HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 30, 2019

KNCV, Muhimbili waboresha huduma kwa wagonjwa wa kifua kikuu

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo imekabidhiwa jengo la wagonjwa wa Kifua Kikuu (TB) lililokarabatiwa na mradi wa TB unaofadhiliwa na USAID chini ya Shirika la KNCV ili kusaidia wagonjwa wengi kutibiwa kwa wakati mmoja katika hospitali hiyo tofauti na awali.

Awali, wataalam wa Muhimbili walikuwa wakitoa huduma kwa wagonjwa sita hadi 10 kwa siku na kwa wiki walikuwa wakitibiwa wagonjwa 30 hadi 40. Lakini hivi sasa baada ya ukarabati wa jengo hilo wagonjwa 10 watakuwa wakilazwa kwa wakati mmoja na wangine 50 wa nje watakuwa wakitibiwa kila siku.

 Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko huo, Dkt. Vishnu Mahamba amesema ukarabati wa jengo hilo umegharimu TSh. milioni 69 na kwamba wametoa msaada wa ukarabati ili kuhakikisha wagonjwa wa kifua kikuu wanapata huduma bora.

Akizungumzia msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru alishukuru mfuko huo kwa kusaidia ukarabati wa jengo hilo  kwani litakuwa na manufaa kwa wagonjwa mbalimbali wanaotibiwa katika hospitali hiyo.

Pia, Prof. Museru aliagiza jengo hilo lianze kutumika mara moja baada ya kukabidhiwa kwa uongozi wa hospitali hiyo na kwamba wataalam wanapaswa kuweka mahitaji muhimu vikiwamo vitanda pamoja na vifaa vingine ili kuanza mara moja kwa huduma za matibabu.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani wa Muhimbili, Dkt. Amina Mgunya amesema kwamba jengo hilo watalitumia kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa ndani na nje wa kifua kikuu na wa kifua kikuu sugu.

Dkt. Mgunya amesema mbali na ukarabati wa jengo hilo, pia wagonjwa watakuwa wakipatiwa matibabu yote Muhimbili badala ya kupelekwa Hospitali ya Kibong’oto mkoani Kilamanjaro kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Kuanzia sasa wagonjwa wa kifua kikuu watakuwa wakipatiwa matibabu yote Muhimbili badala ya kupelekwa Kibong’oto kwa ajili ya matibabu zaidi,” amesema Dkt. Mgunya.

Naye Mkuu wa Idara ya Huduma za Uuguzi Muhimbili, Yassin Munguatosha amesema wamepokea agizo la Prof. Museru na kwamba agizo hilo watalitekeleza maramoja ili kuhakikisha wagonjwa wa kifua kikuu wanapatiwa matibabu katika jengo hilo.

Mbali na ukarabati wa jengo hilo, pia, Muhimbili imekarabati jengo lingine ambalo wataalam wa ugonjwa wa kifua kikuu watakuwa wanalitumia kutoa huduma.

Wagonjwa wa kifua kikuu wamekuwa wakionwa na wataalam katika Kituo cha Magonjwa Yanayoambukiza kwa njia ya hewa (IDC) na baadaye kupelekwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.

 Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
 Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akikata utepe ikiwa ishara ya kufungua  jengo la wagonjwa wa kifua kikuu lililokarabatiwa na mradi wa TB unaofadhiliwa na USAID chini ya Shirika la KNCV. Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Muhimbili, Dkt. Hedwiga Swai, katikati ni Ofisa Mradi wa Shirika la KNCV, Irene Mauya na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la KNCV, Dkt. Vishnu Mahamba.
  Ofisa Mradi wa Shirika la KNCV, Irene Mauya akitoa maelezo kuhusu mradi huo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Museru wa tatu kutoka kushoto. Wengine ni wataalam wa MNH wakimsikiliza ofisa huyo.
  Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani wa Muhimbili, Dkt. Amina Mgunya akitoa maelezo kwa Prof. Museru wa pili kushoto kuhusu matumizi ya jengo hilo.
 Mkuu wa Kitengo cha Majengo Muhimbili, Injinia Gama Kimoto akimweleza Prof. Museru kuhusu ukarabati wa jengo litakalotumiwa na wataalam wa kifua kikuu wakati wa kutoa tiba. Jengo hilo limekarabatiwa na Muhimbili.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Museru akizungumza na wataalam wa MNH  na maofisa mradi wa Shirika la KNCV kuhusu ukarabati na matumizi ya jengo hilo baada ya kukabidhiwa leo.
 Prof. Museru akiwa katika picha ya pamoja na wataalam wa MNH na maofisa mradi wa Shirika la KNCV. Nyuma ni jengo la wagonjwa wa kifua kikuu lililokarabatiwa na KNCV

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad