HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, January 31, 2019

UKATILI DHIDI YA WATOTO HAUKUBALIKI, HAUVUMILIKI, TUWALINDE WATOTO- TGNP

TGNP Mtandao kwa kushirikiana na wadau wa haki za wanawake, watoto na usawa wa kijinsia tunatoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza watoto Mkoani Njombe kutokana na matukio ya mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina.

Vitendo hivi ni vitendo ambavyo havikubaliki katika jamii kwani ni kinyume cha Azimio la ulimwengu juu ya haki za binadamu (Universal Declaration of Human Rights) la tarehe 10 Desemba 1948. Kifungu cha 3 kinachotamka kwamba “Kila mtu ana haki ya kuishi, haki ya uhuru na haki ya kulinda nafsi yake. Na ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) Ibara ya 14 imetamka juu ya Haki ya kuishi sambamba na sheria ya Haki ya kuishi ya mwaka 1984.

Jamii inawajibu wa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Hii ni kwa mujibu wa sheria ya mtoto na. 21 ya mwaka 2009 na mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA), unaolenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii yetu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Matukio kama haya yamesababisha vifo vya wananchi (wanawake, wanaume, wazee na watoto) wasio na hatia kama vile mauaji ya vikongwe, watu wenye ualibino na sasa yanafanyika kwa watoto ambao hawana ulemavu. 

TGNP Mtandao, tunatambua jitihada za serikali ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa katika kukabiliana na suala hili, na kamati ya kuchunguza mauaji haya tayari imeundwa. Kwetu sisi tunaona ni jitihada nzuri pamoja na kwamba upelelezi unaendelea, tunashauri yafuatayo:-

Kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, ilete majibu hayaka iwezekanvyo, na taarifa ya uchunguzi ifanyiwe kazi kwa wakati ili kutokomeza kabisa mauaji haya.

Serikali na vyombo vya dola visimamie kikamilifu sheria ya kudhibiti uchawi na. 12 ya mwaka 1998(The Witchcraft Act). Ambayo imeainisha adhabu kwa watu wanaoendesha vitendo vya kishirikiana vinavyoweza kudhuru wengine.

Tunalitaka jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola kuhakikisha watoto wanakuwa salama kwa kuimarisha ulinzi katika maeneo yote yanayotajwa kuwa sio salama katika mkoa wa Njombe ili kuhakikisha watoto wanahudhuria masomo kikamilifu.

Tunaitaka jamii kutoa ulinzi wa mtoto kwani ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha ustawi wa watoto. Pia, serikali na wadau kuzijengea uwezo kamati za ulinzi wa watoto ili waweze kutimiza majukumu yao ikiwemo kubaini maeneo hatarishi katika kijiji/ mtaa na kupanga mikakati ya kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Imetolewa na



Lilian Liundi
Mkurugenzi Mtendaji
TGNP Mtandao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad