NI RASMI CHUO CHA MADINI KUWA SEHEMU YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 21, 2020

NI RASMI CHUO CHA MADINI KUWA SEHEMU YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

 

Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa (katikati) akizungumza jambo na viongozi mbalimbali katika hafla yakukabidhi Chuo cha Madini (MRI) kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyofanyika Agosti 19, 2020 katika kampasi ya Nzega. (kulia) ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Prof. William  Anangisye,   na (kushoto)  ni Mhe. A.C.P Advera Bulimba, Mkuu wa Wilaya ya Nzega.
Picha ya pamoja ya kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Nzega (kushoto), VIongozi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (katikati) na wafanyakazi wa Wizara ya Madini (kulia) wakisikiliza wakati wa hafla ya kukabidhi Chuo cha Madini (MRI) kulelewa na UDSM katika hafla iliyofanyika Agosti 19, 2020 Kampasi ya Nzega.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akieleza jambo katika hafla ya kukabidhi Chuo cha Madini (MRI) kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyofanyika Agosti 19, 2020 Kampasi ya Nzega. (Kushoto) ni Prof. William Anangiye Makamu Mkuu wa Chuo Cha Dar es salaam.


* Nyongo - Mabadiliko Yasiondoe Majukumu ya Msingi 

* Prof. Anangisye - Msihofu Chuo Kiko Mikono Salama


Asteria Muhozya na Steven Nyamiti, Nzega


Imethibitishwa kuwa sasa Chuo cha Madini kilichokuwa chini ya Wizara ya Madini kitakuwa sehemu ya Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam.

Hayo yalithibitishwa Agosti 19, 2020 wakati wa Hafla ya Kukabidhi Chuo hicho Kampasi ya Dodoma na Nzega Kulelewa kwa muda na Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam katika hafla iliyofanyika katika Kampasi ya Nzega Wilayani Nzega Mkoa wa Tabora . 

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo alisema kuwa Tukio Hilo ni moja ya hatua za uboreshaji wa Sekta ya Madini pamoja na kuhakikisha nchi ya Tanzania inazalisha wataalam wa kutosha na wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya madini kuanzia ngazi ya Astashahada hadi Stashahada ili nchi iweze kusimamia rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia bila kutegemea wataalam kutoka nje.

Alisisitiza kuwa, Serikali inaamini kuwa, ulezi wa Chuo cha Madini kama ilivyoelezwa kwenye mchakato wa awali, kitaendelea kutoa mafunzo ya mchundo na mafundi sanifu katika sekta ya Madini lengo likiwa kukifanya kitengamae hatimaye kiweze kujiendesha.

"Uleaji utakaotolewa na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam ulenge kukiimarisha Chuo Cha Madini Kitaaluma, kuboresha miundombinu na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi," Alisisitiza Nyongo.

Aliongeza kuwa, Mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa na UDSM yasilenge kuondoa majukumu ya msingi ya Chuo Cha Madini.

"Ni matarajio ya Serikali na Wizara kuwa Chuo hiki kitafikia viwango vya Kitaaluma vinavyokubaliwa Kitaifa na Kimataifa," alisema Nyongo.

Akielezea kwamba, kumekuwepo na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na kutokuwepo kwa Sheria ya kuanzishwa Chuo Cha Madini; uvamizi wa maeneo hususan KampasiI ya Nzega na kuongeza kwamba anaamini changamoto hizo zitatuliwa chini ya ulezi huo na kwamba , hafla hiyo ni matokeo ya utatuzi wa changamoto hizo.

Pia, alizungumzia hatua mbalimbali ambazo zimechukukiwa na Serikali, ambazo zimepelekea Sekta ya Madini sasa imeanza kukua kwa kasi kubwa, ambapo Mwaka 2019 iliongoza kwa Ukuaji kwa asilimia 17.7.

Alisema kutokana na jitihada hizi sasa mapato yanayotokana na madini yameongezeka ambapo katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 zilikusanywa Shilingi Bilioni 346 kutoka Shilingi Bilioni 194 Mwaka 2016/17, kwenye Mwaka 2019/2020 zlikusanywa zaidi ya Shilingi Bilioni 470 ambalo ndiyo lilikuwa lengo la Wizara.

"Malengo kwa Mwaka 2020/2021 ni kukusanya Shilingi Bilioni 543 , tunaweza kufika Bil 600 lakini pia tuna ndoto ya kukusanya Shilingi Trilioni Moja kwa Mwaka," alisema Naibu Waziri Nyongo.

Aliongeza kuwa, Rais Dkt. John Magufuli kwa muda mrefu amekuwa akisisitiza kuhakikisha rasilimali zetu ikiwemo madini zinasimamiwa kikamilifu ili ziweze kuwanufaisha watanzania ikiwa ni pamoja na kuimarisha Uchumi hatimaye kupunguza utegemezi.

Aliyataja mafanikio mengine tuliyoyapatikana kwenye Sekta ya Madini kuwa Ni pamoja na kutolewa kwa Leseni 221 za uchenjuaji wa Madini, Leseni 4 za uyeyushaji madini ( smelting) na Leseni 4 za usafishaji madini (refining).

Pia, alisema Wizara imetenga hekta 38.567 kwa ajili ya uchimbaji mdogo na kuwapatia mafunzo wachimbaji wadogo na kuwawezesha kutengeneza maisha yao bila bughudha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Nzega A. C.P Advera Bulimba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora 

alitoa Pongezi kwa Serikali kuchukua hatua za kuboresha Chuo hicho na kueleza Serikali ya Mkoa na Wilaya itashirikiana na Chuo kuhakikisha mazingira na mali za Chuo zinalindwa.

"Ni matarajio Chuo kitaongeza Usajili kulingana na mahitaji ya Chuo. Tunawahamasisha wazazi walete watoto wao ili kuboresha Mkoa wetu,"alisema A.C.P Bulimba.

Aliongeza kwamba Mkoa umefurahia kutokana na hatua hizo zilizochukuliwa kwa kuwa zitauwezesha Mkoa kupata fursa za kimapato kupitia fursa mbalimbali zitakazotolewa na Chuo hicho.

Aidha, aliwasisitiza wazazi Mkoani humo kuhakikisha wanapeleka watoto wao ili kupata Elimu zinazotolewa na Chuo hicho kwa Lengo la kuboresha Maendeleo ya Mkoa huo.

Naye, Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa alizingumza katika halfa hiyo alisema kuwa, wazo la Chuo Cha Madini kulelewa na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam lilitoka Wizara ya Madini mwezi Januari 2018 ambapo uamuzi ulikusudia kukiwezesha Chuo cha Madini kuongeza nafasi za udahili, kuendesha kozi zinazoendana na soko la ajira, kuongeza ufanisi katika maeneo  muhimu ya Utafiti,uchapishsji na kuongeza huduma zinazotolewa na Chuo cha Madini.

Akielezea uzoefu wa Chuo Kikuu Cha Dar katika kuvilea Vyuo vingine alisema kwamba, uzoefu unaonesha njia ya kulelewa na Taasisi kubwa zenye uzoefu ni bora zaidi katika kuziwezesha taasisi changa kujisimamia zenyewe.

"Chuo cha Ardhi- DSM ambacho kililelewa na UDSM kuanzia Mwaka 1996 mpaka Mwaka 2006 kilipoachwa kijiendeshe chenyewe na Chuo Kikuu icha Mzumbe wakati huo kikijulikana Kama Insitute of Development Management ( IDM) kililelewa na UDSM kwa kipindi Cha muda wa miaka 8 na baada ya hapo kiliweza kusimamia na kujiendesha chenyewe na sisi sote ni mashahidi wa mafanikio ya Vyuo hivi viwili," alisistiza Mhandisi Mulabwa.

Akielezea kuhusu hatua kadhaa zilizochukuliwa ambapo alisema kuwa, katika hatua za kukamilisha mchakato wa kulelewa, tarehe 20 Februari 2020 ilisainiwa Hati ya Makubaliano kati ya Wizara ya Madini, Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam ambayo iliandaa iliandaa utaratibu mzima wa kulelewa.

Pia, alisema kutokana na utaratibu uliowekwa katika Hati ya Makubaliano, mambo mbalimbali yalifanyika ikiwemo kutangazwa kwa Order ya kuanzishwa Chuo cha Madini katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na kuandaliwa kwa muundo wa Taasisi na Muundo wa Utumishi wa Chuo Cha Madini kubainisha Mali zilizopo chini ya Chuo Cha Madini.

" Ni Matumaini yangu kuwa utoaji wa mafunzo wa Chuo cha Madini utakuwa wa kiwango cha juu, udahili wa wanafunzi utaongezea nchini na kutoka nje ya nchi, miundombinu itaboreshwa na kutimiza jitihada za Serikali za kuhakikisha inakuwa na wataalam wazawa watakaofanya shughuli mbalimbali katika Sekta ya Madini,"" alisema Mhandisi Mulabwa.

Vilevile alisistiza kuwa, Chuo kitakapoachiwa kitakuwa na mifumo mizuri ya kujiendesha chenyewe

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Prof. William Anangisye alisema kuwa, kwa Chuo Cha Madini kuwa sehemu ya Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam , kinatarajiwa kupata fursa ya kuingia katika wigo mpana zaidi wa kitaaluma.

"Tunafurahi kuwa kwa kupitia mazungumzo ya pamoja kati ya wizara zetu mbili, yaani Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Madini, Sasa tumefikia muafaka kuwa Chuo cha Madini Dodoma kitakuwa sehemu ya Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam baada ya mchakato wake ambao ulianza tangu Mwaka 2018," alisema Prof. Anangisye. 

Aliongeza kwamba, Chuo Kikuu Cha UDSM kimegusa nyanja nyingi za kitaaluma ikiwemo taaluma ya Madini , ambapo Idara ya Jiolojia imetoa wataalam wanaoheshimika duniani na imekuwa na mchango mkubwa sana Kitaifa na kuongeza kwamba, jukumu hilo la kukilea Chuo Cha Madini

litatupeleka Chuo Cha UDSM kuwa karibu zaidi na Watanzania ambalo ndilo Lengo la chuo.

" Napenda niwa hakikishie Makatibu Wakuu wa Wizara zetu mbili kuwa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam kina uzoefu mkubwa wa kukuza taaluma baada ya Kukabidhiwa Vyuo mbalimbali vya Serikali," alisema Prof. Anangisye.

Prof. Anangisye aliwasisitiza Wafanyakazi na Watumishi wa Chuo cha Madini kuwa kuwa wako katika Mikono salama na hivyo hawapaswi kuwa na hofu yoyote ya kuwa sehemu ya chuo hicho.

" Masuala yanayohusu mustakabali wa wafanyakazi na wanafunzi, mali za chuo na mengine mengi, yalijadiliwa kwa kina na umakini mkubwa na Kamati Kuu ya kusimamia Ujumuishaji wa Chuo cha Madini Dodoma kwenye Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam. Sisi tunazingatia yote yaliyopendekezwa na kukubaliwa na tutazingatia wajibu wetu kukiboresha Chuo cha Madini na kuimarisha viwango vyake vya taaluma," alisema

Akizungumzia nafasi ya Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam katika kuendeleza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli katika kuiendeleza Sekta ya Madini Nchini, alisema moja ya matokeo ya uongozi wake ni kuboresha Sekta ya Madini na kuifanya kuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi yetu, hivyo Chuo hicho kinachukulia hatua ya Kukabidhiwa Chuo cha Madini kama sehemu ya Utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kukuza Sekta ya Madini.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Madini Elvanus Kapira alialeza kwamba Menejimenti ya chuo inaamini kwamba kupitia mpango wa kulelewa, Chuo cha Madini kitaimarika katika nyanja za kielimu, kitafiti, pamoja na huduma za kutoa ushauri Elekezi huku changamoto zote zinazokikabili Chuo ambazo zinapelekea kukua kwa kasi isiyolizisha zitatatuliwa chini ya mpango wa kulelewa na Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam.

Alisema kuwa, menejimenti na wafanyakazi wote wa Chuo cha Madini wanaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chote cha mpango kulelewa ili kufanikisha malengo mahususi ya kuboresha elimu na huduma zinazotolewa na Chuo cha Madini kwa masilahi mapana ya Taifa letu.

" Menejimenti ya Chuo cha Madini inaishukuru Wizara ya Madini kwa jitihada ilizochukua kwa ajili ya kukiendeleza Xhuo Cha Dar Es Salaam na pia inaishukuru Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam kwa kuridhi kukilea Chuo hiki," alisema Kapira.

Pia, Kapira akielezea mafunzo yanayotolewa na Chuo hicho na kusema pamoja na mafunzo ya muda mrefu , Chuo Cha Madini kinatoa mafunzo ya muda mfupi pamoja na mafunzo Maalum kwa Wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Chuo cha Madini kilianzishwa Mwaka 1982 kwa lengo la kutoa mafunzo ya Ufundi sanifu katika Sekta ya Madini. Chimbuko la kuanzishwa kwake ni uhitaji uliokuwepo wa wataalm wa kada za ufundi katika miradi ya utafiti, wa maji, Madini ya Bati na metali nyingine uliojulikana Kama Mineral and Ground Water Exploration Project ( MGWEP) Mkoani Kagera.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad