HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 30, 2019

WAZIRI WA MAMBO YA NJE PROF JOHN KABUDI AFANYA MAZUNGUMZO NA MEYA WA NAGAI NCHINI JAPAN

Prof. Kabudi akimwonesha Mhe. Uchiya jarida linaloonesha vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini 
 Prof. Kabudi akiagana na Mhe. Shigeharu Uchiya mara baada ya kumaliza mazungumzo kati yao 
 Prof. Kabudi akisalimiana na mmoja wa raia wa Japan aliyewahi kufanya kazi za kujitolea kwenye sekta ya afya nchini Tanzania miaka ya 1960.





Prof. Kabudi afanya mazungumzo na Meya wa Jiji la Nagai nchini Japan 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuishirikisha Tanzania kikamilifu kwenye maandalizi ya Michezo ya Olympic inayotarajiwa kufanyika jijini Tokyo mwaka 2020 ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wanamichezo wanawake kutoka Tanzania.

Mhe.Prof. Kabudi ametoa shukrani hizo wakati wa mkutano wake na Meya wa Jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya uliofanyika leo tarehe 29 Agosti 2019 jijini Yokohama pembezoni mwa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Ushirikiano na Afrika (TICAD 7).

Mhe. Prof. Kabudi alisema kuwa, anaishukuru Japan kwa kuwa imeonesha nia ya dhati ya kuifanya Tanzania ishiriki kwenye Michezo hiyo muhimu ya Olympic ambayo itafanyika nchini humo mwaka 2020 na kuzishirikisha nchi zote duniani. Mhe. Waziri alifafanua kuwa tayari Serikali hiyo imesaini Hati ya Makubaliano na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mwezi Julai 2019 kuhusu ushiriki wa Tanzania kwenye michezo hiyo pamoja na kufanikisha ziara ya Timu ya wanariadha kutoka nchini wakiongozwa na mkimbiaji wa mbio za marathon mstaafu, Bw. Juma Ikangaa iliyofanyika mwezi Oktoba 2018. Pia Japan imeahidi kutoa mafunzo kwa wanamichezo wanawake yatakayotolewa jijini Nagai. 

“Ushikiano wa kirafiki kati ya Japan na Tanzania ni wa miaka mingi hususan kwenye medani za siasa, uchumi na diplomasia. Umefika wakati sasa nchi hizi mbili zishirikiane katika masuala ya kijamii na utamaduni ili kuwaunganisha mtu mmoja mmoja na kwamba ushirikiano huo ndio muhimu kwa ukuaji wa Taifa lolote” alisema Prof. Kabudi.

Aidha, alieleza kufurahishwa na ahadi kuwa Japan itatoa mafunzo kwa wanamichezo wanawake ili kuwajengea uwezo kwenye michezo mbalimbali ikiwemo ile ya Olympic itakayofanyika Tokyo mwaka 2020. “Tumepokea kwa furaha taarifa kwamba Nagai itatoa mafunzo kwa wanamichezo wetu wanawake. Hii itawajengea uwezo mkubwa wanamichezo hao wakati wakijiandaa na mashindano ya Olympic” alisisitiza Prof. Kabudi.

Kadhalika, Mhe. Prof. Kabudi alitumia fursa hiyo kumweleza Mhe. Uchiya kuwa Serikali ya Tanzania imehamishia shughuli zake jijini Dodoma ambako ni Makao Makuu ya nchi na kwamba ipo tayari kuanzisha ushirikiano wa kidada kati ya Jiji la Dodoma na Jiji la Nagai.

Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Nagai, Mhe. Shigeharu Uchiya alisema kwamba jiji hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania na tayari limeanzisha program ya kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya michezo ambapo Mtanzania, Bw. Bahati Rogers ni miongoni mwa vijana wanaoshiriki program hiyo jijini humo. Pia alisema kuwa aliongoza ujumbe wa watu ishirini kutembelea Tanzania mwaka 2017 kwa ajili ya kubadilisha uzoefu kuhusu michezo.

Serikali ya Japan ambayo imeanza maandalizi ya Michezo ya Kimataifa ya Olympic itakayofanyika jijini Tokyo mwaka 2020, imetenga Jiji la Nagai kuwa kituo cha Wanamichezo wote wa Tanzania kitakachotumika kuwaadaa kabla ya kuanza kushiriki michezo hiyo rasmi. Maandalizi hayo ni pamoja na kuwawezesha wanamichezo kuzoea hali ya hewa, tamaduni, chakula na masuala mengine muhimu kuhusu Japan kabla ya ushiriki wao rasmi wa michezo hiyo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasil
iano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Yokohama, Japan
29 Agosti 2019

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad