HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 1 February 2019

Mahenge resources yachangia majengo,miundombinu ya shule Ulanga

KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Kinywe (Mahenge Resources) imechangia sh. Milioni 16 ili kuboresha majengo na miundombinu ya shule zilizoko katika Wilaya ya Ulanga, Mkoani Morogoro. Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi fedha hizo, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya, aliipongeza na kuishukuru kampuni ya Mahenge Resources kwa ushirikiano wake endelevu katika shughuli za maendeleo wilayani humo.

“Naamini kwamba mshikamano uliojengeka kati ya serikali ya Wilaya yetu na Kampuni hii utachangia sana kuleta manufaa mengi zaidi huko mbeleni kwa maslahi ya pande zote mbili,” “Inatia moyo kuona wawekezaji wakubwa wa kiwango hiki wanaona umuhimu na haja ya kushiriki kwa vitendo maendeleo ya jamii inayowazunguka na ya taifa kwa ujumla,”alisema DC Ngollo.

Naye Makamu wa Rais wa Mahenge Resources, Hekima Raymond, alisema wanachofanya ni kuwekeza kwa ajili ya maendeleo ya Watoto na  taifa.
“Pia tufanya uwekezaji chanya kwa ajili ya watu wanaotuzunguka ni jambo ambalo tumelipa kipaumbele cha muda wote kwenye malengo wakati wote kwa muda mrefu, na hata katika utaratibu wetu wa kurudisha manufaa kwa jamii, almaarufu kama CSR,”alisema Raymond.

Aidha alisema kwamba kiasi cha fedha walichochangia ni takribani asilimia 18 ya fedha zote zilizopatikana katika harambee hiyo maalumu iliyoendeshwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Stephen Kebwe.

“Haya ni majitoleo makubwa toka kwa kampuni yetu, ikizingatiwa kwamba hata hatujaanza hatua ya ujenzi wa mgodi wenyewe wala uchimbaji wa kibiashara utakaoiingizia kampuni faida. Wakati tunashugulikia hatua za leseni na vibali vya uchimbaji, pamoja na kukamilisha uwezo wa kifedha kwa ajili ya uchimbaji, tutaendelea kutilia mkazo maendeleo ya jamii inayotunzunguka sambamba na ukamilishwaji wa hatua ya utekelezaji wa sera ya fidia,uhamishaji na urasimishaji makazi, ili kuendeleza manufaa chanya kwa jamii,”alisema.

Raymond pia alisema kwamba wataendelea kushirikiana na serikali katika ukamilishwaji wa leseni na vibali kwani utekelezaji wa mradi ni suala linalohitaji kukamilishwa kwa usawa kwa maslahi ya pande zote, ili kuendeleza tija.

Kampuni hiyo imeendelea kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa baadhi ya shule za vijijini ili kupunguza tatizo la utoro mashuleni ambalo mara kadhaa limeonekana kuwa tishio ikiwemo kudhamini wanafunzi 100 wa sekondari wanaotoka kaya masikini na kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama kwa shule zenye changamoto.

Mahenge Resources inamiliki kwa asilimia 100 mradi mkubwa wa madini ya kinywe ulioko Wilayani Ulanga ambapo mradi huo umevuka hatua ya upembuzi yakinifu, Oktoba mwaka jana, na kusajili maombi rasmi kwa ajili ya leseni za uchimbaji.
 Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngolo Malenya akipokea hundi ya Milioni 16 kutoka kwa Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mahenge Mineral Resources  Hakima Raymond  kwa ajili ya Maendeleo ya Wilaya hiyo katika hafla iliyofanyika wilayani Ulanga. 
 Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngolo Malenya akizungumza na wananchi wakati wa kupokea hundi ya milioni 16 kutoka kampuni ya Madini ya Mahenge Mineral Resources.
 .Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngolo Malenya akiwa na watendaji mara baada ya kupokea hundi ya milioni 16  kutoka kwa Makamu wa Rais wa  Kampuni ya Madini ya  Mahenge Mineral Resources Hekima Raymond kwa ajili kusaidia Maendeleo ya wilaya hiyo.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad