HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 11, 2019

MRADI WA MTO RUVU KUTIBU TATIZO LA MAJI SIMANJIRO

MBUNGE wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, amesema changamoto ya upungufu wa maji kwa jamii ya wafugaji wa Kata tatu za Orkesumet, Edonyongijape na Langai itapatiwa ufumbuzi Mei mwakani baada ya mradi mkubwa wa maji wa mto Ruvu kukamilika.

Millya aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Lormorjoi kwenye ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza kero, changamoto, malalamiko na kuongea na wananchi. 

Alisema mradi huo mkubwa wa maji kutoka mto Ruvu wilayani Same utagharimu kiasi cha sh41.5 bilioni pindi utakapokamilika mwakani.  Alisema tangu dunia iumbwe na Mungu, jamii ya wafugaji haijawahi kupata mradi mkubwa wa maji kama huo utakaokuwa mkombozi kwao.  Alisema anamshukuru Rais John Magufuli kwa kufanikisha mradi huo mkubwa kwani utakuwa msaada wenye kuhitajika mno kwenye jamii hiyo ya wafugaji. 

"Hivi sasa mkandarasi yupo kwenye eneo la mradi akiendelea kufanya kazi yake ili kufanikisha shughuli hiyo ambayo itakamilika mwaka ujao," alisema Ole Millya.  Hata hivyo, kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Celestine Silayo alisema mradi huo utawanufaisha pia wakazi wa pembezoni mwa kata ya Orkesumet kwani walishabainisha kwenye andiko lao. 

Silayo alisema baadhi ya vitongoji vya kata za Langai na Edonyongijape ambavyo havijawekwa kwenye mradi huo vitaingizwa ili navyo viweze kunufaika na mpango huo.  Mkazi wa kijiji cha Lormorjoi, Julius Saitoti alitoa ombi kwa mbunge huyo kuhakikisha mradi huo mkubwa wa maji unapita pia kwenye kijiji chao kwa faida ya jamii na mifugo yao. 

Saitoti alisema jamii ya eneo hilo ina uhitaji mkubwa wa mradi huo ambao kwa kiasi kikubwa utawanufaisha na wao hivyo wasisahaulike pindi ukikamilika. Mradi huo mkubwa wa maji wa mto Ruvu ukikamilika unatarajia kuwanufaisha zaidi ya watu 50,000 wa kata za Orkesumet, Langai na Edonyongijape, pamoja na mifugo yao. 
  Mbunge wa jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara James Ole Millya (kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Jackson Sipitieck (aliyevaa shati la kijani) wakati wakikagua majengo ya hospitali ya wilaya hiyo iliyotengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.5
Baadhi ya wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wakitoa maelezo ya miradi mbalimbali iliyofanyika kwenye kata ya Komolo kwa mbunge wa jimbo hilo James Ole Millya.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya akizungumza kwenye mkutano wake na wananchi wa eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad