HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 21, 2020

WAKULIMA KUENDELEA KUNUFAIKA NA MUUNGANO WA TANZANIA NA ZANZIBAR- KUSAYA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiongea na wakulima wa skimu ya umwagiliaji zao la mpunga Kwalempona wilaya ya Wete Pemba jana alipokagua kukamika kwa miundombinu yake. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Wete Mhe.Kombo Asa Juma aliyeshiriki ziara hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua skimu ya umwagiliaji mpunga ya Ole Dodea Chake Chake inayotumia mabomba alipotembelea Pemba jana.Mradi huo unatekelezwa kupitia mradi wa ERPP na umegharimu shilingi Bilioni 1.7 
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akitembelea kukagua skimu ya umwagiliaji zao la mpunga ya Kwalempona wilaya ya Wete Pemba hapo jana.Kukamilika kwa skimu hiyo chini ya mradi wa ERPP umesaidia wakulima zaidi ya 120 wengi wao akina mama kuzalisha mpunga na kuwa na uhakika wa kipato.
 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo ( Bara) Bw.Gerald Kusaya akisalimiana na mwenyeji wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (Zanzibar) Bi.Maryam Abdulla mara baada ya kuwasili uwanja wa Ndege Pemba jana kwa ziara ya kikazi.

Wakulima wa Pemba wameanza kunufaika na miradi ya kilimo inayotekelezwa kwa pamoja na serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar ya uendelezaji zao la mpunga (ERPP) na mradi wa Kudhibiti Sumukuvu nchini (TANIPAC).

Mradi wa Kuimarisha Uzalishaji Mpunga nchini (ERPP) umetumia shilingi Bilioni mbili kujenga na kukarabati miundombinu ya skimu za umwagiliaji upande wa Pemba kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Akizungumza wakati akitembelea miradi ya umwagiliaji ya Ole Dodea Chake Chake na Kwalempona Wete Pemba jana (20.08.2020) Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alisema miradi hiyo inathibitisha uimara wa Muungano uliopo .

“ Nimetembelea na ninawapongeza wenzetu wa Zanzibar kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi hii ya umwagiliaji kwani wakulima wameonesha mafanikio ya kuongeza tija ya uzalishaji zao la mpunga na pia thamani ya fedha inaonekana” alisema Kusaya.

Kusaya aliwaeleza wakulima wa Pemba kuwa miradi hiyo ya umwagiliaji ni zawadi toka kwa marais wetu ambapo amewasihi kuitunza na kuifanya iwe endelevu kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Skimu ya Umwagiliaji ya Ole Dodea Chakechake ina ukubwa wa hekta 10 maalum kwa uzalishaji mbegu bora za mpunga na tayari wakulima 62 wameanza kunufaika kulima huku ikigharimu shilingi Bilioni 1.7 kukamilika wakati skimu ya Kwalempona wilaya ya Wete ina eneo la hekta 13 na wakulima 120 wengi wao akina mama wanalima mpunga na imetumia shilingi Milioni 753 kukamilika.

Katibu Mkuu Kusaya akizungumza na wakulima hao alisema ni lengo la serikali kuona wakulima wakilima eneo dogo lakini wavune zaidi na kupata faida kupitia kukamilika kwa skimu hizo za umwagiliaji .

“ Wakulima tunzeni miradi hii na fikirieni kuanza kuchangia fedha kidogo ili mradi uwe endelevu ikitokea miundombinu imeharibika basi iwe rahisi kutumia fedha zenu kuikarabati na kupunguza utegemezi wa serikali” Kusaya aliwasihi wakulima wa Wete.

Katika hatua nyingine Kusaya alitoa wito kwa wakulima nchini kote kuwafundisha na kuwazoesha watoto wao ili washiriki kazi ya uzalishaji mashambani na kuwa na uhakika wa kipato kufuatia taarifa ya mradi wa Kwalempona kuonesha idadi kubwa ya akinamama ndio wanalima kwenye bonde hilo pekee.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa Kwalempona Wete Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakulima Shaibu Ali alisema hapo mwanzo walipata ugumu wa kulima mpunga kwenye bonde hilo kutokana na mitaro kuwa ya udongo hivyo maji mengi yalipotea lakini sasa skimu imeboreshwa .

Mkulima huyo aliongeza kusema mradi wa ERPP umesaidia wakulima kuwa na uhakika wa kulima mpunga mara mbili kwa mwaka na kuongeza mavuno toka wastani wa tani 2 kwa hekta hadi tani 5 na matumizi ya mbegu bora za mpunga.

Naye Juma Shamani Juma mkulima wa Wete alisema “ nilizoea kupanda mpunga aina ya Linga na kuvuna poro 36 ( roba za kilo mia ) katika ploti yangu lakini sasa hivi tumetumia mbegu bora na mavuno yameongezeka hadi wastani wa poro 50 ( sawa na nusu tani) kwa robo hekta” alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar Maryam Abdulla serikali kupitia mradi wa ERPP inahamasisha wakulima kutumia mbegu bora za mpunga ili wapate mavuno mengi toauti na mbegu za asili aina ya linga.

Katibu Mkuu huyo alishukuru serikali ya Muungano wa Tanzania kupitia wizara ya Kilimo kuwa na miradi ya ushirikiano na Zanzibar kwani inaendeleza udugu na kueleza kuwa wakulima wataendelea kufundishwa kanuni bora za kilimo ili waongeze uzalishaji mpunga na mazao mengine ili kuwa na uhakika wa ajira na kipato.

“ Rais Dkt.Ali Mohamed Shein ameagiza wizara ya Kilimo Zanzibar kutuma wataalam kwenda Bara kwa ajili ya kujifunza namna ya kufufua zao la korosho ili wakulima wa visiwani humo wawe na zao jingine la biashara na kukuza uchumi wao” alisema Maryam

Mradi wa Kuimarisha Uzalishaji Mpunga (ERPP) ulianza kutekelezwa mwaka 2015 kwa gharama ya dola za kimarekani milioni 22.9 na utafikia mwisho mwaka 2021 ambapo kwa upande wa bara unatekelezwa kwa kujenga skimu 5 ,maghala 5 yamekamilika na ujenzi wa maabara moja ya kilimo mkoani Morogoro na kwa upande wa Zanzibar jumla ya skimu 9 zimejengwa .

Katibu Mkuu Kusaya amekamilisha ziara yake ya siku mbili ya kutembelea miradi ya Kudhibiti Sumukuvu na ile ya Uimarishaji Uzalishaji Mpunga (ERPP) kwa upande wa Zanzibar na Pemba hapo jana.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad