HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 24, 2019

WANANCHI MBULU KUNUFAIKA NA BARAZA LA ARDHI NA NYUMBA

WANANCHI wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, waliokuwa wanafuata huduma ya Baraza la ardhi na nyumba Wilayani Babati, wataondoka na tatizo hilo baada ya viongozi wa wilaya hiyo kupanga mikakati ya kuanzisha katika eneo hilo.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Joseph Mandoo aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo.

Mandoo alisema wameshapata jengo litakalokuwa linatumika katika mashauri mbalimbali ya baraza hilo litakalokuwa kwenye kata ya Dongobesh.

Alisema baada ya jengo hilo kupatikana hivi sasa wanajipanga ili lianze kutumika na wananchi waliokuwa wanakwenda mbali hadi wilaya ya Babati kufuata huduma hiyo, sasa itakuwa karibu tofauti na mwanzo.

"Tutawachukua wazee wa baraza hilo kutoka kwenye kata mbalimbali za jirani ikiwemo Dongobesh, Tumati na nyinginezo kuliko kuwachukulia waliopo mbali na eneo ofisi ilipo," alisema Mandoo.

Hata hivyo, mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Massay alisema changamoto kubwa inayosababisha kutoanzishwa kwa baraza hilo ni watumishi hasa wapiga chapa. "Kama mkurugenzi angeweza kufanikisha tupate hata wapiga chama wa halmashauri mashauri yangeanza kusikilizwa ila muda siyo mrefu shughuli ya baraza hilo itaanza," alisema Massay.

Awali, diwani wa viti maalum wa Tarafa ya Dongobesh, Ester Joel (CCM) aliuliza swali juu ya jambo linalokwamisha uanzishaji wa shughuli za baraza la ardhi na nyumba kwenye halmashauri hiyo.

Joel alisema hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwateua wenyeviti wa wilaya wa mabaraza ya ardhi na nyumba wa wilaya hivyo ofisi ya Mbulu nayo ianze kazi.

Mkazi wa kijiji cha Dongobesh, John Matle aliipongeza serikali kwa kufanikisha uanzishwaji wa baraza hilo kwani wengi wanaofuata huduma hiyo mjini Babati wanalazimika kutumia gharama kubwa.

"Wengine walikuwa wanalazimika kulala Babati ili kusikiliza mashauri yao na gharama za kupeleka mashahidi nazo ni nyingi ila kuwepo hapa Dongobesh itapunguza muda na gharama," alisema Matle.
  Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Gregory Maasay akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
 Diwani wa viti maalum wa Tarafa ya Dongobesh Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, Ester Joel akisoma taarifa ya utekelezaji wa kamati ya fedha, uongozi na mipango, juu ya uanzishwaji wa baraza la ardhi na nyumba la wilaya hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Stanley Kamoga akizungumzia kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, kushoto ni Mwenyekiti wake, Joseph Guulo Mandoo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad