HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 15 January 2019

NAIBU WAZIRI MASAUNI AYAONYA MAKAMPUNI BINAFSI YA ULINZI KUJIHUSISHA NA UHALIFU

Serikali imeziasa Kampuni Binafsi za Ulinzi kutoshiriki katika matukio ya uhalifu baada ya kuripotiwa mara kwa mara kwa walinzi wa kampuni hizo kupatikana na hatia ya uhalifu katika mahala pao pa kazi ikiwemo kuwaazima silaha wahalifu kwenda kufanya matukio ya uhalifu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Sekta ya Ulinzi Tanzania (TSIA), uliofanyika leo jijini Dodoma.

Amesema kampuni zinatakiwa kuongea na walinzi wao sambamba na kuongeza maslahi kwa walinzi hao ili wasiingie katika vishawishi hali itakayopelekea kutoshiriki katika matukio ya uhalifu sehemu zao za kazi.

“Baadhi ya walinzi wa kampuni mnazozisimamia wamekua wakishiriki katika uhalifu, wengine wameenda mbali zaidi kwa kuwaazima silaha wahalifu kwenda kufanyia uhalifu, jambo hili halikubaliki, sasa naziagiza kampuni zenye walinzi wa namna hii kuhakikisha vitendo hivi vinakoma mara moja,” alisema Masauni

Akizungumza kwa niaba ya Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Narcis Misama alisema wao kama jeshi wanawahakikishia wanachama hao wa sekta ya ulinzi ushirikiano utakaowasaidia kutimiza majukumu yao huku akiweka wazi jeshi kama jeshi haliwezi kuyafikia maeneo yote kwa wakati

“Nawashukuru sana kwani mmekua msaada muhimu kwa jeshi la polisi hasa pale uhalifu unapotokea maeneo mnayolinda, tumeweza kuwapata watuhumiwa wa matukio mbalimbali kupitia taarifa zenu pindi tu uhalifu unapotokea, nawaahidi ushirikiano kwa siku zijazo  zaidi ya mnaoupata kutoka kwa jeshi,” alisema SACP Misama

Akizungumza kwa niaba ya wanachama Mwenyekiti wa Chama cha Sekta ya Ulinzi Tanzania, Felix Kagisa aliiomba serikali ipitishe sharia zinazoongoza sekta ya ulinzi binafsi ili waweze kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na taratibu  za nchi.
 Naibu  Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza  wakati  wa  Ufunguzi  wa  Mkutano  Mkuu  wa  Chama  cha  Sekta ya Ulinzi Tanzania (TSIA), ambapo  aliwaasa viongozi wa kampuni hizo kuwadhibiti walinzi wao kutojihusisha na masuala ya uhalifu.Ufunguzi huo umefanyika leo,  jijini Dodoma.
 Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Narcis Misama akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Sekta ya Ulinzi Tanzania (TSIA), ambapo aliwahakikishia  wanachama  wa  chama  hicho  ushirikiano  kutoka  Jeshi la Polisi. Ufunguzi huo umefanyika leo, jijini Dodoma.
 Mdau  wa  Masuala  ya  Ulinzi, ambae  pia ni  Inspekta Jenerali Mstaafu, Said Mwema  akizungumza  wakati  wa  Mkutano  Mkuu  wa  Chama  cha Sekta  ya Ulinzi  Tanzania (TSIA).Ufunguzi  huo  umefanyika  leo,  jijini  Dodoma.
Wanachama mbalimbali wa Chama cha Sekta ya Ulinzi Tanzania (TSIA), wakimsikiliza  Mgeni  Rasmi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi  Hamad  Masauni (hayupo  pichani), wakati  wa  Mkutano  Mkuu  wa chama  hich, uliofanyika leo, jijini  Dodoma. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad