuboresha sekta ya kilimo nchini, ni dhahiri kuwa bado wapo wakulima, hususan wakulima wadogo, ambao wamekuwa wakifanya kilimo duni kutokana na wengi wao kutomudu gharama za uendeshaji wa kilimo cha kisasa. Jambo ambalo linahitaji ushiriki wa taasisi za fedha na wadau wengine wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuwajengea uwezo kimtaji wakulima hao na kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (wa tatu kulia waliosimama) akishuhudia utiwaji wa saini wa mikataba ya makubaliano baina ya Benki ya CRDB na Kampuni washirika katika kilimo za ETC Agro, Loan Agro na Agricom watakazoshikiana nazo kwenye utoaji wa mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta kwa wakulima nchini, hafla ya uzinduzi huo imefanyika jana, katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia waliosimama ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.

“Nikiwa Waziri mwenye dhamana ya kilimo nimefurahishwa sana na ushirikiano huu wa utoaji wa huduma za uwezeshaji wakulima baina ya Benki ya CRDB na Kampuni za ETC Agro, LoanAgro na Agricom ambao unauzinduliwa rasmi leo hii. Uhusiano ambao unakwenda kuleta manufaa kwa wakulima kwa kuwawezesha kupata mikopo nafuu ya vifaa vya kilimo ikiwamo matrekta, power tiller, mashine za kuvunia na nyinginezo” alisema Waziri Hasunga.


Pamoja na matumizi ya zana za kilimo, Waziri Hasunga amewaomba wakulima kujikita katika kilimo cha kisasa kwa kuhakikisha wanaanza na utafiti wa masoko kabla ya kulima ili kujihakikisha uhakika wa kuuza mazao yao baada ya mavuno badala ya kuanza kulima bila kufahamu mahitaji ya soko na hivyo kuishia kutegemea serikali katika kutafuta masoko. Sambamba na hilo amewaomba makampuni na wanunuzi kuweza kuwekeza katika kilimo cha mkataba ili kuwahakikishia soko wakulima.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati akitoa hotuba yake katika hafla ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Kampuni za ETC Agro, Loan Agro na Agricom iliofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ameshauri Watanzania kujikita zaidi kwenye kilimo cha kisasa ili kuongeza tija na hivo kukuza kipato chao na taifa kwa kwa ujumla huku akisema Benki ya CRDB imejipanga kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa kwa kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa zana za kilimo kwa kushirikiana na kampuni za ETC Agro, Loan Agro na Agricom.


“Kama unavyofahamu Mheshimiwa kuna taasisi za fedha zaidi ya 58 nchini na kwa ujumla wao wanatoa asilimia 60 ya mikopo yote ya sekta ya kilimo wakati Benki ya CRDB pekee inatoa asilimia 40. Hii inadhihirisha adhma ya Benki ya CRDB ya kuunga juhudi za serikali za kuwaletea Watanzania maendeleo kwa vitendo kwa kuzingatia kuwa sekta ya kilimo inatoa ajira kwa takribani asilimia 75 ya Watanzania huku ikichangia asilimia 28 kwenye pato la Taifa” Alisema Nsekela.  


Nsekela alisema Benki ya CRDB inataka kuona mkulima ananufaika na juhudi zake na ndio maana Benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni za ETC Agro, Loan Agro na Agricom zimeungana kutoa mikopo hiyo ya zana za kilimo ambayo imezingatia mahitaji na uhalisia wa mazingira ya mkulima wa Kitanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Kampuni za ETC Agro, Loan Agro na Agricom iliofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam


“Tumepunguza riba ya mkopo kutoka asilimia 20 iliyokuwa ikitozwa hapo awali hadi kufikia asilimia 18, Tumepunguza kiwango cha gharama ya awali ya manunuzi kutoka asilimia 35 iliyokuwa ikilipwa na mteja hadi kufikia asilimia 25, ambapo hivi sasa asilimia 75 iliyobaki italipwa na Benki kama mkopo,” alisema Nsekela huku akibainisha kuwa sasa hivi mteja hata hitajika kuleta dhamana yoyote kwa ajili ya mkopo ambapo zana hizo zitatumika kama dhamana.


Mbali na matrekta mikopo hiyo ya zana za kilimo inajumuisha  power tiller kwa ajili ya kulimia, combine harvester kuvunia,  na zana nyinginezo, ambapo mteja anaweza kuchukua mkopo hadi wa shilingi bilioni 3 kwa kipindi cha miezi 36 hadi miezi 60.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Kampuni za ETC Agro, Loan Agro na Agricom iliofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Agricom, Bi. Angelina Ngalula ambao ni mmoja katika washirika wa Benki ya CRDB katika mikopo hiyo amesema wanaona ndoto yao ya kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini inakwenda kutimia kwa kupitia ushirikiano huo na Benki ya CRDB.


Bi. Ngalula amesema kuwa kampuni yao imeanza kufanya uzalishaji wa zana za kilimo nchini kupitia vijana wa Kitanzania ili kuchangia katika upatikanaji wa ajira. Kampuni hiyo inatarajia katika kipindi cha mwaka mmoja kuuza power tiller 500 ambazo zinahitaji trela 500 na trela zote hizo zitazalishwa nchini na kuchangia kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Hadi sasa Benki ya CRDB imeshatoa mikopo ya zaidi ya shilingi trilioni 1.6 kwa wadau wote katika mnyororo wa thamani katika kilimo, mikopo hii imeelekezwa katika maeneo kama vile; pembejeo na uendeshaji, zana za kilimo, ujenzi wa maghala, uunganishwaji na masoko na    uwekezaji kwenye viwanda.

Picha ya pamoja na baadhi ya Wafanyakazi wa Benki ya CRDB baada ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Kampuni za ETC Agro, Loan Agro na Agricom iliofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam
Picha ya pamoja na baadhi ya wakulima waliowakisha katika hafla ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta inayotolewa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Kampuni za ETC Agro, Loan Agro na Agricom iliofanyika katika viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akijaribu moja ya matreka.No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad