HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 1 February 2019

Mkataba Kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na MOI Kuwanufaisha Wananchi

 Na Mwandishi wetu- MOI
Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesaini mkataba na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) utakaowezesha wagonjwa kutoka Visiwani humo kupata matibabu  ya kibingwa waliyokuwa wakiyapata nje ya nchi kwa gharama kubwa.
Utiaji saini wa mkataba huo umefanywa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo  Bi Asha Ali. Abdulla pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface leo mjini Zanzibar. 
"Tumekuwa tukipeleka wagonjwa wengi nje ya nchi kwa matibabu hususan hawa wa mifupa, sasa tunafahamu kwamba wenzetu  wa MOI wameboresha sana huduma zao hivyo tumeamua wagonjwa wetu waende MOI badala ya kwenda nje, naamnini Mashirikiano hayo haya yatakuwa yenye tija kwa wananchi wetu" alisema Bi Asha.
Asha ameongeza kwamba wagonjwa wamekuwa wakienda MOI kupata huduma kwa kipindi kirefu lakini mkataba huu unafanya ushirikiano uwe rasmi na wagonjwa wapokelewe na kupata huduma kwa namna bora zaidi.
"Hili siyo jambo jipya, wagonjwa wetu wanakuja huko kupata huduma na tunashukuru kwamba mmekuwa mkiwahudumia vyema, mkataba huu utaboresha namna mnavyowapokea na hata kama kutakuwa na changamoto yoyote kwa mgonjwa tutajadiliana na kuangalia nini cha kufanya kwani mambo sasa yamekuwa rasmi" Alisema Bi Asha
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema ni heshma kubwa kwa MOI kuingia mkataba na Wizara ya Afya ya Zanzibar ikiwa ni ishara tosha kwamba Serikali ya Zanzibar imetambua maboresho yaliyofanyika MOI pamoja na huduma za ubora wa hali ya juu zinazotolewa.
" Tunawashukuru sana kwa kuona kwamba huu ni muda muafaka wa kuingia makubaliano nasi, tunawashukuru sana kwa kutambua ubora wa huduma zetu, tunawaahidi kwamba wagonjwa watakaofika kwetu tutahakikisha wanapata huduma bora na kwa wakati kama ambavyo mnatarajia" alisema Dkt. Boniface
Dkt Boniface amesema kwamba huduma zinazopatikana MOI kwa sasa ni sawa na zile zinazotolewa katika mataifa yaliyoendelea hivyo wagonjwa kutoka Zanzibar watapata huduma nzuri tena kwa wakati.
" Ndugu Katibu Mkuu tumeboresha sana huduma zetu, tuna kitengo cha kisasa cha radiolojia, maabara na wodi za kisasa (Executive ) hivyo tunaamini wagonjwa kutoka Zanzibar na watanzania wataendelea kupata huduma bora katika Taasisi yetu" Alisema Dkt Boniface
Hatua hii itapelekea wagonjwa kutoka Visiwani Zanzibar kupata huduma za kibingwa katika Taasisi ya MOI na hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimekuwa kikitumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu. 
Tukio hilo limeshuhudiwa na Mwanasheria wa MOI bwana Suleiman J. Mgerwa pamoja na mwanansheria wa Wizara ya Afya Zanzibar Bi Shufaa Nassoro Ali, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kurasimisha ushirikiano na Taasisi ya MOI kwani imekuwa ikitumia gharama kubwa kupeleka wagonjwa nje ya nchi wakati huduma hizo zinapatikana hapa Tanzania.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar  Asha Ali Abdulla akikabidhiana mkataba wa Matibabu kwa wagonjwa kutoka Zanzibar na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Dkt. Respicious Bonifece katika Hafla iliyofanyika Zanzibar Januari 31, 2019.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Asha Ali Abdulla akitia saini mkataba wa wagonjwa kutoka Zanzibar kupata huduma za kibingwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI)
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Dkt. Respicious Boniface akitia saini mkataba wa wagonjwa kutoka Zanzibar kupata huduma za kibingwa za Taasisi hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar BAsha Ali Abdulla   akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani ) katika hafla ya utiaji saini Januari 31, 2019 Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Dkt. Respicious Boniface akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani ) katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika Zanzibar leo.
Mwanasheria wa Wizara ya Afya Zanziba Bi. Shufaa Nassoro Ali akitia sini Mkataba huo leo mjini Zanzibar. 
Mwanasheria wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Bw. Suleimani Mgerwa akitia saini Mkataba huo leo mjini Zanzibar.(Picha zote na MOI)


No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad