HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 15 January 2019

HESLB YAKUSANYA BILIONI 94.01 KWA NUSU MWAKA PEKEE

*Kuanza kuwasaka wadaiwa sugu na waajiri wanaokiuka sheria.
*Yajiunga rasmi na mfumo wa GePG

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu nchini (HESLB) imekusanya takribani shilingi bilioni 94.01 kutoka kwa wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu kwa kipindi cha Julai hadi Disemba mwaka 2018 na kufanya kuvuka malengo ya kukusanya shilingi bilioni71.4 waliyojiwekea kwa kipindi hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi mtendaji wa bodi ya mikopo nchini Abdul-Razaq Badru amesema kuwa makusanyo hayo yametoka kwa jumla ya wanufaika  198, 659 ambao wamejiajiri na kuajiriwa katika  sekta binafsi na za umma.

Badru amesema kuwa kwa kipindi cha Julai hadi Disemba mwaka 2018 walifanikiwa kuwabaini wanufaika wapya zaidi ya 12,600 ambao walikuwa hawajaanza kurejesha mikopo yao na sasa wameanza kurejesha na kufanya jumla ya wateja wanaorejesha mikopo kwa sasa kufikia 198, 656.

Aidha amesema kuwa makusanyo hayo ya bilioni 94.01 ni sawa na ongezeko la asilimia 8.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 85.87 zilizokusanywa katika kipindi cha Julai hadi Disemba mwaka 2017.

Vilevile amesema kuwa, "Malengo yetu kwa mwaka huu ni kukusanya shilingi bilioni 150 na tunatumaini malengo yetu yatafikiwa na tunawashukuru wateja wetu wanaorejesha mikopo na waajiri wanaotuunga mkono kwa kufuata masharti ya sheria" amesema Badru.

Kuhusiana na mfumo wa serikali wa ukusanyaji wa mapato (GePG) Badru amesema kuwa kuanzia sasa malipo yote kwenda HESLB  yatapokelewa kwa mfumo huo unaofuatwa na taasisi mbalimbali za serikali na kusisitiza kuwa  kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha HESLB waajiri wanapaswa kukata asilimia 15 ya mshahara ghafi kwa mnufaika na kuwasilisha makato hayo kwa HESLB ndani ya siku 14 baada ya tarehe ya mwisho wa mwezi wa makato.

Badru amesema kuwa, " Mwajiri au mnufaika anachotakiwa ni kunakiri namba  ya kumbukumbu iliyopo kwenye ankara  zao na kufanya malipo kwa njia za benki au simu na malipo hayo yatapokelewa kwa mfumo huo unaofuatwa na taasisi mbalimbali za serikali" ameeleza Badru.

Pia amesema kuwa hakuna malipo yatakayopokelewa bila kufuata mfumo huo na wateja wanaweza kupiga namba 065 748 536, 0621 870 172, 0620 714 421 na 0621 870 173 ili waweze kupatiwa majibu ya maswali yao kuhusiana na utaratibu huo.

Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha cha mifumo Wizara ya fedha Bazil Baligyuma amesema kuwa mfumo huo mpya wa malipo utawarahisishia wanufaika katika kulipa madeni yao pamoja na kuzuia upotevu wa fedha na kuweka uwazi katika ukusanyaji wa mapato hayo.

Amesema kuwa malipo hayo yanaweza kufanywa katika benki yoyote muhimu ni kuwa na namba ya kumbukumbu ambayo pia itamsaidia mnufaika kulipa mkopo wake kupitia simu ya mkononi kwa urahisi zaidi.

Mkurugenzi wa urejeshaji mikopo kutoka HESLB Ignatus Oscar amesema kuwa wamerahisha mfumo huo ambao umeonesha mafanikio makubwa kwa walipaji kutofuata huduma bodi ya mikopo au benki  kwa kuwafanya watumie ankara zao kupata huduma popote walipo kwa kutumia simu zao za mkononi.

Amesema kuwa takribani wadaiwa sugu laki moja na elfu tisa wanadaiwa zaidi  ya shilingi bilioni 290 na tayari bodi imejipanga, mapema mwezi huu wataanza kuwasaka wadaiwa hao wakishirikiana na mamlaka ya mapato nchini (TRA) na wadau mbalimbali.
Mkurugenzi wa bodi ya mikopo nchini (HESLB) Abdul-Razaq Badru (wa pili kushoto) akiwa na baadhi ya wawakilishi wa mabenki mara baada ya kuzindua mfumo wa serikali wa ukusanyaji wa mapato (GePG) leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad