HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, January 27, 2019

Wanahabari shirikini kuijenga NHIF- Mziray

Na Grace Michael, Mtwara
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umewahimiza waandishi wa habari kushirikiana nao katika kuendelea kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya pamoja na kushiriki kuulinda Mfuko huo ili uweze kudumu na kunufaisha wengi.

Rai hiyo imetolewa na Meneja Mahusiano wa NHIF, Anjela Mziray wakati wa kikao kazi kilichofanyika mkoani Mtwara kikihusisha wanachama wa vyama vya waandishi wa habari katika Mikoa ya Lindi na Mtwara.

“Nawaomba sana ndugu zangu tuendelee kushirikiana katika kuhakikisha tunahamasisha wananchi kupitia vyombo vyetu ili waelewe na kutumia huduma za Mfuko huu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu lakini pia ili Mfuko uendelee kuwa imara tuendelee kuunganisha nguvu katika kuulinda Mfuko wetu,” alisema Mziray.

Alisema kuwa endapo wanahabari watashiriki vyema juhudi za Mfuko za kufikisha taarifa kwa wananchi zinazohusiana na umuhimu wa kutumia huduma za matibabu kwa mfumo wa bima, wananchi wengi wataweza kujiunga na hatimaye kuwa na uhakika wa kupata matibabu.

“Kwa sasa bima ya afya ndio suluhisho kwa huduma za matibabu kwa wananchi wetu na ili wafanikiwe kujiunga ni lazima tuhakikishe tunawafikia kwa njia mbalimbali ikiwemo ya elimu na uhamasishaji hivyo kama ambavyo mmekuwa wadau wazuri wa Mfuko tangu mwanzo tuendelee kuwafikia wananchi wetu kupitia program mbalimbali za uelimishaji,” alisema Bi. Mziray.

Kwa upande wa wanachama wa vyama vya waandishi wa habari katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, wameupongeza Mfuko kwa juhudi kubwa ambazo umefanya hususan za kuanzisha mpango wa Ushirika Afya ambao utawasaidia kwa kiwango kikubwa wakulima ambao awali hawakuwa na fursa hiyo.

“Mfuko umekuwa ni mkombozi mkubwa kwa afya za wananchi wengi tukiwemo na sisi waandishi wa habari, mfano mzuri sisi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara ni wanufaika na tumeweka kipaumbele sana katika suala hili kwa kuwa tunafahamu kabisa kuwa gharama za matibabu ni kubwa na bila bima ya afya ni ngumu mtu kumudu gharama hizo, hivyo niendelee pia kuwahamasisha wanahabari wa mikoa mingine kuhakikisha wanajiunga na Mfuko lakini pia kuendelea na uhamasishaji,” alisema Katibu wa Chama cha Waandishi wa Mkoa wa Lindi Bw. Christopher Lilai.

Mfuko umesema unaendelea na maboresho mbalimbali ya huduma zake ikiwemo kuongeza wigo wa wanachama kupitia makundi mbalimbali lakini pia upatikanaji wa huduma za matibabu kirahisi kupitia uimarishaji wa mifumo wa TEHAMA.
 Meneja Mahusiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Anjela Mziray akisisitiza jambo kwenye kikao kazi cha wanachama wa vyama vya waandishi wa habari mikoa ya Mtwara na Lindi.
 Meneja Uhusiano wa NHIF, Anjela Mziray akifafanua jambo, kulia kwake ni Kaimu Meneja wa Mkoa wa Mtwara, Gidion Katondo na Meneja wa Mkoa wa Lindi Bw. Emmanuel Mwikwabe, Kulia ni Wenyeviti wa Mtwara, Martina Ngulumbi na Christopher Lilai.
 Washiriki wa kikao kazi wakifuatilia mada juu ya shughuli zinazofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
 Wanachama wa vyama vya waandishi wa habari mikoa ya Lindi na Mtwara wakifuatilia ufafanuzi wa hoja mbalimbali.
 Sehemu ya wanachama hao wakifuatilia mada.
Meneja wa Mkoa wa Lindi Bw. Emmanuel Mwikwabe akiwasilisha mada ya maboresho yaliyofanywa na Mfuko.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad