HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 17, 2020

DC MAGU AWAKUMBUSHA WATENDAJI KWENDA KWA WANANCHI


NA BALTAZAR MASHAKA

MKUU wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, amewaagiza watumishi wa serikali wilayani humo washuke chini wakawasikilize wananchi ili wafahamu kero zao na kuzitatua badala ya kung’ang’ania ofisini na kuahidi kufuata nyayo za waliomtangulia.

Alitoa maagizo hayo jana wakati akijitambulisha kwa Maafisa Tarafa za Sanjo, Itumbili, Ndagalu na Kahangara jana ambao pia walimweleza baadhi ya kero zinazowakabili wananchi kwenye tarafa zao.

Watumishi wa serikali waliopewa dhamana ya kutumikia wananchi watoke ofisini na washuke chini waende kwa wananchi kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi vinginevyo zitawaangusha wote na katu yeye hatakuwa mtu wa ofisini muda wote.

“Tutenge muda wa kuwasikiliza wananchi, tuwe wa kwanza kufahamu changamoto na kero zao, twendeni tuishi na shida za watu wala tusiogope mikutano ya hadhara hata wakikusema, nataka wananchi wahudumiwe.Sitakuwa Mkuu wa Wilaya wa kukaa ofisini muda wote nitakuwa sitekuwasilikiza, tusisubiri waje viongozi wa kitaifa kushughulikia kero zao,vinginevyo tutanguka nazo,”alisema Kalli.

Pia aliwambia wakafuatilie miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao iwe ya serikali kuu, halmashauri ama iliyoibuliwa na wananchi wenyewe, waipitie ili kufahamu ilipaswa kukamilika lini, imekwama wapi na kwa nini ilhali fedha zimetolewa.

Alisema mwaka huu wa fedha anahitaji kuona mpango kazi wa maofisa tarafa hao kuhusu miradi ya maendeleo na vipaumbele vya maeneo yao kwani hayo ndiyo watakayopimwa nayo kwenye utendaji wao ambapo aligusia nidhamu ya watumishi kwa CCM iliyopewa dhamana ya kuongoza dola wala wasione aibu kuitetea.

“Tumepewa dhamana kubwa na serikali, ni wajibu wetu kufuatilia miradi tujue kitu gani kimekwamisha.Tukiyafanya hayo kwa nini Magu isiendelee.Pia tutimize wajibu tuwaeleze wananchi shughuli za maendeleo zilizotekelezwa na serikali wajue maana wanatakiwa wapate manufaa kutokana na CCM,”alisema Kalli.

Aidha Afisa Tarafa ya Sanjo, Aron Laizer alisema huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi na Kituo cha Afya Kisesa hazikidhi na kushauri kitazamwe kwa jicho la tatu lakini pia kero ya maji ya muda mrefu ni changamoto kubwa.

Afisa Tarafa ya Kahangara Jeremiah Anthony yeye alidai mwekezaji wa mradi wa kuku wa mayai katika Kata ya Nyanguge amebadilisha uelekeo wa maji kwa kujenga mtaro unaoelekeza maji kwenye makazi ya watu ambapo kipindi chote cha mvua kaya nyingi zilikuwa kwenye taharuki kubwa na kuomba serikali ya wilaya ichukue hatua.

Akijibu changamoto hizo Mkuu wa Wilaya alisema serikali ipo kwa maslahi ya wananchi na hivyo hatataka kusikia maofisa tarafa wasio sikiliza kero za wananchi na kuomba washirikiane kwa pamoja kwani hakuna mwenye cheo bora, wote ni sawa.

“Kabla ya kuanzisha jambo iwe miradi ya kijamii au ya wawekezaji washirikisheni wananchi wajue ili kuepusha migogoro, tupo kumsaidia Rais kuleta maendeleo ya wananchi,lakini nachukia watu wa kuniingiza chaka, sihitaji kurithi uadui wa mtu na hilo sitakubali.Hili la maji na mwekezaji tutalishughulikia, nafahamu walionitangulia kuna mazuri wamefanya ambayo bado tutaendelea kuyaboresha,”alisema Kalli. 
 
Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kumpa dhamana yakumsaidia kuwatumikia wananchi wa Magu hivyo atamwonyesha imani hiyo na uaminifu kwa kuyafanya yaliyo ndani ya uwezo wake akishirikiano na watumishi wengine kuwatumikia wananchi.
 MKUU wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, akiwa kwenye kikao kazi na Maofisa Tarafa za Wilaya hiyo jana ambapo alitaka watoke ofisini wakawasilikize wananchi nabkutatua kero zao.
 Mofisa tarafa nne za Wilaya ya Magu wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Salum Kalli (aliyevaaa tai) wakati wa kikao cha kukumbushana majukumu kilichofanyika katika ofisi ya mkuu huyo jana.Picha zote na Baltazar Mashaka

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad