HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 23, 2020

Kagera yapunguza udumavu wa watoto chini ya miaka 5

 

Takwimu za udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano mkoani Kagera zimeendelea kupungua kutoka 41% hadi 39% kwa mwaka 2019 kutokana na wananchi kuendelea kuwa na mtazamo chanya kuhusu malezi ya watoto chini ya miaka mitano ikiwemo unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee mtoto anapijifungua mpaka kufikia umri wa miezi 6.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa uhamasishaji na uelimishaji maswala ya afya mkoa wa Kagera, Ndugu Nelison Rumbeli wakati wa shughuli ya wakina mama wenye watoto chini ya miezi sita iliyopewe jina la “Mother Meet up” ikimaanisha kina mama kukutana iiyofanyika jana katika ukumbi wa Bijampora kata ya Kemondo halmashauri ya Bukoba. Shughuli hiyo iliyoandaliwa na serikali kwa ushirikiano na mradi wa USAID Tulonge afya kupitia jukwaa la NAWEZA ilihusisha ushiriki wa akina mama wenye watoto chini ya miezi 6 zaidi ya 50.

Alisema kwa miaka mitano iliyopita kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano kilikuwa 41% ila kwa mwaka 2019 kiwango hicho kimeshuka na kufikia 39 %. Kushuka kwa kiwango hiki ni kutokana juhudi na msukumo wa serikali ya awamu ya tano katika kuboresha Sekta ya Afya. Pia Serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo USAID Tulonge Afya katika kuhamasisha maelezi bora kwa watoto kuanzia kipindi cha kuzaliwa mpaka anapofikisha umri wa miaka mitano.

Rumbeli alisema waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo alizindua na kusainiana mikataba na wakuu wa mikoa, na ngazi mbali mbali za uongozi hadi ngazi ya vijiji lengo likiwa ni kushughulikia swala la lishe kwani ni jambo kubwa lililokuwa linasumbua maeneo mbalimbali hapa nchini.

Aliongeza kuwa, vifo vya mama vinavyojitokeza wakati wa kujifungua mwaka jana vilikuwa 80 kwa mkoa wa Kagera na mwaka huu vifo hivyo vimepungua ambapo hadi sasa ni vifo 45. Kupungua kwa vifo hivyo kumetokana na ongezeko la ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na dispensary pamoja na ongezeko la madawa katika hospitali hizo. Lakini pia uhamiasishaji na elima waliyopatiwa wakina mama juu ya umuhimu wa kuhudhuria kliniki pindi wanahisi ujauzito. 

Kwa upande wa mratibu wa mradi wa USAID Tulonge Afya ngazi ya wilaya kutoka shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na maswala ya afya na mazingira (TADEPA) Benson Rweyemamu alisema kuwa, lengo la “shughuli ya Mother Meetup” ni kutoa nafasi kwa wakina mama wenye watoto chini ya miezi 6 kujadiliana na kupeana uzoefu juu ya malezi ya mtoto kuanzia kipindi anazaliwa mpaka kufikisha umri wa miaka 5 na kuwafanya wao pia kuwa Mabalozi wazuri kwenye jamii zao. Mambo muhimu yaliyojadiliwa kwenye shughuli hii ni unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi 6 kutokea mtoto anapozaliwa, kufuatilia matibabu kwa wataalam wa Afya pindi wanapohisi mtoto anatatizo, kulala kwenye chandarua chenye dawa na matumizi ya njia za kisasa za afya ya uzazi.


Rweyemamu aliongeza shughuli hiyo ya “Mother Meetup” hufanyika kila baada ya miezi sita na walengwa ni wakina mama wenye watoto chini ya miezi sita. Katika shughuli ya leo waalikwa wametoka katika kata saba za halamshauri ya Bukoba ambazo ni za Maruku, Kemondo, Kanyangereko, Katerero, Karabagaine, Nyakato na Katoro. 

Naye Meneja mradi wa Tulonge afya kwa kanda ya ziwa Ndugu Sihiana Mkanda alisema Tulonge Afya ni mradi wa miaka mitano unaotekelezwa kwa ufadhili wa shirika la kimarekani la USAID kwenye mikoa 12 nchini Tanzania. Kwa upande wa kanda ya Ziwa mradi unatekelezwa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Shinyanga na Kigoma.

Alisema katika mikoa ya kanda ya ziwa mradi huo uko katika wilaya 12 na kwa mkoa wa Kagera ni katika wilaya za Muleba na Bukoba vijijini na kuwa walichagua wilaya hizo kutokana na changamoto ya afya walizokuwa nazo wanajamii wa wilaya hizo.

Mmoja wa wakina mama walioshiriki kwenye shughuli ya Mother Meetup Shemsa Nasoro alisema Katika shughuli hiyo amejifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na faida za kunyonyesha mtoto miezi sita tangu anapozaliwa bila kumpa kitu chochote, kumpeleka kituo Cha afya mara tu anapougua na matumizi ya njia njia za kisasa za Afya ya uzazi.

“Na mimi nikitoka hapa ntaenda kuwaeleza wakina Mama wenzangu ambao hawakuweza kufika hapa yote niliyojifunza leo ili tuweze kuwa na jamii yenye afya bora” alimalizia Shemsa. 

Msanii wa Bongo Fleva Mwasiti Almasi akiwatumbuisha akina Mama walioshiriki tamasha la elimu ya unyonyeshaji kwa wanawake wenye watoto wenye umri wa chini ya miezi sita maarufu kama Mothers Meet Up event iliyofanyika Bukoba chini ya mradi wa USAID Tulonge Afya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad