HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 22, 2018

NAIBU KATIBU MKUU MSTAAFU WA WAZAZI AKABIDHI MIKOBA KWA NAIBU KATIBU MKUU MPYA

ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa jumuiya ya Wazazi Zanzibar,Najma Murtaza Giga, amemtaka Naibu Katibu Mkuu mpya wa jumuiya hiyo, Othman Ally, kuendeleza mabadiliko yaliofanyika ndani ya jumuiya ikiwemo kutunza na kuthibiti mali za jumuiya hiyo. Giga alisema jumuiya hiyo kwa sasa inaendana na mabadiliko hayo ambayo jumuiya imeshirikiana na chama katika kuzitunza mali hizo.

Alisema jumuiya hiyo kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi(CCM),kimefanikiwa kuwabaini na kuwatia nguvuni waliohusika na upotevu wa mali za jumuiya hiyo hivyo ni vyema kwendana na mabadiliko hayo. Mbali na hilo, Giga alisema jumuiya hiyo iko salama na kwamba hakuna tuhuma zozote zilizoikumba wanachama wa jumuiya katika suala la usaliti na mambo mengine.

Kauli hiyo ameitoa jana wakati akimkabidhi ofisi mjini Unguja ambapo alisema anamkabidhi jumuiya hiyo ikiwa katika hali ya usalama ikiwemo kutokuwepo kwa majungu na makundi. "Hali hii inatokana na kuwepo kwa upendo baina ya viongozi wa jumuiya hiyo ikumbukwe katika jumuiya hii hakuna viongozi waliopatikana na suala la usaliti wa tuhuma zozote zile," alisema

Naye Naibu Katibu Mkuu huyo mpya, Othman Ally alisema atahakikisha anaendeleza hatua zilizofanyika na uongozi uliopita kwa kuzingatia katiba na misingi ya jumuiya hiyo. Alisema jukumu lilokabidhiwa ni kubwa ikiwemo kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 CCM ina shinda na kwamba lazima wanachama wa jumuiya hiyo watoe ushirikiano ili kutekeleza azma ya ushindi wa chama katika uchaguzi huo.

"Tufanye kazi kwa ushirikiano tuache makundi,majungu na hata hivyo ninamshukuru Rais na Mwenyekiti wa Taifa John Magufuli kwa kuendelea kukijengea heshima chama,"alisema Aliongeza kuwa kazi ambayo ataendelea kufanya ni pamoja na kuhakikisha jumuiya hiyo inaongeza idadi ya wanachama katika CCM na kwamba hatokubaliana na kuwepo kwa makundi ndani ya jumuiya hiyo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Zanzibar wa CCM,Dk.Abdallah Sadala Juma 'Mabodi' aliwataka wanajumuiya na viongozi wa jumuiya hiyo kumpa ushirikiano Naibu Katibu Mkuu huyo mpya katika kutekeleza maendeleo ya CCM. Alisema jumuiya hiyo ni chachu,tegemeo kubwa kwa chama katika kusimamia maadili na mambo ya kisiasa hivyo wanachama wa jumuiya wanapaswa kuelewa kuwa jumuiya hiyo ina historia ndefu.

"Jumuiya hii ndio msimamizi wa kazi za chama hivyo tunatakiwa tumpe ushirikiano wa kutosha Naibu huyu mpya mimi nimefurahi kuwa tumempata mtu makini na tunakukaribisha katika utendaji kichama,"alisema.
 NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Ndugu Othman Ally Maulid akipokelewa na viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Wazazi Zanzibar mara baada ya kuwasili Zanzibar kwa mara ya kwanza toka alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
 NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Ndugu Othman Ally Maulid akiwapungia mkono Viongozi mbali mbali wa Jumuiya hiyo mara baada ya kuwasili katika Afisi Kuu ya Wazazi Zanzibar iliyopo mtaa wa Mpirani Kikwajuni Unguja.
 NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Ndugu Othman Ally Maulid akivishwa koja mara baada ya kuwasili Kisiwandui katika hafla ya mapokezi yake.
 VIONGOZI mbalimbali wa Jumuiya ya Wazazi wakisikiliza kwa makini nasaha mbali mbali zinazotolewa na Naibu Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Ndugu Othman Ally Maulid.
 NAIBU Katibu Mkuu Mstaafu wa Wazazi Ndugu Najma Giga akizungumza katika hafla ya mapokezi Naibu Katibu Mkuu mpya ndgugu Othman Ally Maulid katika Kikao cha kujitambulisha kwa viongozi na Watendaji wa ngazi mbali mbali za Jumuiya hiyo hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Ndugu Othman Ally Maulid akifafanua namna atakavyoongoza Jumuiya hiyo kwa kufuata Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la mwaka 2017.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad