HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 7 December 2018

Takukuru: Wananchi toeni maarifa za maendeleo ya miradi


Wananchi wameombwa kutoa taarifa mapema kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa miradi ya maendeleo wanaoitilia shaka kugubikwa na ufisadi ili kuokoa matumizi mabaya ya fedha za umma. Akizungumza wakati wa kongamano la kujadili utatuzi wa changamoto ya maji, kuanzia ufuatiliaji wa rasilimali fedha na utekelezaji wake,  ufuatiliaji wa maji lililoandaliwa na asasi ya Pakacha Group na kufadhiliwa na The Foundation For Civil Society, Elly Makala, Mkuu wa dawati la Elimu kwa Umma  (Takukuru ) Wilaya ya Kinondoni amesema ikiwa wananchi watatoa taarifa mapema , itakuwa ni rahisi kuchukua hatua mapema.

“Tutaokoa fedha nyingi za serikali zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwemo miradi ya maji, Barabara na ujenzi wa vituo vya afya,” amesema Makala. Amesema takukuru ina majukumu mbalimbali, ikiwemo kutoa elimu ya madhara ya rushwa katika maendeleo ya nchi na wananchi wake. Hivyo ameongeza ni wajibu wa wananchi kushirikiana na viongozi kuanzia ngazi ya kata katika dhana nzima ya maendeleo, ikiwemo kuhoji mapato na matumizi ya miradi iliyomo maeneo yao.

Ameipongeza Pakacha kwa elimu wanayoitoa kwa wananchi wa Manispaa ya Ubungo juu ya ufuatiliaji ya miradi ya maji na dhana nzima ya ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi. Upatikanaji wa maji umekuwa na changamoto katika kata za Kwembe, Msigani na Kibamba, hivyo asasi ya Pakacha, kwa ufadhili wa The Foundation For Civil Society kulazimika kutoa elimu kwa wananchi juu ya ufuatiliaji na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Kongamano hilo lilishirikisha wananchi, wenyeviti,watendaji wa serikali za mitaa wakiwemo madiwani na mwakilishi wa mhandisi wa maji wa Manispaa ya Ubungo. Katibu wa Pakacha, Haroun Jongo amesema lengo la kongamano hilo ni kutoa msukumo kwa utelekezaji wa miradi ya maji kwa kuibua hoja kwa wananchi, baada ya Pakacha kuunda kamati iliyofuatilia kutokamilika kwa miradi ya maji iliyotengewa fedha kutoka serikali kuu kwa ajili ya kata zao. “Lengo ni kuleta jukwaa la majadiliano kati ya viongozi, wananchi na watendaji wa serikali za mitaa ili kutatua kero za maji kwa wananchi kupitia mfumo wa Pets.

Pets ni mfumo unaowezesha ufuatiliaji matumizi ya rasilimali za umma zinazotoka Serikali Kuu au halmashauri kwa maendeleo ya wananchi kuanzia ngazi za mitaa hadi kata na kuendelea. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad