HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 24 October 2018

THE DESK &CHAIR YATOA VIFAA TIBA VYA WALEMAVU WA MACHO

Na Baltazar Mashaka, Mwanza
SERIKALI mkoani Mwanza imepokea msaada wa vifaa tiba na upasuaji kwa walemavu wa macho vilivyotolewa na The Desk & Chair Foundation (TD & CF) Tawi la Tanzania.

Vifaa hivyo vitakavyotumika kwenye kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho wakati wa maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe yanayofanyika kitaifa jijini humu, vilipokelewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk. Philis Nyimbi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela.

Akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa The Desk & Cir Foundation Sibtain Meghjee alisema wanaunga mkono juhudi za serikali za kuhudumia jamii kwa kuwa taasisi hiyo inatambua watu wenye ulemavu wana changamoto nyingi zikiwemo kushindwa  kumudu gharama za matibabu.

“Taasisi hii inafanya shughuli za kusaidia jamii (walemavu,wagonjwa na masuala ya elimu),kulingana na mahitaji.Kwa changamoto za walemavu wa macho ni kushindwa kumudu gharama za tiba sababu ya ugumu wa kipato hivyo serikali iangalie jinsi ya kuwasidia wapate Bima ya Afya,”alisema Meghjee.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo Mongela alisema maadhimisho ya ya Fimbo Nyeupe ni kielelezo kuwa walemavu wana mchango mkubwa na ndiyo maana TEHAMA inawaelekeza kwenye Uchumi wa Viwanda kama ilivyo kauli mbiu.

Alisema vifaa hivyo vitahudumia wilaya saba za Mkoa wa Mwanza  na hivyo serikali imejipanga wananchi watakaojitokeza hawatakosa huduma kwenye maadhimisho hayo na kambi ya uchunguzi wa macho, watakaobainika watatibiwa kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou Toure.

“The Desk & Chair wameonyesha njia kwa kuendelea kusaidia serikali ya awamu ya tano ambayo wananchi wake wana changamoto nyingi na naamini vifaa hivi vitaleta afya na tija kwa wenye matatizo mkoani kwetu, hivyo wafadhili wengine wasisite kuunga mkono na kuchangia maendeleo yanayosistizwa na serikali,”alisema Mongela.

Aliishukuru taasisi hiyo kwa kazi kubwa yenye tija inayofanyika mkoani humu na kwamba vifaa alivyokabidhiwa vitasaidia wananchi wenye ulemavu na matatizo ya macho kama ilivyo Kauli Mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu “Mafunzo ya Tehama kwa wasioona ni nyenzo jumuishi katika uchumi wa viwanda.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Mkoa wa Mwanza (TLB) Musa Mashauri alieleza kuwa hawahitaji walemavu wa macho waongeze na ndiyo maana ya msaada huo wa vifaa tiba na upasuaji na anaamini Nyamagana itakuwa kitovu cha shughuli za walemavu wa macho.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Silas Wambura alisema vifaa tiba hivyo na vya upasuaji vina ubora unaohitajika,vitasaidia watu wenye matatizo wasiopungua 100.

Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni miwani ya macho 268,lensi 103 za macho, Eye pad sterile 98, miwani 51 ya kujikinga na mionzi ya jua, maji tiba,plasta roll 20,pamba roll 20, spirit lita 5, boksi mbili za Ophthalmic cannulas,mabomba ya sindano mbaimbali, visu 120 na nyembe za upasuaji,mipira mbalimbali ya vidoleni (gloves) wakati wa upasuaji,fimbo nyeupe 56 pamoja na   vifaa vingine.
 Mwenyekiti wa The Desk Chair Foundation Sibatain Meghjee akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa tiba vya macho na upasuaji kwa serikali ya Mkoa wa Mwanza. Kushoto wa kwanza ni Katibu Tawala Msaidizi Seif Rashid, wa pili ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagan Dk. Philis Nyimbi.
 Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Silas Wambura akizungumza kuhusu ubora wa vifaa hivyo kabla ya kukabidhiwa.
  Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk. Philis Nyimbi,akipokea vifaa tiba na upasuaji pamoja na fimbo nyeupe kutoka kwa Mwenyekiti wa Desk & Chair Foundation Sibtain Meghjee (kulia) kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela.
 Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk. Philis Nyimbi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akizungumza baada ya kupokea msaada wa fimbo nyeupe, vifaa tiba vya macho na upasuaji vilivyotolewa an The Desk & Chair Foundation.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Mkoa wa Mwanza (TLB) Musa Mashauri akitoa shukurani kwa Taasisi ya The Desk & Chair Foundation kwa msaada huo wa vifaa tiba vya macjo na upasuaji pamoja na fimbo nyeupe. Picha na Baltazar Mashaka

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad