HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 6, 2019

WATU 10,000 WAPATIWA MAFUNZO YA KUPINGA UKEKETAJI WILAYANI IKUNGI MKOANI SINGIDA

Na Dotto Mwaibale,Singida
WANANCHI wapatao 10,258 katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wamepatiwa elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia  na ukeketaji kwa wanawake na watoto.

Hayo yalielezwa juzi na Mratibu wa mradi wa kupambana na mila potofu za ukeketaji wilayani humo , Evaline Lyimo katika mkutano wa hadhara wa uhamasishaji wa utetezi dhidi ya mila potofu kama ukeketaji wanawake na wasichana na udhalilishaji wa kijinsia uliofanyika Kata ya Iseke.

"Tumefanikiwa kutoa elimu ya kutokomeza ukatili huo katika Kata tatu za Ihanja, Ikungi na Iseke ambapo jumla ya watu 10,258 wanaume wakiwa 1200, wanawake 2400 na wale wasio wa moja kwa moja wakiwa ni 6,658 tuliwafikia kwa kufadhiliwa shilingi milioni 40 na Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) " alisema Lyimo.

Akizungumza katika mkutano huo ulioenda sanjari na kampeni  ya kuimarisha klabu za watoto wa shule za msingi na sekondari za kupinga ukatili huo , Mwezeshaji wa mradi huo
Japhet Kalegeya alisema mikutano na kampeni hizo zinasaidia kutoa elimu ya kutokomeza kabisa vitendo hivyo ambavyo vipo kinyume na haki za binadamu.

Mzee Emanuel Lie (89) alisema baadhi ya mambo yanayochangia udhalilishaji na mimba kwa wanafunzi ni wazazi na walezi kushindwa kusimamia malezi ya watoto wao.

Mkazi mwingine wa kata hiyo, Edward Migamba (68) alisema umbali mrefu kutoka kijijini na zilipo shule unachangia watoto kupata mimba ambapo mama Eliwanje Ibrahim aliongeza kuwa utandawazi nao ni sababu nyingine ya janga hilo.

Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Unyangwe, Prisca Elifaraja akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema kutembea umbali mrefu porini wakati wa kwenda shuleni, kukosa chakula na wazazi wanapotoa adhabu ya kuwafukuza watoto nyumbani pale wanapokuwa wamefanya makosa huchangia watoto kujikuta wakiangukia katika vishawishi na kupata mimba na kubakwa.

Mkutano na kampeni za kuimarisha klabu hizo za watoto mashuleni  uliandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Save the Mother and the Children of Central Tanzania (SMCCT) na kuhudhuria na wanafunzi kutoka Shule za Ihanja, Unyangwe na Nkhoiree ulihitishwa na sinema ya kutoa mafunzo ya kuepuka vitendo vinavyoweza kuwashawishi wanafunzi kupata mimba.
Mratibu wa mradi wa kupambana na mila potofu za ukeketaji, Evaline Lyimo akizungumza na wanafunzi wakati wa kuimarisha klabu za watoto mashuleni za kupinga ukatili wa kijinsia na ukeketaji.
Wananchi wa Kata ya Iseke, wanafunzi kutoka Shule za Ihanja, Unyangwe na Nkhoiree pamoja na maofisa wanaosimamia mradi wa kupambana na mila potofu za ukeketaji na ukatili wa Kijinsia wakionesha mshikamano wa kutokomeza kabisa vitendo hivyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Iseke wilayani Ikungi mkoani Singida juzi.
Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Muhintiri, Anatory Mzuma akizungumza na wanafunzi hao.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Unyangwe wakitoa burudani ya ngoma ya asili ya kabila la Wanyaturu.
Picha ya pamoja baada ya kuimarisha klabu za wanafunzi.
Mratibu wa mradi huo Evaline Lyimo akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Iseke.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa mama na mtoto wa Kata ya Iseke wakitambulishwa kwenye mkutano huo.
Mwezeshaji wa mradi huo, Japhet Kalegeya akihutubia kwenye mkutano wa hadhara.
Wakina mama wakiwa kwenye mkutano huo.
Mzee Emmanuel Lie (89) akizungumza kwenye mkutano huo.
Mzee Edward Migamba (68) akizungumza.
Mama Eliwanje Ibrahim akizungumza.
Mama Maria Jason akichangia jambo katika mkutano huo.
Mwanafunzi Prisca Elifaraja akielezea changamoto zinazochangia wanafunzi kupata mimba.
Wananchi wakiangalia sinema ya mafundisho namna ya kujikinga na vishawishi kwa wanafunzi kupata mimba.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad