Na WAMJW- ARUSHA
MKURUGENZI
wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt. Grace Magembe ametoa wito kwa Watoa huduma za Afya wote nchini
kufanya kazi kwa kushirikiana baina yao na viongozi wao ili kuboresha
huduma za afya nchini.
Dkt. Grace, ametoa wito huo wakati
alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya, na kuongea na
Watumishi juu ya njia za uboreshaji huduma za afya katika hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Arusha - Mount Meru.
"Ninawaomba sana tufanye
kazi kwa umoja na ushirikiano, migongano na misuguano haileti maana
yoyote katika kuwahudumia Watanzania, kama kuna mwenzetu katoka nje ya
mstari, tuambiane ukweli na tuonyane bila kuleta misuguano" alisema Dkt.
Grace.
Aliendelea kusema kuwa, Serikali imeendelea kujenga
vituo vya kutolea huduma za afya, na kuboresha vilivyo chakaa, hivyo ni
wakati wa watoa huduma kushirikiana kwa karibu na kufanya kazi kwa
juhudi na ubunifu ili kuleta matokeo chanya katika utoaji huduma.
Hata
hivyo, Dkt. Grace amesisitiza agizo la Mganga Mkuu wa Serikali juu ya
kuongeza jitihada katika mapambano ya kuendelea kupunguza vifo vya mama
na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya, ndani ya miezi sita.
"Licha
ya kuendelea kufanya Juhudi kubwa katika kupunguza vifo vya mama na
mtoto, bado tuna namba kubwa ya vifo hivyo, kama Serikali inaongeza
vituo na kuboresha huduma, kwanini vifo bado vipo juu, na mara nyingi
vifo vingi vinaweza kuzuilika" alisema Dkt. Grace.
Mbali na hayo,
Dkt. Grace ametoa rai kwa viongozi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Arusha - Mount Meru kuhakikisha wanajiongeza ili kuongeza ukusanyaji
mapato, jambo litalosaidia katika kuboresha huduma kwa wagonjwa.
Pia,
Dkt. Grace ameagiza uongozi wa hospitali kuweka mpango mkakati mzuri
wa matengenezo ya vifaa na kuhakikisha vipimo vyote vinafanyiwa uhakiki
wa ubora na majibu yote yakaguliwe na yasainiwe na aliyepima na
kuthibitishwa kabla ya kurudi kwa mgonjwa, katika ngazi zote ikiwemo
maabara na mionzi.
Aliendelea kusema kuwa, kila muuguzi ni
lazima awe na mpango wa huduma ya mgonjwa wake (nursing care plan),
ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma kwa mgonjwa anaemhudumia.
Nae
Mkurugenzi wa uhakika ubora wa huduma Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Eliakim Eliud ametoa rai kwa
viongozi kushughulikia malalamiko ya wagonjwa kwa haraka, huku akiagiza
namba za viongozi zibandikwe maeneo yanayoonekana na ziandikwe kwa
kuonekana.
Aidha, aliwataka watoa huduma kutoa majibu kwa
wagonjwa haraka pindi wanapowahudumia ili kufahamu wanasumbuliwa na
shida gani, kuliko kuwapa dawa bila kuwapa mrejesho wa magonjwa
yanayomsumbua.
Mbali na hayo, Dkt. Eliakim amewataka Watumishi
wote katika maeneo ya kutolea huduma za afya kuboresha maadili, ikiwemo
matumizi mazuri ya lugha kwa wanaokuja kupata huduma, kuanzia
wanapoingia getini mpaka wanapomaliza kupata huduma, ili kupunguza
malalamiko yasiyo na ulazima.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Arusha Dkt. Alfello Sichalwe ameishukuru Serikali kupitia Wizara
ya Afya kwa kuendelea kuboresha huduma katika Mkoa wa Arusha, huku
akiahidi kuendelea kusimamia vizuri hali ya afya ikiwemo kupunguza vifo
vya mama na mtoto katika Mkoa huo.
Mkurugenzi
wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt. Grace Magembe (wakwanza kushoto) akijadiliana jambo na Mkurugenzi
wa uhakiki ubora Wizara ya Afya Dkt. Eliakim Eliud na Daktari katika
wodi ya wagonjwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Arusha - Mount Meru.
Mkurugenzi
wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt. Grace Magembe (wakwanza kushoto) akiongea na moja kati ya wagonjwa
waliofika kupata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha -
Mount Meru, ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kukagua hali ya utoaji
huduma za afya Mkoani Arusha
Mkurugenzi
wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt. Grace Magembe akiwa na Mtaalamu wa maabara, akikagua idadi ya
wagonjwa walio katika mfumo wa kupata huduma katika maabara ya Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa Arusha - Mount Meru.
No comments:
Post a Comment