HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 2 January 2019

Vituo vya Mafuta Vyakumbushwa Kuweka Mabango Yanayoonyesha Bei


Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Vituo vya mafuta nchini vimekumbushwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana ili kuepusha usumbufu unaojitokeza kwa wateja na kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Nzinyangwa Mchany wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu bei kikomo za mafuta aina ya petroli zilizoanza kutumika leo januari 2, 2019.

“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja, adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika”, alisema Mchany.

Mchany ameongeza kuwa mabango hayo yanatakiwa kuonesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika ili wateja waweze kuwa na uwanja mpana wa kuchagua wapi pa kununua.Aidha, Mchany ametoa rai kwa wateja kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.

Kwa upande mwingine wauzaji wa mafuta ya petroli wamekumbushwa kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine za EFPP (Electronic Fiscal Pump Printers) na wanunuzi wametakiwa kuhakikisha wanapokea stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.

Amefafanua kuwa Stakabadhi hizo za malipo zitatumika kudhibiti watoa huduma wasio waaminifu pale ambapo wanunuzi wa mafuta watakuwa na malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora kinachofaa, pia stakabadhi hizo zitasaidia kurahishisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na nishati mafuta.

Bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote zimepungua ambapo kwa mwezi Januari 2019, bei za rejareja za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimepungua kwa Shilingi 141/lita (sawa na asilimia 5.80), Shilingi 212/lita (sawa na asilimia 8.69) na Shilingi 167/lita (sawa na asilimia 7.03).

Vilevile, bei za jumla za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimepungua kwa Shilingi 140.81/lita (sawa na asilimia 6.09), Shilingi 212.12/lita (sawa na asilimia 9.14) na Shilingi 166.02/lita (sawa na asilimia 7.40).

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad