HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 27 February 2019

MGALU AWATAKA WAKANDARASI UMEME VIJIJINI KUWA NA MAGENGE KILA WILAYA

Na Veronica Simba – Ruangwa
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kuweka magenge yenye vifaa vya kazi katika kila wilaya nchi nzima ili kuboresha utendaji kazi wao. Alitoa maagizo hayo kwa nyakati tofauti jana, Februari 26, 2019 akiwa katika ziara ya kazi katika vijiji kadhaa vya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa kuwaunganishia umeme wananchi wengi wa vijijini, Naibu Waziri alisema ni lazima wakandarasi husika wahakikishe wanakuwa na genge lenye vitendea kazi katika kila wilaya ili kusiwepo na sababu au kisingizio cha kuchelewa kuunganisha umeme katika maeneo yao.

Akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Lindi, Mgalu aliviwashia umeme vijiji vya Chimbila B, Mtakuja na Nandanga vilivyoko wilayani Ruangwa, ambapo pia alisisitiza kuwa taasisi za umma zipewe kipaumbele katika kuunganishiwa umeme kwa manufaa ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri aliwataka wakandarasi kuwapa kipaumbele wenye ulemavu pamoja na wazee katika zoezi la kuunganishiwa umeme kwa kutumia vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) ambavyo serikali imetoa 250 bure kwa kila eneo.

Aidha, aliwaagiza wasimamizi wa miradi ya umeme vijijini kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa agizo hilo.

Vilevile, alihamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kulipia gharama za kuunganishiwa umeme ambazo ni shilingi 27,000 tu kupitia mradi wa umeme vijijini ili waweze kupatiwa nishati hiyo na waitumie kwa shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato hivyo kuboresha maisha yao.

Alisisitiza kuwa, serikali imepitisha azimio la kuwaunganishia umeme wananchi wote walioko vijijini kwa gharama ya shilingi 27,000 tu pasipo kujali aina ya mradi unaohusika.

“Mwananchi yeyote wa kijijini ataunganishiwa umeme kwa shilingi 27,000 tu. Uwe ni umeme wa REA au TANESCO au wowote ule, gharama ni hiyo. Mkitozwa gharama tofauti, toeni taarifa kwa mamlaka husika zichukue hatua mara moja.”

Pia, aliwaelekeza Wakuu wa Wilaya katika maeneo yote nchini kuwasimamia wakandarasi hao wa miradi ya umeme vijijini na kuchukua hatua stahiki pindi wanapoona hawatekelezi kazi zao kama wanavyotakiwa.

Naibu Waziri yuko katika ziara ya kazi ya siku nne mkoani Lindi ambayo anatarajia kuhitimisha Februari 27, mwaka huu.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mtakuja, Kata ya Nandanga wilayani Ruangwa, Mkoa wa Lindi, kabla ya kuwasha rasmi umeme katika eneo hilo, alipokuwa katika ziara ya kazi Februari 26, mwaka huu.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa umeme katika Zahanati ya Nandanga, wilayani Ruangwa, Mkoa wa Lindi, Februari 26, mwaka huu.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwasha rasmi  umeme katika Zahanati ya Nandanga, wilayani Ruangwa, Mkoa wa Lindi, Februari 26, mwaka huu.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akikabidhi Jenereta katika Kituo cha Afya Nkowe, Kata ya Nkowe, wilayani Ruangwa, Mkoa wa Lindi akiwa katika ziara ya kazi, Februari 26, mwaka huu.

 Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji vya Mtakuja na Nandanga, wilayani Ruangwa, Februari 26, mwaka huu.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mwenye kilemba) akizungumza na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya umeme Manispaa ya Lindi, Februari 26, 2019.
 Sehemu ya umati wa wananchi wa kijiji cha Chimbila B, Kata ya Mnacho, wilayani Ruangwa, Mkoa wa Lindi, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipofanya ziara eneo hilo na kuwasha rasmi umeme Februari 26, 2019.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mnacho, Kata ya Mnacho wilayani Ruangwa, Mkoa wa Lindi, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipofanya ziara eneo hilo na kuwasha rasmi umeme Februari 26, 2019.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad