MAKOSA YA KUEPUKA KATIKA KUPIGA KURA, UCHAGUZI MKUU OKTOBA 2020 - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 23, 2020

MAKOSA YA KUEPUKA KATIKA KUPIGA KURA, UCHAGUZI MKUU OKTOBA 2020

 

 

Na. Paschal Dotto-MAELEZO

Kutokana na ukuaji wa teknolojia, huduma ya habari imekuwa ni nyenzo muhimu ya kuwaweka pamoja watu katika taifa lolote duniani. Teknolojia imeleta thamani kubwa ya habari hasa katika ukuaji na upatikanaji wa habari mitandaoni, ikihusisha Youtube, Facebook, Twitter, Instagram na mitandao mingine ya kijamii. Mitandao hii inawajibu mkubwa wa kujenga jamii na inapaswa kusimamiwa vyema na wamiliki hususan katika tukio muhimu la kikatiba kwa wananchi wa Tanzania ambao watakuwa na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwezi Oktoba, 2020. 

Ukuaji huo wa habari mitandaoni uliilazimu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo ipo kisheria kwa kifungu cha 4C cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, ikiwa na jukumu kubwa la kusimamia na kuratibu shughuli zote za uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara kutoa elimu ya mpiga kura kwa Watanzania wote wenye haki ya kufanya hivyo. 

Hivi karibuni NEC, ilikutana na wanahabari wanaotoa huduma ya habari mitandaoni na kuwapa mafunzo juu ya kuwaelimisha wananchi makosa mbalimbali yanayoweza kutokea na kuharibu mchakato mzima wa wananchi kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi katika ngazi zote.

Aidha, NEC ilifafanua makosa matano ambayo wananchi wanapaswa kuyaepuka ili kutekeleza vyema zoezi ya upigaji kura katika maeneo yao. Kwa kutambua umuhimu na haki hiyo ya kutekeleza jukumu hilo, NEC walitoa elimu kwa waandishi wa vyombo vya habari za mitandaoni ili waweze kuwaelimisha wananchi kuhusu makosa ya uchaguzi.

Afisa Elimu, Idara ya Habari na Elimu kwa Mpiga kura, Titus Mwanzalila alibainisha makosa hayo kuwa ni makosa ya uandikishaji ambayo yanatokana na mwananchi na mpiga kura kutoa taarifa za uongo kwa madhumuni ya kujipatia kadi ya mpiga kura.

“Makosa haya ni yale yanayotokea wakati wa uandikishaji na au uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura na yanaambatana na kutoa taarifa za uongo, kujiandikisha zaidi ya mara moja, kuomba kadi ya pili bila maelezo maalum na kutoa tamko linalohusu kupotea kwa kadi ya mpiga kura.Makosa haya yote yameainishwa katika kifungu cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na. 88(3)”, anaeleza Mwanzalila.

Alieleza kuwa kupatikana na hatia ya makosa hayo kwa mwananchi kutamuondolea sifa ya kutekeleza wajibu wake lakini pia adhabu yake ni faini isiyopungua laki moja au tatu au kifungo cha miaka miwili au vyote kwa pamoja 

Mwanzalila alibainisha makosa mengine kuwa yanaweza kutokea wakati wa uchaguzi, uteuzi, daftari na makosa yanayohusu kadi ya mpiga kura, katika kifungu namba 89A cha makosa ya wakati wa uchaguzi yameelezwa na kifungu namba 89(1) makosa ya uteuzi yameelezwa kwa hiyo mwananchi anapaswa kufuata sheria ili kutekeleza majukumu yake kikatiba bila kuvunja sheria.

Makosa yanayohusu daftari na kadi za wapiga kura katika Sheria ya Taifa ya uchaguzi ambayo yako katika kifungu namba 90(1) (9), ambapo kinamtaka mwananchi kutoghushi au kuharibu daftari la wapiga kura, lakini pia kutoharibu na kuchafua kadi ya mpiga kura.Kifungu hicho kinaeleza kuwa kufanya hivyo kutamsababishia mwananchi kupigwa faini ya shilingi laki mbili au kifungo cha miaka miwili jela.

Aliongeza kuwa makosa mengine ni yahusianayo na fomu za uteuzi au karatasi za kura yaliyoelezwa kifungu namba 91 (1) (a), kumdhamini mgombea urais zaidi ya mmoja kifungu namba 91(1) (b) kughushi au kutengeneza karatasi bandia kifungu namba 91 (1) (c) na msimamizi wa uchaguzi kushindwa kuweka alama rasmi katika karatasi ya kura imeelezwa katika kifungu namba 91(1) (d). Makosa yote yanaepukika ikiwa mpiga kura atafuata Katiba na Sheria katika kutekeleza wajibu wake.

Katika kutekeleza wajibu wa mwananchi kikatiba Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inaeleza kuwa ni makosa kutangaza uongo kijitoa kwa mgombea yeyote kwa wananchi ili kumsaidia mgombea mwingine kushinda. Kosa hili linaangukia kwenye kifungu namba 102 (2) (c), ambacho kinampa mhusika adhabu ya kupigwa faini ya shilingi laki mbili au kifungo cha miezi 12 au vyote kwa pamoja, lakini pia masuala ya rushwa yamelezwa kwenye kifungu namba 91 B na adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka mitano.

Kosa lingine ni pamoja na kutoa hongo au kushawishi kutoa hongo ambayo yameelezwa katika kifungu cha 94 na adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi laki tano na isiyozidi shilingi milioni moja au kifungo kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Kutokana na elimu inayotolewa na NEC kwa njia mbali mbali kupitia kwenye vyombo vya habari na mikutano mbalimbali, wananchi wanatakiwa kujiepusha na makosa yanayoweza kuwafanya kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kikatiba wa kupiga kura au kwa kufahamu au kwa kutofahamu ili wajiepushe kukumbana na kukumbana na mkono wa sheria na wakati mwingine adhabu zilizotajwa na Tume.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad