Makamu wa Pili wa Raius wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein.
Baadhi ya Washiriki wa Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mkaazi wa Shirika hilo Nchini Tanzania Bibi Jacquiline Mahon akitoa salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu {UNFPA} kwenye Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu.
Baadhi ya Viongozi wa Serikali walioshiriki kwenye Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman akitoa salamu za Wizara ya Afya katika Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Watendaji wa Taasisi na Mashirika ya Kimataifa waliobahatika kushuhudia Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika Mtazamo wa Kiislamu.
Balozi Seif akimpongeza Mmoja wa Wahadhiri wa
Chuo Kikuu cha Al – Ahzar cha Nchini Misri kutokana na uamuzi wao wa
kusaidia kufanyika kwa Mjadala huo wa Uzazi wa Mpangilio katika
Mtazamo wa Kiislamu.
Kati kati yao anayeshuhudia ni Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harusi Said Suleiman.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al - Hajj Dr.
Ali Mohamed Shein alisema maradhi mengi yanayowakumba Watoto yakikosa
kushughulikiwa kwa Tiba sahihi katika hatua za awali huendelea kubakia
kuwa matatizo ya kudumu katika maisha yao ya baadae.
Alitanabahisha kwamba Mtoto asiye na afya njema kamwe hawezi kukua
vizuri jambo ambalo huathiri ustawi wa maisha yake na baadhi ya wakati
hushindwa kufanya vizuri katika masomo na kukosa ushirikiano mwema na
wanafunzi wenzake.
Dr. Ali Mohamed Shein alitoa kauli hiyo katika Hotuba iliyosomwa kwa
niaba yake na Makamu wa Pili wa Raius wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
wakati akizindua Mjadala wa Kitaifa kuhusu Uzazi wa Mpangilio katika
Mtazamo wa Kiislamu hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil
Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 90% ya Watoto walio
na umri wa chini ya Mwaka Mmoja hunyonyeshwa, lakini ni Watoto 37 kati
ya Watoto 100 walio na umri kati ya Mwaka Mmoja hadi Miwili ndio
wanaonyonyeshwa kabla ya Mama zao kubeba ujauzito mwengine.
Dr. Shein alisema hali hiyo inaonyesha wazi kwamba Jamii inahitaji
kuimarisha Utamaduni muhimu kwa Wanawake wananyonyesha kwa kipindi
kinachokubalika kama wanavyoifanya kina Mama walio wengi hivi sasa ili
kuimarisha Afya za Watoto.
Alisema asilimia 30% ya vifo vinavyotokana na Uzazi vinaweza kupungua
kama Jamii itakuwa na matumizi mazuri ya huduma za Uzazi wa
Mpangilio, na hii inajionyesha wazi elimu ya mpango huu kuanza
kuwafikia Wananchi kutokana na Takwimu zinazothibitisha Wanawake 28
kati ya 100 hutaka kutumia huduma hizo.
Rais wa Zanzibar alieleza kwamba njia hizo hawazipati kutokana na
sababu tofauti ikiwemo ukosefu wa Taarifa sahihi za Afya ya Uzazi
dhana zisizokuwa sahihi kuhusu njia ya Uzazi wa Mpangilio pamoja na
ufahamu mdogo wa Elimu ya Dini juu ya suala la zima la uzazi wa
mpangilio katika Uislamu.
Alifahamisha kwamba wapo baadhi ya Watu wanaopotosha maana halisi ya
Uzazi wa mpangilio kwa kuvihusisha vitendo vya utoaji wa mimba bila ya
sababu zilizoruhusiwa za afya.
Alisema hali hii imewafanya baadhi ya watu hasa akina Mama wakose hamu
ya kutafuta na kupata taaluma sahihi juu ya suala hilo ambalo hata
dhamira ya Serikali Kuu haihusiani na njia yoyote ya utoaji mimba kwa
njia ye yote ile.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitahadharisha
na kuonya kwamba ni kosa la jinai kufuatana na Sheria ya Makosa ya
Jinai ya Mwaka 2017. Hivyo Serikali inapinga vikali utoaji Mimba na
vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya Watoto wa rika zote.
Akigusia suala la unyonyeshwaji kwa Watoto, Dr. Ali Mohamed Shein
alisema tafiti nyingi zimethibitisha kwamba Mama anaponyonyesha uwezo
wake wa kuchukuwa mimba unapungua kutokana na mabadiliko ya kemikali
zinazofanya kazi ya kusaidia mfumo wa kiwiliwili ufanye kazi vyema.
Alisema hayo ni masuala muhimu yanayopaswa Jamii hasa Kina Baba
kuyafahamu iwapo kutafanyika Mijadala itayotoa elimu itakayohusiana na
masuala mazima ya mfumo wa uzazi wa mpangilio unaokubalika Kisayansi
sambamba na Kidini.
Dr. Ali Mohamed Shein aliwaeleza washiriki wa Mjadala huo wa Kitaifa
wa Uzazi wa Mpangilio katika Uislamu kwamba Serikali inatambua
mafanikio makubwa katika uimarishaji wa Afya za Wananchi yanategemea
usimamizi mzuri wa Mipango ya Taifa.
Alisema juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuimarisha Afya ya akina Mama na Watoto zimelenga katika
kupunguza idadi ya Vifo vya Mama na Watoto vinayotokana na masuala
yote ya uzazi.
Hata Hivyo Dr. Shein alifahamisha kwamba Sera, Maendeleo na Sheria
zilizopo za Nchi zimetoa uhuru kwa Wananchi kufanya maamuzi yao
wenyewe kuhusu namna bora ya kupanga Uzazi kwa kutegemea Imani za
Kidini, Utamaduni na Mipango ya Maendeleo ya Familia.
Alisisitiza kwamba suala la Uzazi wa Mpangilo bado linaendelea kuwa
ni suala la hiari kwa Wanafamilia kadri watakavyo, wanandoa kufuatana
na Imani za Dini na Mitazamo yao.
Dr. Shein alitanabahisha kwamba bado wapo baadhi ya Wananchi wenye
hitilafu ya mawazo inayowapa taabu ya kutofautisha kati ya Uzazi na
Mpango na uhuru wa kuzaa hasa pale Serikali inapoweka Mikakati ya
kutekeleza Uzazi huo ambapo Watu hao hufikiria kuzuiwa kuzaa.
“ Serikali ni Watu, walioichagua kwa ajili yao , kwa maslahi yao na
kwa madhumuni yao. Serikali si ya Mtu Mmoja, bali ya Watu wote. Hivyo
suala la uzazi ni la lazima kwa Maendeleo yetu” Alisisitiza Rais wa
Zanzibar.
Alisema Taifa linahitaji kuwa na kiazi kipya kitakacho chukuwa
urithi wa kile chilichopo hivi sasa kwa lengo la kuimarisha nguvu kazi
kadri ya Uchumi wake unavyoendelea kukua.
“ Tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba tunazaa , ili pawe na warithi wa
Taifa letu. Imani hii haipingani hata chembe na mafundisho na miongozo
ya Dini”. Alifafanua Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alieleza kwamba
Serikali Kuu imeweka utaratibu mzuri wa kuzitambua na kuzikubali ndoa
zote zilizofungwa kwa misingi ya Kiislamu na kwa taratibu za Dini
Nyengine zinazojuilikana na kutambuliwa katika Sheria za Nchi.
Alisema kinachofanyika kwa Serikali ni kufanya jitihada kubwa katika
kutoa Elimu ya Uzazi wa Mpangilio unaozingatia mafundisho ya Dini zote
zilizopo pamoja na maadili na Utamaduni wa Watu wa Zanzibar.
Mapema kitoa Taarifa ya Mjadala huo wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpangilio
katika Uislamu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bibi Asha Ali
Abdullah alisema asilimia 14% ya Wananchi wote Visiwani Zanzibar
ndio wanaotumia Uzazi wa Mpangilio hali inayotoa mwana kwa Akina Mama
wengi kuendelea na uzazi wa papo kwa papo unaoleta athari kwa afya za
Mama na Mtoto.
Bibi Asha alisema changamoto hiyo inatokana na mtazamo wa Jamii
katika kuihusisha Dini na masuala ya Uzazi wa Mpangilio.
Alisema juhudi za kushirikisha Viongozi wa Kidini zimesaidia kwa kiasi
kikubwa kampeni ya kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi
vinavyosababisha maambukizo ya Ukimwi Nchini.
Bibi Asha Ali Abdullah alisema ni vyema Kampeni hiyo iliyohusisha
Viongozi wa Kidini kwa sasa ikaelekezwa katika kampeni ya kupunguza
vifo vya Akina Mama kwa kuzingatia zaidi Uzazi wa Mpangilio.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya Zanzibar alilipongeza na
kulishuruku Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu
{UNFPA},Taasisi ya Chuo Kikuu cha Aga Khan pamoja na Chuo Kikuu cha
Kiislamu cha Al - Azhar cha Nchini Misri kwa moyo wao wa kusaidia
Taaluma juu ya uzazi wa Mpangilio.
Akitoa salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu {UNFPA},
Mwakilishi Mkaazi wa Shirika hilo Nchini Tanzania Bibi Jacquiline
Mahon alisema mchango mkubwa uliotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kupitia Ofisi ya Mufti Mkuu na Wizara ya Afya Zanzibar
umesaidia kufanikisha Mjadala wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpangilio katika
Uislamu.
Bibi Jacquiline alisema kitendo cha kufanywa mjadala huo kitatoa fursa
kwa Wananchi walio wengi kupata Taaluma ya uelewa juu ya uhumimu wa
kuimarisha Uzazi wa Mpangilio hasa ikizingatiwa kwamba hadi sasa
Zanzibar ina asilimia 14% ya Watu wanaotumia Uzazi huo.
Alisema asilimia hiyo ndogo ikiachiwa kuendelea upo uwezekano wa kutoa
mwanya wa kukaribisha vifo vya papo kwa papo vya Akina Mama na Watoto
vitavyoendelea kutokea kutokana na kutokuwa na mipango madhubuti ya
kuwapa haki yao Akina Mama na Watoto ya kubeba Mimba na Kunyonyeshwa
kwa mpangilio unaokubalika Kiafya.
“ Kwa tafiti zilizowazi ni thuluthi Moja tu ya Akina Mama Visiwani
Zanzibar wanaozingatia umuhimu wa Uzazi wa Mpangilio kwa kuchelewesha
Mimba moja hadi kutunga Mimba nyengine”. Alisisitiza Bibi Jacquiline.
Mwakilishi Mkaazi huyo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu
{UNFPA}, Nchini Tanzania Bibi Jacquiline Mahon aliupongeza Uongozi wa
Vyuo Vikuu vya Aga Khan na Al – Azhar ya Misri kwa ushirikiano wao na
Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Idadi ya Watu.
Alisema Ushirikiano huo umesaidia kuchapisha vitabu mbali mbali
vinavyosaidia kutoa elimu inayohusiana na Uzazi wa Mpangilio ambayo
hutoa muelekeo wa kuzingatia maisha bora yanayofaa kuendelezwa na wana
Familia .
Bibi Jacquiline aliithibitishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kwamba Shirika hilo litaendelea kushirikiana nayo katika Mipango na
Miradi yake ya Maendeleo hasa Dira ya 2020 pamoja na mapambano ya
vita dhidi ya kupunguza vifo vya Akina Mama na Watoto.
No comments:
Post a Comment