HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 24 April 2019

RC Wangabo asisitiza kasi katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo amemtaka Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kusimamia kwa karibu,  umakini na kuongeza kasi ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya sumbawanga baada ya kuona kusuasua kwa ujenzi huo tangu kuanza kwake tarehe 19 Januari, 2019 ambapo wananchi walijitokeza kuchimba misingi ya majengo saba ya hospitali hiyo.

Amesema kuwa muda mwingi umepita tangu kuanza kwa ujenzi huo na hadi sasa ilistahili uwe umefikia hatua ya lenta na matokeo yake bado ipo kwenye hatua ya jamvi pamoja na changamoto zilizokuwepo na kuongeza kuwa hali hiyo inawakatisha tamaa wananchi kwa kuona jengo halipandi tangu kuanza kushiriki kwao kwenye ujenzi huu na kutahadharisha kuwa kwa sasa hakuna sababu ya kusuasua katika ujenzi huo.

“Kuna haja kwa halmashauri kusimamia ujenzi huu kwa karibu kuanzia sasa hivi kasi iongezeke mara mbili hata tatu kwa ile iliyokuwepo kwasababu kuapanga matofali kwenda juu hata siku mbili ytatu unafika kwenye lenta lakini kutoka kule kwenye msingi kunahitaji uangalifu na kupanga vizuri zaidi, kwahiyo Mkurugenzi narudia tena simamia vizuri ujenzi wa hapa na kwa ukaribu zaidi,” Alisisitiza.

Ameyasema hayo alipotembelea eneo la ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga inayojengwa katika Kijiji cha Mtowisa, Kata ya Mtowisa, bonde la ziwa Rukwa na kuwataka mafunzi wote waliokabidhiwa kujenga majengo saba ya hospitali hiyo kuhakikisha wanafikia ngazi ya lenta ifikapo tarehe 10 Mei, 2019 na kuongeza kuwa asiyefikia hatua hiyo atawajibishwa.

Wakati akisoma taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Fani Musa aliwashukuru wananchi kwa kujitolea kwao kwa kazi za songambele zilizookoa shilingi 18,600,200 ikijumuisha kazi za kuchimba misingi ya majengo na mtaro wa kupeleka maji eneo la ujenzi, kusogeza tofali na ujazaji wa kifusi kwenye majengo hayo.

“Kwa ujumla kazi inaenda vizuri kwa mujibu wa ratiba ya kazi na tunatarajia kuikamilisha kwa wakati kama ilivyoelekezwa. Halmashauri inahitaji ushirikiano wa viongozi wote uendelee kama sasa ili kufikia mafanikio na kukamilisha ujenzi huu wa hospitali kwa muda uliopangwa,”Alisema

Ili kukamilisha ujenzi wa majengo saba ya hospitali hiyo ambayo ni majengo ya Utawala, Kufulia, Dawa, OPD, Maabara, Mionzi na Wazazi ni matofali 84,000 yanahitaji ambapo hadi sasa matofali 70,666 yameshafyatuliwa huku shilingi milioni 496 zikiwa zimeshatumika.
 Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo (kulia) akihoji maswali juu ya namna matofali hayo yatakavyopangiliwa ikiwa kuna yanayotakiwa kulala na mengine kusimamishwa kwenye ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga unaoendelea katika bonde la ziwa Rukwa. Wa tatu toka kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Khalfan Haule. 
 Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo akijaribu ubora wa matofali yanayotumika katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga katika bonde la ziwa Rukwa. 
  Sehemu ya Jengo la Mionzi likiwa limeanza hatua ya kupandisha ukuta ili kufikia usawa wa lenta ifikapo tarehe 10 Mei, 2019. 
 Sehemu ya jengo la Utawala inayoendelea na ujenzi katika hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga inayojengwa katika bonde la ziwa Rukwa.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad