Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante
Ole Gabriel (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa kutoka
Benki ya NMB na menejimenti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante
Ole Gabriel akifafanua jambo wakati wa kikao na maafisa kutoka Benki ya
NMB na menejimenti wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (hawapo pichani) kuhusu
uwekezaji katika sekta ya maziwa

Meneja
Mwandamizi kutoka Benki ya NMB idara ya kilimo Bw. Carol Nyagaro
akimuelezea Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anyeshughulikia Mifugo
Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) juu ya uwekezaji wa sekta
ya maziwa na Benki ya NMB
………………………
Na. Edward Kondela
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante
Ole Gabriel ameitaka Benki ya NMB kushirikiana na wizara hiyo katika
kukuza sekta ya maziwa nchini kwa kuwa bado kuna mwitikio mdogo wa
wananchi kunywa maziwa kutokana na taarifa iliyotolewa na Shirika la
Chakula Duniani (WFP)
Prof.
Gabriel amebainisha hayo leo (31.01.2019) Jijini Dodoma, akiwa kwenye
kikao na maafisa kutoka idara ya kilimo ya Benki ya NMB, waliofika
ofisini kwake kumwelezea mikakati ya Benki ya NMB ambayo imekuwa
ikifanya tafiti na wadau wa sekta ya maziwa lengo likiwa ni kutaka
kuwekeza katika sekta hiyo.
“Kwa
takwimu ambazo zimetolewa na Shirika la Chakula Duniani ni kwamba kwa
wastani angalau mtu anatakiwa walau atumie lita mia mbili kwa mwaka za
maziwa lakini kwa bahati mbaya kwa watanzania wastani ni lita arobaini
na saba tu, bado tuna kazi kubwa sana.” Alisema Prof Gabriel
Prof.
Gabriel amesema Benki ya NMB inapaswa kuwa na ushirikiano na Wizara ya
Mifugo na Uvuvi kupitia Dawati la Sekta Binafsi ambalo limekuwa
likiwaunganisha wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi, ili kuhakikisha mazao
yatokanayo na ng’ombe yakiwemo maziwa yanatumika ipasavyo.
Katika
kikao hicho ambacho kimehudhuriwa pia na watendaji wakuu wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Katibu mkuu huyo pia amesema ni wakati muafaka kwa
Benki ya NMB kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika
kuhakikisha inawaletea maendeleo wafugaji, hususan wafugaji wadogo ambao
wamefanikiwa pamoja na wafugaji ambao watakuwa tayari kubadilika na
kuingia katika ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhamahama.
Aidha
Prof. Gabriel amesisitiza umuhimu wa kufanyika kwa tafiti kwa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Benki ya NMB kupitia idara ya
kilimo ili tafiti hizo ziweze kufanyiwa kazi na kuleta matokeo chanya
kwa wafugaji.
“Ningependa
sekta hii ya mifugo, iwe pia na tafiti nyingi zinafanyika, sasa
tukifanya hizo tafiti tutaweza kuleta mabadiliko chanya na yenye uhakika
katika maendeleo ya wafugaji kwa sababu lengo siyo tu kufanya jambo,
lakini liwe jambo ambalo linaweza kugusa maisha ya wafugaji.” Alisema
Prof. Gabriel
Katika
kikao hicho pia Katibu Mkuu Prof. Gabriel ameshauri uwepo wa mahusiano
ya karibu kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Benki ya NMB na taasisi za
elimu ya juu, ili kuhakikisha tafiti ambazo zimekuwa zikifanywa na
wanafunzi ziweze kutumika katika kuleta mabadiliko na kuleta manufaa kwa
wafugaji, badala ya tafiti hizo kuwekwa katika maktaba za vyuo hivyo
pekee.
Kwa
upande wake Meneja Mwandamizi wa Benki ya NMB kutoka idara ya kilimo
Bw. Carol Nyagaro amesema kutokana na kasi ya utendaji kazi wa serikali
ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Magufuli pamoja na utendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi
imewalazimu benki hiyo kubadili mtazamo wa namna ya kutafuta wateja
wapya kupitia sekta mbalimbali.
“Kutokana
na kasi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli na uongozi mzima wa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwetu inajenga mazingira mazuri ya kufanya
biashara, pia kuchangia maendeleo ya jamii na kuweza kutengeneza wateja
wa siku zijazo.” Alisema Bw. Ngayaro
Aidha
Bw. Nyagaro amesema Benki ya NMB kupitia idara ya kilimo inafikiria pia
kuwekeza katika sekta ya samaki ambayo imekuwa ikifanya vizuri kiuchumi
katika siku za hivi karibuni.
Bw.
Nyagaro amemueleza pia Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, kuwa Muunganiko wa
Vyama vya Ushirika Vikuu vya Maziwa Duniani unatarajia kufanya mkutano
wake hapa nchini Tarehe 25 na 26 Mwezi Februari mwaka 2019 kwa
kushirikiana na Benki ya NMB lengo kuu likiwa ni kuangalia uwezekano wa
kuwekeza katika sekta ya maziwa hapa nchini.
Amefafanua
kuwa muunganiko huo wenye nchi wanachama 95 ambao unafanya biashara ya
takriban Dola za Marekani Bilioni 200 kwa mwaka, umeichagua Tanzania kwa
ajili ya kufanya majadiliano kwa kuhusisha wadau wa sekta ya mifugo ili
kuwekeza katika sekta ya maziwa.
Amesema mkutano huo pia utaainisha mambo ambayo tayari yalishafanyiwa tafiti kwa ajili ya utekelezaji wa mipango hiyo.
No comments:
Post a Comment