BENKI YA CRDB YATOA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 17 KWA SERIKALI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 10, 2020

BENKI YA CRDB YATOA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 17 KWA SERIKALI

Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Mpango akipokea mfano wa hundi ya gawio la shilingi bilioni 9.3 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (watatu kushoto) kutokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya benki hiyo kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa DANIDA kwa kushirikiana na Serikali ya Denmark. Waziri Mpango leo amepokea jumla ya gawio la shilingi bilioni 17 kutoka Benki ya CRDB ikiwa ni gawio kutokana na uwekezaji wa Serikali kuu, taasisi na mashirika yake. Wengine pichani ni Waziri wa TAMISEMI, Suleiman Jaffo (wanne kushoto), Waziri wa Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (watatu kulia), Balozi wa Denmark Nchini, Mette Dissing-Spandet (wapili kulia), Msajili wa Hazina, Athman Mbuttuka (wakwanza kulia), Makamu Mwenyekiti wa Bodi Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (wakwanza kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.

Waziri wa Fedha na Mipango Dokta Philip Mpango amepokea gawio la shilingi bilioni 17 linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay.

Makabidhiano hayo ya hundi kifani yalifanyika katika ukumbi wa Kambarage, Wizara ya Fedha na Mipango Dodoma na kuhudhuriwa na baadhi ya mawaziri na viongozi mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma yenye hisa ndani ya Benki ya CRDB na Menejementi ya Benki ya CRDB.

Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Mpango aliipongeza Benki hiyo kwa kutoa gawio kwa Serikali na kwa kupata faida katika biashara yake katika kipindi cha mwaka 2019/20 ambayo yamepelekea kuongezeka kwa gawio kwa Wanahisa  ikiwamo Serikali.


Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Benki ya CRDB ilitoa gawio la shilingi bilioni 10 kwa Serikali na mwaka 2019/2020 imetoa gawio la shilingi bilioni 17 jambo ambalo Dkt. Mpango alisema nimapinduzi makubwa katika utendaji wa benki hiyo.

Waziri wa Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama (wapili kulia) akipokea gawio la shilingi bilioni 5.8 kutoka Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (wapili kushoto) na kumkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF, Hosea Kashimba (wakwanza kulia), kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela. Benki ya CRDB leo imekabidhi jumla ya gawio la shilingi bilioni 17 kutokana na uwekezaji wa Serikali kuu, taasisi na mashirika yake.


“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki yetu ya CRDB inazidi kuimarika zaidi kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo Watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii”, alisema Dkt. Mpango.


Dkt. Mpango alisema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitakwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeianisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2020/2021 hususan sekta ya afya. “Kipekee kabisa niipongeze Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB kwa kazi nzuri mnayoifanya,” aliongezea Dkt. Mpango.


Aidha, aliipongeza Benki ya CRDB kwa matokeo mazuri ya biashara iliyopata katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2020 ambapo faida ya Benki imeongezeka kwa asilimia 15 kufikia shilingi bilioni 70.4 kutoka TZS bilioni 61.1 zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2019. “Mkiendelea na kasi hii mwakani tunategemea kupata gawio nono zaidi,” alisisitiza Dokta Mpango.

Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa taasisi za fedha katika maendeleo ya taifa, Dkt. Mpango aliipongeza Benki ya CRDB kwa kupunguza riba katika mikopo kutoka asilimia 24 kufikia wastani wa asilimia 18 na 14 ili kuchochea shughuli za maendeleo nchini. “Niwapongeze kwa kupunguza riba katika mikopo, hiki kimekuwa kilio cha muda mrefu cha Serikali kwa mabenki nchini, niyasihi mabenki mengine kufuata nyayo hizi za Benki ya CRDB,” alisema Dkt. Mpango.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, alisema kuwa gawio hilo ni sehemu ya faida ya shilingi bilioni 120.1 baada ya kodi ambayo Benki ya CRDB na kampuni zake tanzu imeipata katika mwaka wa fedha 2019/2020 na kuahidi kuwa  Benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora ili kukidhi mahitaji ya wanahisa wake na wananchi kwa ujumla.


“Katika Mkutano wa Wanahisa uliofanyika kidijitali mwezi Juni mwaka huu, Wanahisa wa Benki ya CRDB walipitisha kwa pamoja gawio la shilingi 17 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 112.5 na hivyo kufanya gawio la mwaka huu kufikia jumla ya shilingi bilioni 44.4,” aliongezea Dkt. Laay.
Aidha, Dkt. Laay aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji mzuri ambao umeiwezesha Benki ya CRDB kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuahidi kuendelea kushirikiana nayo ili kukuza uchumi wa nchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alimhakikishia Dokta Mpango kuwa Benki ya CRDB kupitia kauli mbiu yake ya “Tupo Tayari” itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha nchini huku akielezea kuwa benki hiyo sasa hivi imejikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya kidijitali ya kutolea huduma kama CRDB Wakala, SimBanking, SimAccount na Internet banking ambayo humsaidia mteja kupata huduma kwa urahisi, unafuu na haraka.


Akipokea gawio kutokana na uwekezaji wa Halmashauri za Mbinga, Lindi, Shinyanga, Mufindi, Chunya na Rungwe, Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Suleiman Jaffo alizihimiza halmashauri nyingine nchini kuwekeza katika hisa ili kupanua wigo wa mapato katika halmashauri zao.

Naye Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alipongeza mifuko ya jamii ya PSSSF, NSSF na ZSSF kwa uwekezaji ndani ya Benki ya CRDB huku akiwataka viongozi wa mifuko hiyo kutumia gawio walilopata kuboresha utendaji kazi ili kunufaisha wanachama wa mifuko hiyo.

Kwa upande wake Balozi wa Denmark Tanzania, Mette Dissing-Spandet amesema Serikali ya Denamark inajivunia kwa uwekezaji ulioufanya ndani ya Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa DANIDA huku akibainisha kwa pamoja Serikali hizo zimekubaliana kuelekeza gawio hilo katika kuboresha sekta ya afya nchini.


Serikali ndio mwanahisa mkubwa ndani ya Benki ya CRDB kutokana na kuwa na umiliki wa asilimia 21 kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA kushirikiana na Serikali ya Denmark, huku taasisi na mashirika ya umma yakiwa na umiliki wa hisa za asilimia 17.1.

Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Mpango akitoa hotuba yake katika hafla fupi ya kupokea jumla ya gawio la shilingi bilioni 17 kutoka Benki ya CRDB ikiwa ni gawio kutokana na uwekezaji wa Serikali kuu, taasisi na mashirika yake, iliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo.
Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama akitoa hotuba yake katika hafla fupi ya kupokea jumla ya gawio la shilingi bilioni 17 kutoka Benki ya CRDB ikiwa ni gawio kutokana na uwekezaji wa Serikali kuu, taasisi na mashirika yake, iliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo.
Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Suleiman Jaffo akitoa hotuba yake katika hafla fupi ya kupokea jumla ya gawio la shilingi bilioni 17 kutoka Benki ya CRDB ikiwa ni gawio kutokana na uwekezaji wa Serikali kuu, taasisi na mashirika yake, iliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay akitoa hotuba yake katika hafla fupi ya kukabidhi hundi zenye jumla ya gawio la shilingi bilioni 17 kutoka Benki ya CRDB ikiwa ni gawio kutokana na uwekezaji wa Serikali kuu, taasisi na mashirika yake, iliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akitoa hotuba yake katika hafla fupi ya kukabidhi hundi zenye jumla ya gawio la shilingi bilioni 17 kutoka Benki ya CRDB ikiwa ni gawio kutokana na uwekezaji wa Serikali kuu, taasisi na mashirika yake, iliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo.
 Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akitoa hotuba yake katika hafla fupi ya kukabidhi hundi zenye jumla ya gawio la shilingi bilioni 17 kutoka Benki ya CRDB ikiwa ni gawio kutokana na uwekezaji wa Serikali kuu, taasisi na mashirika yake, iliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo.
 Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori akitoa shukrani za Bodi kwa Serikali baada ya katika hafla fupi ya kukabidhi hundi zenye jumla ya gawio la shilingi bilioni 17 kutoka Benki ya CRDB ikiwa ni gawio kutokana na uwekezaji wa Serikali kuu, taasisi na mashirika yake, iliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma leo.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad