NMB yawezesha Kilimo cha katani nchini, yatoa shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya matrekta - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 10, 2020

NMB yawezesha Kilimo cha katani nchini, yatoa shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya matrekta

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amevutiwa na juhudi kubwa iliyofanywa na Benki ya NMB katika kilimo cha Katani mkoani Tanga, baada ya benki hiyo kutoa matrekta 11 yenye thamani ya Sh Bilioni 1.

Akizungumza baada ya kukabidhi matrekta hayo, Majaliwa alisema wakulima wa Mkonge hawana budi kutumia vema fursa ya uwepo wa NMB ambapo aliwahimiza kuyatumia vema kwa manufaa ya wote na kuongeza tija kwenye kilimo cha mkonge.

Waziri Mkuu alipokea matrekta hayo katika hafla iliyofanyika nje ya kiwanda cha kuchakata singa cha Mwelya wilayani Korogwe, mkoani Tanga hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi mkoani humo.

“NMB ni benki yenye watu wabunifu, nimeshuhudia hata kwenye mazao mengine ya kimkakati kama Pamba na Korosho; wakiwakopesha wakulima na mimi mwenyewe hukabidhi matrekta hayo, hivyo wakulima mnatakiwa kuchangamkia benki hii yenye matawi nchi nzima,” alisema Majaliwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela ambaye alikuwepo kwenye tukio hilo alisema mkoa wake utahakikisha matrekta hayo yanatumika kama yalivyokusudiwa na kwamba kama atatokea mkulima au mfanyakazi yeyote kutaka kuyahujumu sheria zitachukua mkondo wake.

“Matrekta haya ni ukombozi mkubwa kwa wakulima wa Mkoa wa Tanga, kwa sababu huko nyuma walikuwa wakinyonywa na Katani Limited kiasi cha kutokopesheka kabisa, lakini hivi sasa Serikali imefanyia maboresho ili waweze kufaidika na zao hili muhimu kwa uchumi wa taifa,” alisema Shigela.

Awali akizungumza katika makabidhiano hayo, Afisa Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Biashara Benki ya NMB, Filbert Mponzi alisema benki hiyo  inatambua kilimo ni moja ya kipaumbele cha Taifa kwa kuwa takwimu zinaonyesha Watanzania zaidi ya asilimia 80 wanaoishi vijijini na mijini wanategemea kilimo.

Kwa kulitambua hili, NMB imefungua akaunti za wakulima zaidi ya 800 katika vyama vitano vya ushirika vya msingi vinavyoendesha mashamba ya mkonge ya  Ngombezi, Magunga, Mwelya, Hale na Magoma mkoani humo.

“NMB imetoa mikopo ya jumla ya Sh Bilioni 1.024 kwa vyama vinne vya ushirika vya msingi vya Ngombezi, Magunga, Mwelya na Magoma kwa  ajili ya ununuzi wa matrekta 11 na matrela 22, ili kuwezesha usafirishaji wa mkonge kutoka kwenye mashamba ya wakulima kwenda kwenye viwanda vya uchakataji wa mkonge,” alisema Mponzi na kuongeza:

“Mikopo hii itawanufaisha wakulima wa mkonge zaidi ya 949 walioko kwenye mashamba hayo. Upatikanaji wa matrekta hayo utaongeza tija na faida kwa vyama vya ushirika vya msingi na wanachama na itakuwa chachu ya kuongeza uzalishaji wa zao la mkonge. Vilevile benki ya NMB imeendelea kutoa mikopo kwa mkulima mmoja mmoja na wachakataji wa mkonge na hadi sasa zaidi ya Sh Bilioni 3.4 zimeshatolewa.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa vyama vya msingi vya ushirika wa wakulima wadogo wa mkonge (Amcos) wilayani Korogwe, Greyson Nyari alisema: “Tunaishukuru Benki ya NMB kutukabidhi matrekta haya ikiwa ni mkopo nafuu, yatatusaidia kuendesha shughuli za kuhudumia mashamba, tutachonga barabara za kuingia mashambani na kusombea  majani ya mkonge kwa ajili ya kupeleka kwenye korona tayari kuchakatwa na kuwa singa.”

Katika hatua nyingine, Mponzi alimhakikishia Waziri Mkuu kuwa wakulima hawatawaacha hivi hivi baada ya kuwakabidhi matrekta, bali watahakikisha wanawapa mafunzo ili waweze kuendesha kilimo kitaalamu huku wakitunza ipasavyo hesabu za mapato yanayopatikana.

Aidha, kwa kutambua sekta ya Kilimo ni endelevu na muhimu kwa Mkoa wa Tanga, NMB inashirikiana na wadau mbalimbali kuboresha huduma zake. Mpaka sasa Mkoa wa Tanga benki hiyo ina matawi 12, mawakala wa benki 152, kituo cha kukusanyia mapato kimoja (Horohoro) na mashine za kutolea pesa (ATMs) 18.

Aidha, wameendelea kutoa huduma za kifedha kwa wakulima wanaojishughulisha na uzalishaji wa mazao mbalimbali katika mnyororo wa thamani kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi nchi nzima.
Waziri Mkuu – Kassim Majaliwa akikabidhi mkopo uliotolewa kwa mkopo na Benki ya NMB wa matrekta  11 na matrela  yake 22 yenye thamani ya sh. Bilioni  moja, kwa Vyama Vinne vya ushirika vya wakulima wa mkonge Mkoani Tanga. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Vyama vya Mkonge mkoani Tanga – Greyson Nyari akionyesha ufunguo wa moja ya matrekta aliyokabidhiwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi ufunguo wa moja ya matrekta hayo  Greyson  Nyari, Mwenyekiti wa Vyama vya Mkonge  Mkoa wa Tanga kwenye shamba la mkonge la wakulima wadogo wadogo la  ‘Mwelya Sisal Estate’ la Korogwe. Katikati ni  Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara – Filbert Mponzi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad