HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 25 April 2019

ABDALLAH GAMA MWENYE HISTORIA NDEFU KATIKA MUZIKI

Na Moshy Kiyungi
Nina uhakika wale mashabiki wa bendi DDC Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ Ngoma ya Ukae’ wakati huo ambao walikuwa vijana wa zamani, watakuwa wanakumbuka mbali kila pale linapotajwa jina la mwanamuziki Abdallah Gama.

Gama ni mkung’utaji mahiri wa gitaa la kati, Rhythm, aliyepata kusumbua akili za wapigaji magitaa wengine wengi enzi zile, hususani alipokuwa katika bendi hiyo ya Sikinde.

Nguli huyo ni mmoja miongoni mwa wanamuziki 12 ambao mwaka 1978 walijiengua kwenye kundi la Dar International kwa madai ya kupinga uongozi mbovu wa mmiliki wao, Zachariah Ndabameiye na kuanzisha bendi ya Mlimani Park Orchestra.

Waliondoka kwa madai ya kupinga uongozi uliokuwa mbovu wa mmiliki wao, ambapo imeelzwa kuwa baada ya kujiengua walikwenda kuungana na wanamuziki wengine akina Abel Bartazal, George Kessy, Haruna Lwali na Ibrahim Mwinchande na kuwa waanzilishi wa bendi ya Mlimani Park Orchestra.

Baadhi ya wanamuziki wengine waliochomoka Dar International na kwenda kuanzisha bendi hiyo walikuwa ni Michael Enock, aliyekuwa mtaalamu wa kupiga ala zote za muziki, Cosmas Chidumule, Abel Bartazal, Joseph Mulenga’King Spoiler’, George Kessy na Machaku Salum. Wengine ni Haruna Lwali, Ibrahim, Mwinchande, Joseph Benard na Habib Jeff.

Wakati akiwa kwenye bendi ya Dar International aliyoitumikia kuanzia mwaka 1977, Gama alishiriki kupiga Rhythm kwenye vibao vingi, baadhi yake vikiwa ni ‘Sikitiko’, ‘Mwana Rudi Uoe’ na ‘Mwalimu Nyerere’.

Alipoingia katika bendi hiyo ya Mlimani Park Orchestra, Gama kwa kipindi kifupi aliweza kujipatia umaarufu mkubwa, hasa kwa umahiri aliokuwa nao katika kulicharaza ipasavyo gitaa la Rhythm kwenye vibao vingi vya bendi hiyo.

Abdallah gama ni mwanamuziki aliyefaulu kwa kiasi kikubwa kuzigusa nyoyo za mashabiki wengi kutokana na tungo zake zenye maudhui maridhawa yaliyoshiba ujumbe mzito, za ‘Hadija’, ‘Dar es Salaam Airport’, ‘Maudhi ya Nyumbani’, ‘Linda’ na ‘Nawashukuru Wazazi’.

Akielezea wasifu wake Gama alianika mambo mengi hususani historia yake kimuziki na maisha kwa ujumla.

“Baba yangu alikuwa fundi Cherahani, ndiye aliyenivuta kwenye muziki kwani alikuwa akipiga gitaa lisilotumia umeme la Galatoni, kujifurahisha na wakati mwingine akiwaburudisha rafiki zake…” anasema Gama.

Alisema kuwa, akiwa na umri wa miaka 28, alikuwa tayari anafahamu kikamilifu jinsi ya kulikung’uta gitaa. Bendi yake ya kwanza kupigia ilikuwa ni Safari Trippers aliyojiunga nayo mwaka 1973.

“ Nikiwa Safari Trippers nilishiriki kupiga gitaa la solo kwenye vibao kadhaa, vikiwamo ‘Ooh Lila’ na ‘Mateso’ ambavyo vyote ni matunda ya marehemu Marijani Rajabu...” alibainsha Abdallah Gama.

Ni mwanamuziki asiyependezwa na tabia ya wanamuziki kuhamahama makundi, alisema kwamba mwaka 1975 alijiunga na bendi ya Tanzania Stars ambayo maskani yake yalikuwa katika hoteli ya Margot.

Hoteli hiyo ilikuwa katika mtaa wa Independence (siku hizi ni mtaa wa Samora) jijini Dar es Salaam. Ikumbukwe kuwa, mwaka 1984 Gama alijiunga katika bendi ya Bima Lee iliyokuwa ikimilikiwa na Shirika la Bima la Taifa (NIC)

“Nikiwa na bendi ya Bima Lee, iliyokuwa ikipiga muziki kwa mtindo wa “Magnet tingisha” nilitunga kibao cha ‘Fungua Macho’, pamoja na kushiriki kucharaza gitaa kwenye vibao kama vile; ‘Makulata’ na ‘Tujemaso…” anafafanua Gama.

Abdallah Gama atakumbukwa kwa kazi zake alipokuwa bendi ya Bima Lee Orchestra akishirikiana vyema na watunzi na waimbaji akina Jerry Nashon, Shaaban Dede, wapiga magitaa Joseph Mulenga ‘Kig Spoiler’ kwa upande wa solo na Suleiman Mwanyiro kwa upande wa gitaa zito la besi.

Wanamuziki hao walichukuliwa kwa mpigo na Shirika hilo la Bima kwa ajili ya kuimarisha bendi ya Bima Lee Orchestra kufuatia ushindani mkubwa wa bendi zilikuzokuwepo wakati huo. Abdallah Gama wakati huo alikuwa mithiri ya Kito cha thamani kwani aliitumikia bendi Bima Lee Orchestra kwa mwaka mmoja.

Mwishoni mwa mwaka 1985, alihitajika kurejea tena katika bendi yake ya zamani ya ‘Wana Sikinde’. Wimbo wa ‘Gama Unisamehe’ kilichoporoshwa na bendi yake wakati huo ya Mlimani Park Orchestra, baadhi ya wapenzi na mashabiki hudhani kwamba mtunzi wa wimbo huo kuwa alikuwa yeye. Lakini Gama pasipo kujigamba ametamka kwamba pasipo kumung’unya maneno akisema:

“Kibao kile kilitungwa na Tshimanga Kalala Asossa, tukiwa Zanzibar kwenye shoo, mimi nilikuwa Kiongozi wa Jukwaa, sasa kabla hatujaanza kutumbuiza nilipanda jukwaani na kuwaita wanamuziki kwa kutumia mlio wa gitaa langu...”

Nguli huyo aliendelea kueleza kuwa, ghafla alimuona Asossa aliyekuwa anapenda kutembea na redio ndogo ya kurekodia sauti, akarekodi kipande alichokuwa anakipiga kisha akaondoka.

Waliporejea Dar es Salaam wakiwa kwenye mazoezi, Tshimanga Kalala Asossa alikuja na mashairi ya wimbo huo, akiambatanisha kile kipande alichokipiga Gama kule Zanzibar.

Wakaufanyia kazi wimbo huo na kuamua kuupa kumbukumbu kwa kuuita ‘Gama Unisamehe’. Tshimanga Asossa alijiunga na bendi hiyo ya Mlimani Park Orchestra mwaka 1981, baada ya uongozi wa Mlimani Park kumfuata kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kuja kupiga muziki na bendi hiyo kwa mkataba.

“Maisha ni kutafuta…” usemi huo ulijionesha wazi kwa mwanamuziki Abdallah Gama, ambaye mwishoni mwa mwaka 1985, alivuka mpaka wa Tanzania na kiungia nchini Kenya kwa kupitia bandari ya Tanga.

Alipotua katika jiji la Nairobi, alijiunga na bendi ya Super Mazembe iliyokuwa ikitumbuiza kwenye ukumbi wa Garden Square, jijini Nairobi. Alishirikiana kikamilifu na wapiga magitaa wa bendi hiyo ya Super Mazembe akina Loboko Bua Mangala, Bukasa wa bukasa ‘Bukalos’, Atia Joe ‘Mwanza wa Mwanza’ aliyekuwa akiliungurumisha gitaa la besi

Matarajio ya kila kazi ni kupata mafanikio mazuri yanayoweza kumnemesha muhisika pamoja na familia yake. Kwa upande wa mafanikio aliyoyapata mwanamuziki huyo Abdallah Gama anasema “…Mafanikio niliyokwishayapata kwenye muziki ni kutembea nchi nyingi duniani, jambo ambalo sikutarajia hapo kabla…” Gama kati ya ziara alizowahi kuzofanya nje ya nchi, anaikumbuka mno ziara yake alipokuwa katika bendi ya Malembe Stars.

Aidha anazikumbuka baadhi ya nchi alizowahi kufika kuwa ni pamoja na Japan, Malaysia, Ufilipino, Pakistan na Misri. Bila kusita Gama amesema kuwa yeye ni baba wa watoto wanne anawataja kuwa ni Mgeni, Pili, Hadija na Maimuna. Gama elimu kwa familia yake aliipa kipa umbele na sasa anajivunia kwa kuweza kusomesha watoto wake wote hadi elimu ya Chuo Kikuu.

Ili kutunza kumbukumbu za kazi zake alizokwisha kuzifanya awali, Gama ana mpango wa kurudia kuvirekodi upya vibao vyake vya zamani, alivyovitunga akiwa na bendi za Mlaimani Park Orchestra ‘Wana Sikinde’ na Bima Lee Orchestra, kutokana na shinikizo kubwa la mashabiki wake. Abdallah Gama hivi sasa yuko katika bendi ya Excel ya jijini Dar es Salaam, wakati akiwa katika mkakati wa kuanzisha bendi yake binafsi.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad