Eneo la kuzikia Watu liliyopo katika Kijiji cha Kama Wilaya ya Magharibi “A”. ambalo litachukuwa nafasi mbadala ya lile lililozoeleka la Mwanakwerekwe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed Kati kati pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi yake Nd. Abdulla Hassan Mitawi kulia yake na Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatib wakilikagua eneo hilo.
Waziri Aboud akiuagiza Uongozi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar kumalizia kulisafisha eneo hilo la makaburi liliopo Kama.
Baadhi ya Makaburi ya Watu waliokufa kutokana na Maafa ya kuzama kwa Meli za M.V Spice Islander na M.V Skagit yaliyopo katika Kijiji cha Kama Wilaya ya Magharibi “A”.
Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Kukabiliana na
Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatibu Makame akifafanua jambo wakati wa
ziara ya Waziri Aboud kulikagua eneo la Makaburi la Kama.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa
Mohamed Aboud Mohamed amefanya ziara ya kulikagua eneo mbadala la
kuzikia Watu liliyopo katika Kijiji cha Kama Wilaya ya Magharibi “A”.
Eneo hilo la Makaburi ya Watu waliofariki kutokana na Maafa ya kuzama
kwa Meli ya M.V. Spice Islander mnamo Tarehe 10 Septemba Mwaka 2011 na
M.V Skagit Mnamo Tarehe 18 Julai Mwaka 2012 limetengwa maalum kufuatia
lile lililozoeleka la Mwanakwerekwe kujaa Makaburi.
Mh. Mohamed Aboud Mohamed akiambatana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Abdullah Hassan Mitawi alisema
Uongozi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar unapaswa
kusimamia usafishaji wa eneo hilo pamoja na kukamilisha kazi
zilizobakia.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshatoa maelekezo
ya kutumiwa eneo hilo la kama kwa vile Mwanakwerekwe hivi sasa
kumekuwa na msongamano mkubwa wa Makaburi hali inayoweza kusababisha
baadae kuharibika kwa yale yaliyopo.
Waziri Aboud hata hivyo alifahamisha kwamba bado upo umuhimu wa
mahitaji ya kuongezwa kwa ukubwa zaidi wa eneo la kuzikia ili liweze
kukidhi mahitaji kwa kipindi kirefu kama ilivyokuwa Mwanakwerekwe.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar
Nd. Makame Khatibu Makame alisema eneo hilo tayari limeshatumika
kuzikiwa Watu 80 waliokufa kutokana na Maafa ya kuzama kwa Meli za M.V
Spice Islander na M.V Skagit.
Ndugu Makame alisema uzikwaji wa Watu hao ambao wapo waliotambuliwa na
jamaa zao na kutoa idhini pamoja na wale wasiotambulika umefanywa kwa
kuzingatia tofauti ya Imani za Dini zao.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar
alifahamisha kwamba katika kukamilisha vyema eneo hilo yapo mambo ya
muhimu yanayostahiki kujengwa kama Msikiti na sehemu ya kuoshea Maiti.
No comments:
Post a Comment