HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 27 February 2019

Onesheni uzalendo kwa kurejesha mikopo ya HESLB – RC Gambo

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amewataka wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kuonesha uzalendo kwa kujitokeza na kuanza kurejesha ili watanzania wengine wanufaike.

Mkuu huyo wa mkoa ameyasema hayo leo (Jumatano, Feb. 27, 2019) jijini Arusha katika hafla fupi ya kukabidhi tuzo za utambuzi kwa waajiri 12 kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambao wanatekeleza vizuri sheria ya Bodi ya Mikopo.

Taasisi hizo kutoka mkoani Arusha ni World Vision Tanzania, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Kampuni ya Off-Grid Electric, Vision Fund Tanzania, Shule ya Mtakatifu Jude na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Arusha ambazo kwa jumla zina wanufaika 410 wanaorejesha Tshs 74.08 milioni kwa mwezi.

Kwa mkoa wa Kilimanjaro, taasisi zilizopokea tuzo ni Mamlaka ya Uendelezaji wa Uwanja cha Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO), Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge, Tanganyika Planting Company, Kampuni ya Vinywaji ya Bonite, Kampuni ya Marenga Investment na Benki ya Biashara ya Uchumi ambazo kwa ujumla zina wanufaika 142 wanaorejesha Tshs 23.8 milioni kwa mwezi.

“Lazima wajiulize, kama Bodi (ya mikopo) isingekuwepo, labda wasingeweza kusoma, na kama wasingesoma, wangekuwa wapi?” aliuliza Mkuu huyo wa mkoa ambaye alikuwa mgeni rasmi na kuongeza:

“Ili kuonesha uzalendo, wanapaswa kuwa ‘honest’ na kuwataarifu waajiri wao kuwa walinufaika na mikopo na kuanza kurejesha,” aliongeza katika hafla iliyohudhuriwa na mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mikopo Dkt. Richard Masika ambaye pia ni Mwenyeki wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na majitaka Arusha.

Gambo aliwakumbusha waajiri waliopokea tuzo kuwa Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya fedha za mikopo ili kusomesha watanzania wengi ambao baada ya kuhitimu masomo huajiriwa na taasisi mbalimbali.

“Tangu kuingia madarakani mwaka 2015, Serikali ya Awamu Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, imeongeza bajeti ya fedha za mikopo kutoka TZS 322.4 bilioni mwaka 2014/2015 hadi kufikia TZS 427.5 bilioni mwaka wa masomo 2018/2019,” alisema na kuongeza kuwa idadi ya wanufaika nayo imeongezeka kutoka 100,937 hadi 124,000 katika kipindi hicho.

Awali akiongea katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru alisema katika mwaka wa fedha 2017/2018, Bodi ya Mikopo ilikusanya Tshs 181.4 bilioni, na kati ya hizo, Tshs 17.4 bilioni zilikusanywa kutoka kwa taasisi binafsi na umma kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.  

Aidha, Badru alieleza kuwa sheria ya HESLB imetoa wajibu wa aina nne kwa waajiri.

“Kwanza wanapaswa kuwasilisha kwa HESLB orodha ya waajiriwa wapya ndani ya siku 28 baada ya kuwaajiri. Pili, kukata asilimia 15 kutoka kwenye mshahara ghafi wa mnufaika na kuwasilisha kwa HESLB makato hayo ndani ya wiki mbili baada ya mwisho wa mwezi,” alisema Badru.

Mkurugenzi Mtendaji huyo aliongeza kuwa waajiri pia wanapaswa pia kutoa taarifa pale mnufaika anapoanza kazi, kufukuzwa au kufariki ili kuiwezesha Bodi ya Mikopo kuhuisha taarifa zake.
Kwa mujibu wa Badru, wajibu mwingine wa kisheria ni kutoa ushirikiano kwa maafisa wa Bodi ya Mikopo wanapokuwa katika ziara za kikazi kwa waajiri ikiwemo kufanya kaguzi.

Bodi ya Mikopo ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wa kitanzania wenye sifa za kujiunga na taasisi za elimu ya juu lakini hawana uwezo wa kiuchumi kumudu gharama hizo. Jukumu jingine ni kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika waliopata mikopo kutoka serikalini tangu mwaka 1994/1995.
 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka ya Majisafi na Majitaka Arusha (AUWSA) Dkt. Richard Masika tuzo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kufuatia AUWASA kuwa mmoja wa waajiri wanaotekeleza vizuri Sheria ya HESLB. Hafla hiyo imefanyika jijini Arusha leo (Jumatano, Feb., 27, 2019). (Picha na HESLB) 
 Mwakilishi wa kiwanda cha vinywaji baridi cha Bonite cha mjini Moshi Frank Hamba akipokea tuzo ya utambuzi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gamba kufuatia kampuni hiyo kuwa moja ya taasisi zinazotekeleza vizuri sheria ya Bodi ya Mikopo. Hafla hiyo imefanyika jijini Arusha leo  (Jumatano, Feb., 27, 2019). (Picha na HESLB). 
 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akimkabidhi tuzo ya utambuzi Mwakilishi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) Moreen Mwaimale kufuatia mamlaka hiyo kuwa moja ya taasisi zinazotekeleza vizuri Sheria ya HESLB. Hafla hiyo imefanyika jijini Arusha leo (Jumatano, Feb., 27, 2019). (Picha na HESLB)


No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad